MIPANGO TU-Pep huchungulia mbinu za wapinzani kabla ya kuingiza kikosi chake uwanjani

Muktasari:

  • Baadaye Pep akawa na dakika zake tano za kufurahia ushindi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kwa mara nyingine akaanza kuangalia mambo yajayo.

TOLEO lililopita kwenye Kitabu cha Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau alielezea kwa mara nyingine utaratibu wa Kocha Pep Guardiola kutopenda kuonyesha furaha ya ushindi mbele ya waandishi wa habari, badala yake anazungumzia matatizo ya hapa na pale aliyoyabaini wakati wa mechi na Stuttgart na kufurahia ushindi baadaye. Endelea…

“Pep tuhakikishe hatufanyi kosa lilelile walilofanya kabla yetu,’’ aliongeza Domenec Torrent.

“Hatuwezi kumuingiza mchezaji akimbie tu uwanjani kwa lengo la kuvunja rekodi kadhaa.

Baadaye Pep akawa na dakika zake tano za kufurahia ushindi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kwa mara nyingine akaanza kuangalia mambo yajayo.

Pep analalamika kwa sauti ya juu: “Miguu yangu imekuwa kama barafu, hapa kuna baridi kali hatari!”

Kilichotokea Stuttgart na ule ushindi wa dakika za majeruhi kwa sasa ni mambo yaliyopita. Thiago amepongezwa na magazeti katika kurasa za mbele lakini kwa Pep huu ni wakati wa kurudi katika taratibu zake za kawaida.

Kuna timu pinzani mpya ya kukabiliana nayo na Pep anataka kumfanyia tathmini mpinzani huyo na kujiandaa na mikakati ya kumuwezesha kupata ushindi.

Kama ilivyo ada yake, Pep ana utaratibu wa kufanya mazungumzo na timu yake mara tatu kabla ya mechi, kila mazungumzo yanachukua dakika 15, anatumia picha kufafanua pointi yake hasahasa picha za video ambazo hazichukui zaidi ya dakika saba, mazungumzo yote yanahusisha utaratibu huohuo.

Siku moja kabla ya mechi Pep huwa anatumia muda kuchambua nguvu yao katika kufanya mashambulizi, kwa kuumia video hizo anabaini ni vipi timu hiyo ni hatari, anakuwa makini kwa namna ambavyo wachezaji wao muhimu wanavyojipanga na kucheza.

Baada ya hapo Pep huwapa maelekezo maalumu wachezaji wake kuhusu safu ya ulinzi itakavyocheza ili kuwasimamisha wapinzani wao, kinachofuata ni kwa wachezaji kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwenye mazoezi yanayofuata.

Maelekezo mengine huyatoa siku ya mechi kabla ya mazoezi ya asubuhi ya siku ya mechi, hapo kutakuwa na maelekezo ya kina kuhusu ni vipi watatumia safu ya ulinzi na ushambuliaji katika mipira ya kurusha na ile ya adhabu ndogo.

Kocha Msaidizi, Torrent anakuwa tayari amezichambua kona 50 za mechi zilizopita za wapinzani wao na kuelezea kitu chochote muhimu ambacho wanakijaribu mara kwa mara.

Torrent atakumbusha nafasi tofauti wanazohitaji kuzitumia kutengeneza mashambulizi kabla ya kwenda kwenye mechi, baada ya mazungumzo hayo timu inafanya mazoezi mepesi ambayo hapohapo wanahusisha namna ya kujipanga kushambulia na kuzuia mashambulizi.

Hadi hapo Pep anakuwa hajaamua kuhusu kikosi chake cha kwanza kwa hiyo kila mmoja anawajibika kujihusisha kikamilifu katika mazoezi, kama ni mechi ya ugenini hawafanyi hayo badala yake wanarudia kuangalia video walizotumia kufanya mazoezi ya kupiga mipira ya adhabu.

Pep anatoa maelekezo ya tatu na ya mwisho saa mbili kabla ya mechi wakati wakiwa hotelini (huwa hapendi kufanya hili wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo), mazungumzo ya hapo unaweza kuyaita ni mazungumzo ya kuwahamasisha wachezaji lakini pia yanahusisha uchambuzi wa mbinu za Bayern katika kushambulia.

Huo pia ndio wakati ambao Pep atawaambia wachezaji wake ni nani na nani watakaokuwa katika kikosi chake cha kwanza kitakachoanza katika mechi hiyo. Hadi hapo wachezaji wanakuwa tayari wanajua nini kinafuata.

Mazungumzo hayo moja kwa moja yanahusu kushambulia, yanakwenda moja kwa moja kujadili ni vipi wataitumia kona ya kwanza au mpira wa adhabu utakaopigiwa pembeni, yote hayo yatachambuliwa na kocha.

Kwa kawaida ingawa si mara zote, Pep pia atayatumia mazungumzo hayo kama njia ya kuwahamasisha wachezaji wake, mfano katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester United, Pep mapema Aprili, Pep hakuwa na mazungumzo ya mara ya tatu.

Katika tukio hilo alikuwa tayari ameshaitangaza timu ya kikosi cha kwanza siku moja kabla, tayari walishafanyia mazoezi namna timu itakavyoshambulia na akaona hakukuwa na jambo la zaidi ambalo angeliongeza.

Itaendelea Jumanne ijayo…