LeBron, Curry goma lao limeisha kitemi

Muktasari:

  • Timu mbili zinazoongozwa na manahodha na nyota wa mchezo huo duniani, Stephen Curry na LeBron James zilichuana katika mchezo huo mkali wa NBA All-Star unaochezwa kila msimu.

JUMAPILI iliyopita Dunia ilishuhudia mtanange mkali wa Mpira wa Kikapu uliopigwa nchini Marekani.

Timu mbili zinazoongozwa na manahodha na nyota wa mchezo huo duniani, Stephen Curry na LeBron James zilichuana katika mchezo huo mkali wa NBA All-Star unaochezwa kila msimu.

Kila aliyeutazama na kuufuatilia mchezo huo, aliridhika kwa jinsi ulivyokuwa wa ushindani wa hali ya juu na purukushani zenye ubora baina ya nyota wa timu yaliyosababisha matokeo ya aina yake kwa timu ya LeBron James iliyoibuka na ushindi wa ‘usiku’ vikapu 148-145.

Katika mfululizo wa kuangazia mchezo wa All-Star, Mwanaspoti linakuletea sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala kuhusu kilichotokea kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa kushinda misimu iliyopita.

MATARAJIO KUFIKIWA

Kwa kutambua mechi ya aina hii ilishaanza kupoteza mvuto, Shirikisho la Kikapu Marekani kupitia Rais Adam Silver walikuja na ubunifu huu wa manahodha kuchagua wachezaji miongoni mwa wale waliopigiwa kura za kuanza na wa kuingia kutokea benchi lengo kubwa lililopangwa ni kuleta upinzani ulioanza kukosekana tangu msimu wa 2014/2015.

Baada ya ubunifu huo kukamilika na kutangazwa utaratibu utakavyokuwa kila kitu kilienda kama ilivyopangwa na hatimaye timu mbili zilizotokana na manahodha LeBron na Curry zimefikia matarajio na kukata kiu ya upinzani wa mechi ya All-Star.

ILIKUWA NGUMU KUFUNGANA

Haina ubishi, mechi ya msimu huu iliyobadilishwa muundo imeleta kitu kipya na cha kufurahia zaidi kwa hadhi ya mchezo wenyewe unavyopaswa kuwa, tofauti na misimu iliyopita, timu za Mashariki na Magharibi zilipopambana zilikuwa na pointi nyingi kuanzia robo ya kwanza hadi robo ya mwisho.

Tofauti na misimu iliyopita, mechi ya msimu huu wakati kota ya kwanza inamalizika timu hizo ukiunganisha pointi za timu zote zilifungana vikapu 73 pekee ikiwa ni vikapu 28 pungufu ya vya msimu uliopita.

Mtiririko wa vikapu kwa kila timu kuanzia kota ya kwanza hadi ya mwisho ilikuwa 31, 45, 33 na 39 kwa timu ya LeBron James ukijumlisha ndio unapata jumla ya vikapu 148, huku timu ya Curry ilipata 42, 36, 34 na 33 na kuvuna jumla ya vikapu 145.

Achana na hiyo robo, ukifuatilia matokeo ya mwisho timu zote mbili ukijumlisha idadi ya pointi walizofungana 148-145 unapata vikapu 293 ambavyo ni tofauti na msimu uliopita, timu zilifungana jumla ya vikapu 374.

UFUNDI KWA MBINU

Kilichotokea baada ya mchezo wenyewe kila mtu anafahamu ila kwa jicho la ziada mchezo huu ulikuwa wa aina yake na uliojaa ufundi/ujuzi mkubwa kutoka kwa nyota wa pande zote mbili.

Ukija kwenye mbinu ni timu ya LeBron iliyofanikiwa zaidi kwani mbinu waliyoingia nayo iliwapa ushindi dakika 4 kabla ya mchezo kumalizika.

