Liverpool ya 2005 kila mtu kimpango wake

MIAKA inakwenda mbio sana. Nyakati nazo zinakwenda kwa kasi hiyohiyo. Hii leo unaweza usiwe na kitu cha kuizungumzia Liverpool, lakini miaka 12 iliyopita wababe hao wa Anfield walifanya maajabu huko

Uturuki.

Ilikuwa kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool na AC Milan na hadi mapumziko, wababe hao wa Anfield walikuwa wamepigwa 3-0. Ndiyo, Tatu Bila.

Kipindi cha pili bana, Liverpool chini ya kocha wake, Rafa Benitez, ndiyo huyu huyu Benitez kocha wa Newcastle United kwa sasa, ikachomoa bao zote hizo na kushinda kwa penalti kuwafanya wakali hao wa Merseyside kuwa mabingwa wa Ulaya katika msimu wa 2004/2005.

Wako wapi wale wanaume wa Anfield waliouteka usiku huo wa Ulaya huko Istanbul, Uturuki?

Jerzy Dudek - Kipa

Huenda hakuwa mtu sahihi kusimama katikati ya ile milingoti miwili.

Wengi hawakuwa na imani Jerzy Dudek, lakini ushujaa aliounyesha wakati kupigiana penalti utamfanya azidi kukumbukwa na pengine jina lake kuandikwa katika orodha ya mashujaa wa Liverpool.

Miguu ya kipa huyu ndio iliyoibeba Liverpool. Aliweza kupangua mashuti ya Serginho na Andrea Pirlo kabla ya kuamsha shangwe alipomvimbia Andry Shevchenko na kumnyima fursa ya kuipa AC Milan ubingwa. Miaka 12 baadaye, unajua ni wapi aliko Dudek na anafanya nini? Amini usiamini baada ya kustaafu kabumbu, Dudek hakuishia hapo. Ameendelea kushangaza wengi kutokana na kipaji chake.

Hivi sasa anaishi maisha tofauti kabisa. Anaishi katika ukurasa mwengine wa historia ya maisha yake. Dudek anaendelea kuonyesha uwezo wake michezoni ila kwa sasa sio katika soka, bali ni dereva wa magari ya mashindano, maarufu kama ‘safari rally’.

Ndio, Dudek anaendesha magari ya mashindano na mpaka sasa ameshashiriki mashindano 33 na amewahi kushinda mara moja!

Steve Finnan – Beki wa kulia

Steve Finnan mwanzoni hakuwa akifahamika. Alianzia chini akapanda fasta na kufikia hatua ya kukaa meza kuu pamoja na wakuu. Alianzia

soka lake katika klabu ya Welling United kabla ya kusajiliwa na

Liverpool.

Baada ya hapo alichokifanya uwanjani kila mmoja anakifahamu. Alitundika daluga mwaka 2010 baada ya kuiongoza Portsmouth dhidi ya

Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA. Tangu hapo hajaonekana tena

katika soka na hivi sasa, raia huyo wa Ireland anajishughulisha na kazi ya usanifu wa majengo jijini London.

Jamie Carragher – Beki wa kati

Hili liko wazi. Kila mmoja anafahamu aliko na anachokifanya beki huyu

wa kati tangu atangaze kutundika daluga. Jamie Carragher anafanya kazi Sky Sports pamoja na gwiji wa Man United, Gary Neville kama wachambuzi wa soka.

Wapo wanaohisi nyota huyu hakustahili kuingia katika fani ya uchambuzi na badala yake alipaswa kuelekea katika ukufunzi wa soka.

Sababu kuu ni kwamba umahiri, uzoefu na utulivu aliokuwa nao uwanjani unaweza kumfanya awe kocha bora pengine hata zaidi ya Zinedine Zidane, Pep Guardiola na Jose Mourinho.

Sami Hyypia – Beki wa kati

Hadi kufikia tamati ya fanaili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2005 alikuwa amebakisha siku chache kuadhimisha miaka 32 ya kuzaliwa.

Kutokana na umri wake mkubwa ilikuwa ni dhahiri kuwa Sami Hyypia asingeweza kucheza dakika 90.

Lakini cha kushangaza ni kwamba, beki huyu wa kati alipiga dakika 120 na kuishuhudia Liverpool ikibeba ndoo. Mwaka 2010, akaamua kustaafu soka ambapo aligeukia ukocha. Hata hivyo, mpaka leo ameshindwa kufanya la maana. Amefundisha klabu ya Bayer Leverkusen, Brighton na FC Zurich. Alichoambulia ni kuishusha daraja klabu ya FC Zurich katika msimu wa 2014.

Kwa sasa hana timu lakini kuna kila dalili kuwa hivi karibuni atapata klabu ya kufundisha.

Djimi Traore – Beki wa kushoto

Huyu hata hakutarajiwa kuwepo katika kikosi cha timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa achilia mbali kucheza mechi ya fainali na isitoshe kuwepo katika kikosi cha Rafael Benitez.

Djimi Traore anakumbukwa kwa kitu kimoja tu, uzembe alioufanya katika historia yake ya kusakata kabumbu. Kujifunga tena kwa kupiga kisigino.

