Mabeki wenye rekodi za kufunga mara nyingi Ulaya

Muktasari:

  • Moja ya matokeo kwenye mechi hizo, Liverpool iliichapa Manchester City mabao 3-0 huko Anfield na sasa inasubiri tu kipute cha marudiano kitakachofanyika Etihad.

LONDON,ENGLAND


MECHI za kwanza za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zimeshapigwa. Kuna timu zimemaliza kabisa mechi hizo za kwanza na nyingine zinasubiri mechi za marudiano kufahamu hatima yao.

Moja ya matokeo kwenye mechi hizo, Liverpool iliichapa Manchester City mabao 3-0 huko Anfield na sasa inasubiri tu kipute cha marudiano kitakachofanyika Etihad.

Lakini katika kufurahia michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuna mabeki wameweka rekodi kwa kufunga mara mbili katika michuano hiyo. Hawa hapa mabeki wenye rekodi za kupasia nyavu mara nyingi kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

5. Sergio Ramos- mabao 11

Nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos amecheza mechi 111 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mhispaniola huyo, ambaye ni beki wa kati anayecheza kwa kiwango kikubwa kwenye michuano ya Ulaya kwa miaka ya karibuni. Ni kiongozi bora wa ndani ya uwanja na ndio maana katika rekodi zake amekuwa mmoja kati ya mabeki waliofunga mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, akifunga mabao 11 akiwa na kikosi cha Los Blancos.

Moja kati ya mabao yake yanayokumbukwa ni lile la kusawazisha kwenye fainali dhidi ya Atletico Madrid na kushinda mechi hiyo. Beki mwingine aliyefunga mabao 11 kwenye michuano ya Ulaya ni beki wa zamani wa Real Madrid na AS Roma, Christian Panucci.

4. Gerard Pique- mabao 12

Barcelona iliichapa AS Roma 4-1 katika robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Camp Nou usiku wa Jumatano iliyopita.

Katika mechi hiyo, beki wa kati Gerrard Pique alitikisa nyavu wakati alipofunga katika dakika 59 na kuifanya Barcelona kuongoza kwa mabao 3-0. Bao hilo lilimfanya Pique afikishe mabao 12 katika michuano hiyo ya Ulaya baada ya kucheza mechi 101.

3. Dani Alves- mabao 12

Paris Saint-Germain ilimsajili Dani Alves katika majira ya kiangazi mwaka jana akitokea Juventus. Beki huyo wa pembeni wa zamani wa Barcelona na Sevilla ni matata sana anapokwenda mbele kushambulia. Mbrazili huyo alifunga mabao 12 katika mechi 152 alizocheza kwenye michuano ya Ulaya.

PSG imeshindwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini msimu ujao mambo yanaweza kuwa tofauti na Alves anaweza kuboresha rekodi yake.

2. Ivan Helguera- mabao 15

Mmoja kati ya mabeki waliokuwa matata ndani ya uwanja ni Ivan Helguera, ambaye alikuwa beki wa Los Blancos kuanzia mwaka 2000 hadi 2007. Kwenye michuano ya Ulaya amecheza mechi 97 na kufunga mabao 15. Kutokana na hilo, Sergio Ramos ana kazi nzito ya kuwazidi mabeki wawili wa kati katika kufikia rekodi ya kuwa kinara wa mabao kwa michuano hiyo ya Ulaya huko Madrid.

1. Roberto Carlos- mabao 16

Roberto Carlos ameweka heshima duniani akiwa beki wa kushoto bora duniani. Gwiji huyo Mbrazili amefunga mabao 16 Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa nyakati zake alizokuwa akiichezea Real Madrid na msimu mmoja huko Inter Milan. Alikuwamo kwenye kikosi cha Brazil kilichobeba ubingwa wa wa Kombe la Dunia 2002.