UCHAMBUZI: Mafanikio ya Msuva iwe chachu kwa wengine

Muktasari:

·         Mafanikio anayoyapata Msuva kwa sasa ni matokeo ya kile alichojifunza kwa miaka yote akiwa ndani ya Moro United, Azam na Yanga. 

WIKI iliyopita mchezaji wa Kitanzania anayecheza Ligi Kuu ya Morocco, Simon Msuva aliteuliwa katika kikosi bora cha ligi hiyo kwa Novemba.

Winga huyo wa zamani wa Yanga, anayekipiga Difaa El Jadidi alijiunga na timu hiyo msimu huu wa 2017/2018. Ndani ya mwezi huo, Msuva alifunga mabao mawili na kusababisha matatu, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kuibeba timu yake iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo inayofahamika zaidi kama Batola.

Kwa miaka mingi ukiachilia mbali enzi za kina Sunday Manara ‘Computer’, ila kwa miaka ya hivi karibuni Watanzania tumekuwa na kiu kubwa ya kutaka kuona siku moja wachezaji wetu wakikipiga katika ligi kubwa barani Ulaya.

Kiu yetu kubwa ni kuona nyota wao wakicheza katika ligi maarufu na zenye mashabiki wengi katika kila kona ya dunia kama England, Italia, Ujerumani ama Hispania kama sio Ufaransa.

Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walipopata nafasi ya kukipiga TP Mazembe ilionekana kama vile njia imeanza kufunguka kwa nyota wa Tanzania kuanza kucheza nje ya nchi. Kwani siku zote mtu anapoanza kufanya kitu na kufanikiwa, basi na wengine huiga kwa kufanya kitu hichohicho ili nao wafike mbali kwa kutumia njia wanazopita wenzao.

Samatta aliendelea na kufanikiwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, Januari ya 2016 na baadaye kupata timu Ulaya, hivyo kuzidi kuonesha njia kwa vijana wengine wa Kitanzania.

Siku zote katika mafanikio ya mwanadamu huwa kuna somo la kujifunza, hivyo mapito ya wachezaji hawa waliyopitia kabla ya kufika huko walipo kwa sasa yana mafunzo makubwa kwa vijana wa Kitanzania wenye dhamira ya kutafuta nafasi ya kucheza ligi kubwa Ulaya ama katika nchi za Afrika kama Msuva.

Ukimwangalia Samatta aliyekuwa Mbagala Market utaiona tofauti kubwa na Samatta aliyekuwa Simba, kadhalika yule aliyecheza TP Mazembe na hata sasa anayekipiga Genk ya Ubelgiji, hakika utaona pia tofauti yao.

Kila alipokuwa akipiga hatua alikuwa akibadilika kulingana na hatua aliyofika kitu ambacho kimemfanya leo hii kuwepo hapo alipo kwani siku zote kipaji pekee sio sababu ya kumfanya mchezaji kufanikiwa katika soka.

Ingekuwa ni kipaji tu sote tunafahamu kuwa wapo vijana wengi wenye vipaji pengine mara mbili ya Samatta, lakini hawajaweza kufanikwa na kuwa wachezaji wakubwa wa kulipwa kama alivyo Samatta.

Kwa Msuva mapitio aliyopita yanaweza kuwa na mafunzo makubwa zaidi kuliko mapitio aliyopita Samatta kwani nyota huyo hakucheza kwa muda mrefu katika Ligi Kuu Bara wakati Msuva ameitumikia Yanga tangu mwaka 2012-2017.

Hivyo kwa miaka yote aliyokuwa akichezea Yanga kuna somo kubwa ambalo vijana wanaweza kujifunza kupitia kwake. Ikumbukwe kwa muda wote huo alipokuwa akikipiga Yanga alikuwa ndiye mchezaji aliyekuwa akiongoza kwa kuzomewa zaidi na mashabiki wa timu yake kuliko yeyote.

Lakini kitendo cha kuvumilia kebehi na manenio mengine yanayokera yakiwamo matusi na kuamua kuendelea kujifunza kwa muda wote huo kimewashinda vijana wengi sana wa rika lake waliowahi kupita njia kama aliyopitia Msuva.

Mafanikio anayoyapata Msuva kwa sasa ni matokeo ya kile alichojifunza kwa miaka yote akiwa ndani ya Moro United, Azam na Yanga. Nakumbuka siku moja tukiwa Uwanja wa Taifa, Vijana wa Jangwani ilipokuwa ikicheza mechi na mara kadhaa Msuva alikuwa akikosa mabao kutokana na mashabiki wa timu yake kumlaumu na kutoa maneno yasiyo ya kiungwana.

Kitu cha ajabu katika mechi hiyo, baadaye Msuva alifanikiwa kufunga bao na mashabiki wa Yanga wakalishangilia, kwani lilikuwa ni la ushindi.

Hivyo moja katika ya vitu vikubwa vilivyafanikisha safari ya Msuva hadi kufika hapo alipo, ikiwamo kuingia kwenye orodha ya wachezaji bora wa mwezi tena katika Ligi Kuu ya Morocco ni uvumilivu wake aliokuwa nao.

Pia, utayari wa kutaka kujifunza, kwani mtu unaweza kuwa mvumilivu lakini ukakosa utayari wa kutaka kujifunza, hivyo kushindwa kufanikiwa. Msuva anaonekana kuendeleza mafanikio kwa kuwa ana sifa ya uvumilivu na yupo tayari kufunza, hivyo ninategemea wachezaji wengine wa Kitanzania wanaokutana naye wanapoitwa katika kambi ya timu ya taifa wamepata mtu mwingine wa kujifunza kwao na kufuata nyayo za kuyaendea mafaniko.