MAJEMBE: Mabeki wa kati visiki VPL

Muktasari:

· Makala haya yanakuletea orodha ya mabeki 10 wa kati wakali zaidi ndani ya VPL, watu wa kazi.

MCHEZO wa soka sio lelemama. Unahitaji kuwa mwanamume wa shoka ili kuweza kucheza kwa kiwango kikubwa, hasa katika nafasi za ulinzi.

Hata kama ni mwanasoka wa kike ni lazima naye awe wa shoka vilevile. Kazi ya kucheza kama beki haijawahi kumwacha mtu salama.

Mabeki ni watu wa kazi, ni kama tu walivyo walinzi wa nyumba ama mali za watu, lazima awe mkakamavu, jasiri na asiye na nyoyo za uoga.

Ndani ya Ligi Kuu Bara kuna wanaume mashine bwana! Yaani watu wa kazi. Kuna mabeki wa kati ambao ukipambana nao lazima uwe umekula na kushiba.

Makala haya yanakuletea orodha ya mabeki 10 wa kati wakali zaidi ndani ya VPL, watu wa kazi.

YAKUBU MOHAMMED, AZAM FC

Beki katili zaidi Ligi Kuu Bara. Beki mmoja hivi mwenye rasta fupi na ndevu nyingi. Ni mtu wa kazi kwelikweli.

Kama ulikuwa hujui, beki huyu Mghana ndiye aliyeziba nafasi ya Sergie Wawa Azam na mpaka leo pengo lake limebaki historia.

Amekuwa makini katika kucheza mipira ya juu na chini, anatoka kwa hesabu na anahakikisha safu nzima ya ulinzi inajipanga. Ni nguzo kubwa katika kiwango cha Azam FC msimu huu na mpaka sasa wameruhusu mabao matatu tu. Azam ilimtaja kama mchezaji bora wa mwezi Agosti.

ASANTE KWASI, LIPULI

Ukiwauliza mashabiki wote wa Lipuli, watakwambia Asante Kwasi ndiye mchezaji wao bora wa msimu huu. Si kwa bahati mbaya. Beki huyo raia wa Ghana hana utani kabisa na washambuliaji wa timu pinzani.

Kwa hesabu zake ni ama mtu apite mpira ubaki, ama vibaki vyote. Ni mara chache sana kumwona anafanya makosa. Anacheza pia mipira  ya juu na chini kwa ufasaha.

Uzuri zaidi, anajua pia kufunga, msimu huu tayari amefunga mabao manne na kutengeneza moja. Siyo beki wa mchezo ati.

KELVIN YONDANI, YANGA

Hakuna ubishi ndiye beki bora zaidi mzawa kwa sasa. Katika umri wake wa miaka 33 bado ameendelea kuwa beki wa viwango vya juu. Ni mtu wa kazi muda wote.

Licha ya kimo chake kifupi, Yondani amejipambanua kuwa mlinzi bora wa kati. Anacheza vizuri mipira ya chini na anapandisha timu. Kwenye mipira ya juu siyo mzuri sana, lakini bado amekuwa imara. Ni wazi kazi yake ndani ya Yanga haina mashaka kabisa.

JUUKO MURSHID, SIMBA

Beki mwingine aliyejipambanua vizuri nchini ni Juuko Murshid wa Simba. Beki huyu raia wa Uganda anasifika kwa soka la kazi na la kibabe, hasa kwa washambuliaji wenye mbwembwe nyingi.

Kwa Juuko ukitaka kumpiga chenga lazima ujiulize mara mbili. Kwanza, hapendi kabisa kuletewa ujuaji na washambuliaji. Pamoja na kwamba wakati mwingine anafanya makosa madogo madogo, bado ni beki wa viwango vya juu.

AGGREY MORRIS, AZAM

Huwezi kutaja mabeki wa kati wa viwango vya juu nchini bila kumtaja Aggrey Morris wa Azam. Mwanamume huyo wa shoka kwanza yuko fiti vilivyo. Ukigongana naye tu unaweza kwenda kulazwa hospitali.