Haikushangaza sana baada ya mechi hiyo ya fainali, raia huyu wa Mali, alionyeshwa mlango wa kutokea pale Anfield. Akaelekea Charlton Athletic, kisha Portsmouth, Monaco, Marseille kabla ya kujikuta  Marekani katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, MLS.

Jambo la kushangaza zaidi kuhusu maisha ya mwanasoka huyu ni kwamba, licha ya kutofanya mambo makubwa katika enzi zake uchezaji, mwaka 2015 alipewa kazi ya kocha msaidizi akimsaidia Brian Schmelter.

Xabi Alonso– Kiungo wa kati

Nani asiyemfahamu Xabi Alonso? Kushinda taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2005 akiwa na Liverpool ilikuwa ni mwanzo tu safari ya Mhispania huyu katika soka.

Mwaka 2009, akatimkia Real Madrid baada ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa kuvutiwa naye.

Mwaka mmoja baadaye akatwaa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Hispania.

Miaka miwili baadaye akabeba ndoo ya La Liga. Miaka miwili mingine mbele akabeba Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine tena.

Pep Guardiola akaweka pesa mezani, fasta sana mabosi wa Madrid wakamruhusu aondoke wakihisi nyota huyu anaanza kushuka kiwango.

Akahamia Allianz Arena. Mwaka huu alitangaza rasmi kustaafu soka baada ya kuiongoza Bayern Munich kutwaa taji la Bundesliga.

Luis Garcia – Winga wa kulia

Huyu ndiye aliyefunga lile bao la dhahabu lililorudisha uhai katikakambi ya Liverpool katika usiku ule wa Istanbul.

Luis Garcia, hakuwa na nguvu za giza, lakini uwezo wa kufunga mabao tena katika mazingira magumu, uliwafanya wengi wamuone kama mchawi.

Baada ya kuondoka Anfield mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 29, hakukaa tu, aliendelea kufanya kazi yake akichezea klabu nyingine saba katika nyakati tofauti. Klabu yake ya mwisho ni Coast Mariners. Mwaka 2016, aliichezea klabu hii mechi 10.

John Arne Riise – Winga wa kushoto

Historia inamtaja kama mchezaji tishio kwa kuwa na mguu wa chuma.

Unajua ni kwa nini? John Arne Riise anaongoza kwa kupiga mashuti makali. Sio hivyo tu, mashuti yake hayazuiliki na alithibitisha hili baada ya shuti lake kuuvunja mguu wa nchezaji wa zamani wa Man United, Alan Smith, aliyejaribu kuzuia shuti lake (2006).

Mnorway huyu hata hivyo, hakuwa na fomu nzuri katika fainali ile. Kiwango chake kilikuwa ni cha kawaida sana na hata ndiye aliyekosa mkwaju wa penalti usiku ule. Lakini bado ataendelea kutajwa miongoni mwa mashujaa pale Anfield.

Baada ya kuichezea Fulham kwa muda mrefu, beki huyu ambaye pia mara nyingine hutumika kama kiungo hasa katika eneo la pembeni, amehitimisha sehemu kubwa iliyobaki katika safari ya maisha yake katika soka akichezea klabu za kwao, Cyrpus na India.

Steven Gerrard – Kiungo mshambuliaji

Aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa fainali ile. Huyu ndiye aliyeibeba Liverpool mgongoni usiku ule. Alihakikisha Jiji la Istanbul linalipuka kwa shangwe, likiimba wimbo mmoja tu, ‘You Will Never Walk Alone’.

Alifunga bao la kwanza mara baada ya kurejea kutoka mapumziko na kufanya matokeo yasomeke 3-1.

Baada ya kuingia dimbani mara 710, akifunga mabao 186, Steven Gerrard aliamua kuachana na klabu hii aliyoitumikia tangu akiwa na miaka 16 na kuelekea Marekani akaichezea Swansong inayoshiriki MLS kwa muda mfupi.

Novemba mwaka jana, alitangaza kutundika daluga na mapema mwezi Januari mwaka huu, alipewa kazi ya kuwa kocha wa kikosi cha vijana cha Liverpool.

Harry Kewell/Vladimir Smicer– Kiungo mshambuliaji

Uwezo na kipaji cha Harry Kewel hakihitaji mjadala. Kila mtu anafahamu anachoweza kukifanya akiwa uwanjani. Dakika 23 alizocheza kwenye fainali ile usiku ule kabla ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Vladimir Smicer, zilitosha kabisa kumpa heshima.

Baada ya kuingia dimbani Smicer akafunga bao la pili kabla ya kufunga mkwaju wa penalti lililoipa Liverpool ubingwa. Kewell kwa sasa ni kocha wa Crawley ikiwa ni siku chache baada ya kutimuliwa katika klabu ya Watford ambako alikuwa kama kocha msaidizi.

Milan Baros – Straika

Milan Baros alikuwa na sifa ya ubutu. Straika huyu alithibitisha hili baada ya kushindwa kufunga bao kwenye mechi ya fainali jijini Istanbul kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mtukutu Djibril Cisse.

Msimu uliopita, Baros (35), alikuwa na kikosi cha Slovan Liberec. Akiwa na klabu yake hii, alifunga bao moja tu katika mechi mbili za michuano ya Uropa.