MAKALA: Simba imeanza kupotea taratibu

OKWI

UNAKWENDA mwaka wa sita sasa Simba ikiwa haijaonja ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL). Mtoto aliyezaliwa mwaka 2012 Simba ilipotwaa ubingwa wa mwisho tayari ameanza masomo ya darasa la kwanza.

Katika kipindi hicho Simba haikuwa na jipya sana zaidi mwaka jana kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kupitia Kombe la FA, baada ya kuifunga Mbao FC mabao 2-1.

Wakati mashabiki wa Simba wakiendelea kukata tamaa, mambo yalionekana kuwa tofauti msimu huu. Mashabiki hao walipata matumaini kupitia usajili  wa kujiandaa na msimu ambapo timu hiyo ilichukua mastaa wenye majina makubwa ndani na nje ya nchi.

Majina makubwa kama Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, John Bocco, Aishi Manula na wengineo kwa imani kwamba watawapa raha kwa kwenda mbele. Pia wakiamini hakutakuwa na kikwazo cha kuchukua ubingwa msimu huu.

Hata hivyo kuna kitu hakiendi sawa Msimbazi. Tayari baadhi ya mambo Simba inaonekana kupata wakati mgumu, na wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakiambulia maumivu badala ya shangwe walizoanza nazo mwanzo wa msimu.

Imefeli FA,Mapinduzi

Simba imechemka kuwania taji la Kombe la FA na Mapinduzi na kujikuta wakibakiza nafasi moja ya kupambana na ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu huu. Pia, Simba ina nafasi katika kombe la Shirikisho Afrika ambalo watashiriki.

Ugumu kwenye Ligi Kuu ni kwamba ushindani ni mkubwa hasa kutoka kwa timu za Azam na Singida United bila kuwasahau Yanga ambao ndiyo watetezi wa taji hilo.

Mastaa wa zamani wa timu hiyo, wamekishauri kikosi cha Wanamsimbazi kutuliza akili zao katika mechi za Ligi Kuu na kwamba ndio fursa pekee iliyobakia kwao kuhakikisha mwaka 2018 hawatoki patupu.

Mussa Hassan ‘Mgosi’ ni nyota wa zamani wa timu hiyo na sasa anakinoa kikosi cha Simba B, anasema bado wachezaji wana nafasi ya kupambania ubingwa na waache kufikiria yaliopita.

“Si wakati wa kushikana mashati, badala yake wajipange kutumia fursa ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo waandae nguvu na akili zao kuhakikisha wanatimiza malengo ya timu,” anasema.

Kwa upande wa Ulimboka Mwakingwe amewataka Wanamsimbazi kujua wapo nyakati za vita na hawatakiwi kuangalia nyuma badala yake watazame mbele hasa juu ya namna ya kuwavua ubingwa Yanga.

“Ikitokea Azam ama Yanga, mmojawapo akatolewa kuwania ubingwa wa FA, basi shughuli itahamia kwenye Ligi Kuu, lazima wachezaji wa Simba, watambue kwamba huu mwaka kwao ni wakutoa jasho,” anasema.

Pesa zimechomeka

Simba ndio klabu iliyosajili kikosi ghali msimu huu, hasa kwa kuwachukua mastaa wenye majina makubwa kwenye soka kama Emmanuel Okwi, John Bocco, Haruna Niyonzima na Shomary Kapombe.

Hilo liliwafanya wapenzi wa klabu hiyo,kuamini kwamba msimu huu utakuwa wa furaha kwao, tofauti na wanachokivuna kwa sasa kama kutolewa kuwania Kombe la Fa na Mapinduzi.

Jambo hilo limefanya baadhi ya mashabiki waanze kunung’unika kama usajili wa Niyonzima ulikuwa wa kisiasa kwani hapakuwa na haja ya kumchukua kwa kuwa ndani ya kikosi hicho kuna mlundikano wa viungo.

Uzalendo, Nidhamu

Kuna wasiwasi mkubwa kuwa nyota wengi wa Simba wanakosa