Mbali na kutandaza kandanda safi, kukaba na kuhakikisha usalama katika timu yake, Morris pia ana soka la kibabe. Wachezaji Emmanuel Okwi na Abaslim Chidiebele kwa nyakati tofauti waliponea hospitali baada ya kugongana na Morris uwanjani.

YUSUPH NDIKUMANA, MBAO FC

Huwezi kuitaja Mbao FC bila kumzungumzia nahodha wake, Yusuph Ndikumana. Beki huyo Mrundi anaupiga mpira mwingi pale Mwanza mpaka unamwagika. Ana hesabu nzuri za mipira ya juu na chini.

Amekuwa kiongozi si tu wa safu ya ulinzi ya Mbao, bali timu nzima. Msimu uliopita alicheza kwa kiwango bora na kuzivutia timu za Simba na Yanga.

TUMBA LUI, MAJIMAJI

Beki mwingine wa viwango vya juu yuko pale Majimaji, Songea. Anafanya kazi ya maana kwenye kukaba. Pamoja na kwamba Majimaji haiko katika kiwango bora, Tumba ameendelea kujipambanua kuwa mlinzi bora.

Nyota huyo wa zamani wa  Azam na Mbeya City, licha ya kwamba hachezi soka la kibabe, siyo mtu wa kupitika kirahisi. Anakaba vilivyo. Anaipanga pia safu ya ulinzi ya timu hiyo kwa umakini mkubwa. Amekuwa pia msingi mkubwa timu hiyo ya Songea, akijihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

KENNEDY JUMA, SINGIDA

Kwa mara ya kwanza ameitwa kwenye timu ya Taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars iliyopo kule nchini Kenya inakoshiriki michuano ya Chalenji. Kennedy Juma amepanda na kuwa mlinzi bora wa kati msimu huu, kutokana na namna anavyoipambania timu yake ya Singida United.

Amekuwa na umakini mkubwa uwanjani. Anacheza vizuri mipira ya juu, japo chini bado ana changamoto kidogo. Pamoja na mapungufu yake, ni beki wa viwango. Beki anayeaminiwa na kocha Mholanzi, Hans Van Pluijm siyo wa kiwango cha kidogo.

DICKSON JOB, MTIBWA SUGAR

Umewahi kujiuliza inawezekanaje Mtibwa Sugar imeendelea kuwa na safu ngumu ya ulinzi licha ya kuondoka kwa Andrew Vincent ‘Dante’ na Salim Mbonde ambao ndiyo walikuwa nyota tegemeo wa nafasi za ulinzi? Jibu ni jepesi, yupo Dickson Job.

Beki huyo mzawa amekuwa na kiwango cha kuvutia msimu huu. Anacheza vizuri katika mechi ndogo na kubwa. Ni mara chache kumwona anafanya makosa, hasa ya kizembe. Siyo bure kwamba Mtibwa Sugar imeruhusu mabao manne tu MPAKA SASA.

NURDIN CHONA, PRISONS

Beki mwingine anayeendelea kuwa bora nchini ni Nurdin Chona wa Prisons. Chona amekuwa Prisons kwa miaka zaidi  ya mitano sasa, huku akiendelea kujipambanua kuwa mchezaji bora. Nafasi yake katika kikosi cha kwanza haijawahi kupata mpinzani.

Ni beki fulani mbabe hivi. Anacheza soka la kazi. Ni mzuri zaidi katika mipira ya juu, japo si haba sana katika mipira ya chini pia.

ANDREW VINCENT, YANGA

Orodha hii inakamilishwa na Dante wa Yanga. Beki mmoja mfupi mwenye uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu. Ukimtazama Dante na kazi anayofanya uwanjani huwezi kuamini.

Amekuwa na kiwango bora msimu huu akianza karibu mechi zote za Yanga. Ni mpambanaji na ni mara chache kuona anafanya makosa.