Wakati zilipobaki dakika 4 ubao ulisomeka vikapu 136-128 na timu ya Curry ndio ilikuwa inaongoza, lakini haikutosha kuamua mchezo kwa timu ya LeBron kurejesha ndani ya muda huo kufanya kusomeka 144-144 katika dakika ya mwisho mbinu ya timu LeBron kutowapa nafasi wapinzani wao wasitupe mitupo yao ikawapa ushindi wa 148-145.

Matokeo hayo yalitokana na mbinu kuanzia dakika za mwanzo hadi mwisho timu ya LeBron kuwazuia timu Curry wasifunge pointi tatu wakati huo, wao wakipenya ngome ya wapinzani wao na kufunga pointi mbili nyingi.

DURANT, LEBRON WALIKUWA MOTO

Wakati nyota wanaotabiriwa kutwaa tuzo ya MVP msimu huu Giannis Atentokounmpo na James Harden wakiwa na mchezo mbovu tofauti na ilivyotarajiwa, hali ilikuwa tofauti kwa nyota wawili Kevin Durant na LeBron James.

Wawili hao walionyesha umahiri wao wa kupanda na kushuka kwa ushirikiano wa hali ya juu tofauti na wasiwasi wa wengi wachezaji hao wasingeshirikiana kwa kila mmoja kutaka kuonekana bora badala yake walicheza pamoja kuhakikisha wanashinda mchezo huo wakisaidiwa na Russell Westbrook.

Kutokana na ushirikiano wa nyota hao kwenye mchezo huo, inaweza kuwa sababu nyingine ya uongozi wa timu ya Golden State Warriors kufanya kweli kumsajili LeBron katika timu yao ili kuthibitisha tetesi zilizozaa wiki chache zilizopita za kumtwaa nyota huyo.

CURRY KUSHINDWA UONGOZI

Akiwa kama nahodha kwenye timu yake, Stephen Curry alikuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha timu yake inacheza kwa ari na ushirikiano muda wote wa mchezo kutokana na hamasa yake kama kiongozi kama alivyofanya LeBron kwenye timu yake wakati wote wa mchezo.

Hata hivyo, Curry alishindwa kufanya hilo, ni kama alimwachia jukumu hilo mwenzake Klay Thompson aliyekuwa na mchezo mzuri zaidi katika mchezo huo akionyesha umahiri wake kwenye mitupo ya pointi tatu baada ya nahodha wake Curry kubanwa vilivyo kutopiga mitupo hiyo upande wa LeBron.

LEBRON NA TUZO YA MVP

Ili kutwaa tuzo hii yenye thamani kubwa kwenye mpira wa kikapu hususan katika mechi ya All-Star, sifa kubwa ni kufunga idadi kubwa ya pointi zaidi ya wengine, kuwa bora zaidi kiuchezaji kwenye mchezo huu pamoja na namna ambavyo mchezaji husika alivyosaidia timu kupata ushindi.

Katika mchezo huo, James alifanikiwa kufunga pointi 29, Rebound 10 na Assist 8 akimpita mbali DeMar DeRozan aliyeongoza upande wa timu ya Curry kwa kufunga pointi 21.

Sifa hizo zilitosha kumpatia LeBron tuzo ya tatu ya All-Star kwenye jumla ya mechi 14 alizokwishacheza na mara ya mwisho kwake kutwaa tuzo hii ilikuwa mwaka 2008, baada ya awali kushinda mwaka 2006 na endapo mchezo utakaofuata msimu ujao wa All-Star atakuwepo, atakuwa na kazi ya kusaka tuzo ya nne ili awafikie Kobe Bryant na Bob Pettit.

HITIMISHO

LeBron alitupilia mbali kurudiwa kwa mchezo huu ambao kama utarudiwa matokeo yanaweza kuwa tofauti kutokana na ubora wa timu zote mbili na hii inamaanisha Kamishna Mkuu Adam Silver na wote walioshiriki kubadilishwa kwa mfumo wa mechi hii wamefanikiwa kuufanya mchezo kuwa na thamani inayotakiwa tofauti na misimu mitano iliyopita. Mchezo ulikuwa na msisimko mkali wa aina yake.