MACHO MANNE: Aah! Hizi sasa ni vurugu usajili Ligi Kuu Bara

Mwanahiba Richard

Muktasari:

Hata hivyo, kabla dirisha hilo halijafunguliwa, tumezishuhudia timu kama Singida United, Simba, Azam, Yanga na Kagera Sugar, zikiwa zimeshaanza usajili wao kimya kimya.

DIRISHA la usajili linafunguliwa leo Alhamisi na litafungwa Agosti 6 ambapo ndani ya muda huo, klabu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kwa Tanzania Bara zinatakiwa kusajli wachezaji wanaotarajiwa kuwa na mabadiliko chanya kwenye vikosi vyao.

Hata hivyo, kabla dirisha hilo halijafunguliwa, tumezishuhudia timu kama Singida United, Simba, Azam, Yanga na Kagera Sugar, zikiwa zimeshaanza usajili wao kimya kimya.

Mashabiki na wadau wengi wa soka walikuwa wanajiuliza ni vipi usajili huo umeanza mapema kabla ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kufungua rasmi dirisha husika? Hata hivyo, jibu lake ni rahisi tu, pengine wachezaji walisaini mikataba ya awali ya ajira yao.

Miaka ya nyuma tulizoea Simba na Yanga zikipigana vikumbo katika usajili, hata hivyo, kwa sasa upinzani umeongezeka baada ya Azam nayo kuingia kwenye vita hiyo ya usajili ambao imefanya vurugu kama mara tatu kwa kusajili wachezaji waliokuwa tayari wamefanya mazungumzo na Yanga, Mbaraka Yusuph, Waziri Junior na Salmin Hoza. Kitendo hicho kimewaumiza Yanga ambao awali walipokonywa mchezaji Jamal Mwambeleko.

Tatizo kubwa la Yanga ni ukata unaowakabili baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kujiuzulu. Jeuri ya fedha sasa imetawala ndani ya Simba na Azam tu ambao wanaonekana wamepania kufanya maajabu msimu ujao hasa Simba iliyokata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani kumaliza kiu ya miaka mitano ya kuikosa michuanp ya kimataifa.

Ukiachana na zile klabu ambazo zipo chini ya taasisi ama kampuni, lakini kuna klabu ambazo zinamilikiwa na wanachama ambazo sasa zenyewe zinakuwa kama hazijielewi kwa mambo kadhaa, hazina nguvu ya pesa, wachezji wao wengi mikataba yao imamalizika, hivyo wana kazi ya kufanya upya mazungumzo, ambayo kwa asilimia kubwa ni makavu kwani usajili wao utakuwa wa mkopo.

Hakuna pesa kwenye klabu hizo, wachezaji wazuri wanachukuliwa na Simba na Azam, hivyo hapo ni kutoa ahadi ili kutimiza usajili wa mali kauli na wachezaji wengi wamekuwa wakikubali pia.

Wanakubaliana na hilo kwa sababu tu hawana pa kwenda, nafasi kwenye timu zenye uhakika zimejaa.

Dirisha sasa limefunguliwa hakutakuwa na kificho katika usajili, viongozi watakuwa na mwendo wa kupigana vikumbo kama ilivyokuwa kwa nyota kadhaa waliosajiliwa tayari kina Shomary Kapombe, Mbaraka, Hoza na Waziri Jr.

Bado usajili wa kushitukiza utaendelea na utawashangaza watu, wengine wanaweza kukata tamaa na timu zao, nyota wa maana wataondoka kwenye vikosi vyao, wachezaji ambao wana umuhimu kwao, ni lazima watu walie kwenye usajili wa msimu huu kutokana na vurugu za ‘Mafia wa Usajili’.