Kwako Mwalimu Kashasha-Kuna nini kabatini?

Muktasari:

  • Katika kukidhi matakwa ya utashi wetu, tuna hulka ya kupanga mipango ya maendeleo ili kuyatawala mazingira yetu tukiongozwa na malengo tuliyojiwekea na kisha kupima kama yametimia baada ya kipindi maalumu ili kubaini kiwango cha mafanikio kilichofikiwa. Wahenga walisema wakati ni ukuta ukipigana nao utaumia.

KUUMBWA kwa dunia na sayari nyingine zote, binadamu amebahatika kupewa upendeleo wa aina ya pekee katika viumbe vyote vyenye uhai kuweza kuishi kwa kujali na kuzingatia wakati. Hii ni kwa sababu maisha yake yanatawaliwa na kufanya mambo kwa nguvu za utashi alionao.

Katika kukidhi matakwa ya utashi wetu, tuna hulka ya kupanga mipango ya maendeleo ili kuyatawala mazingira yetu tukiongozwa na malengo tuliyojiwekea na kisha kupima kama yametimia baada ya kipindi maalumu ili kubaini kiwango cha mafanikio kilichofikiwa. Wahenga walisema wakati ni ukuta ukipigana nao utaumia.

Tulianza safari ya siku 360 za mwaka 2017 Januari Mosi siku ya Jumapili. Nina hakika kila mtu mmoja mmoja, familia, taasisi mbalimbali na taifa kwa ujumla wake tulimwomba Mungu atupe uhai na nguvu za kutosha ili tufanye kazi na shughuli mbalimbali kwa ajili ya kujiletea maendeleo na ustawi wetu katika mapana yake.

Miongoni mwa tasnia na shughuli zilizohusika katika harakati za maendeleo kwa mwaka 2017 ni michezo, sanaa na utamaduni kuanzia ngazi za vijiji, kata na tarafa, hadi taifa, lakini hatukuishia katika ngazi ya taifa pekee bali baadhi ya vikundi, timu na mtu mmoja mmoja walipata bahati ya kupeperusha bendera ya taifa katika kuipigania nchi kwenye mashindano ya kimataifa katika nyanja ya sanaa na michezo kama vile soka, wavu, kikapu, pete, soka la ufukweni, riadha, ngumi, muziki na wanamitindo. Kwa ujumla tulijitahidi kutupa karata yetu katika maeneo mbalimbali.

Zikiwa zimesalia siku chache takribani tisa kumaliza mwaka, wadau, wapenzi na mashabiki wa sanaa, michezo na utamaduni kwa sababu za kikanuni katika maisha wanaona kama kama vile siku zimekimbia kwani wanalazimika kuangalia kila mmoja katika fani anayoipenda tumepata mafanikio kiasi gani kwa mwaka huu,ni wazi wapo wachache wanaoelewa malengo yaliyokuwa yamewekwa,lakini kundi kubwa katika jamii hawajui ni malengo yapi yaliyowekwa na chama cha mchezo husika, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) au wizara yenye dhamana katika michezo, lakini kwa walio wengi kinachoangaliwa ni mara ngapi alisikia au kuona kupitia kwenye vyombo vya habari kwamba wawakilishi wetu katika mashindano ya kimataifa wamefanya vizuri,mfano kutwaa kombe, kupata zawadi na vitu vinavyokamilisha furaha ya wapenzi wa michezo na sanaa.

Bahati nzuri hadi sasa sera yetu ya michezo imetoa wigo mpana wa kushiriki katika michezo mingi mbalimbali kuanzia ndani hadi nje kimataifa, kwa mantiki hii kila fani ilikuwa na nafasi sawa katika kuonesha uwezo na umahiri wake ili kuwapa burudani, kuwafurahisha na kuwaunganisha watanzania,vile vile kuibua vipaji vipya pamoja na kutoa ajira.

Hadi kufikia hapa tulipo baadhi ya fani chache zimejitutumua kidogo kimataifa na kuliletea sifa taifa mathalani timu ya vijana ya miaka 17, muziki wa Bongo fleva (Diamond na Alikiba ), Riadha (Simbu) na ngumi (Class) na wengineo wachache .

Tukiwa tunajiuliza na kuhesabu mafanikio ya jumla kwa mwaka nzima, wapenzi wa soka hawana pa kushika wala hawaoni kitu chochote cha maana kitakachowakumbusha matukio makubwa ya mashindano ya soka, si kwa ngazi ya vilabu au timu ya taifa katika michezo ya kimataifa.

Sifa ziwaendee Zanzibar heroes ambao wamejitolea kwa nguvu zao zote na kufanikiwa walo kupata nafasi ya pili katika mashindano ya chalenji huko Kenya na kulifanya jina la Tanzania kupaa wakati mwaka ukizidi kuyoyoma.

Bahati nzuri Tanzania ni mwanachama wa Fifa/CAF tangu tupate Uhuru mwaka 1961, hivyo tuna sifa ya kushiriki mashindano yoyote yanayoandaliwa na mashiriikisho haya makubwa katika Afrika na dunia, kwa mantiki hii mwaka huu timu zetu zilishiriki mashindano yote yaliyoandaliwa na CAF na Fifa lakini kwa bahati mbaya hakuna sehemu yoyote tuliyo fanikiwa kufanya vizuri.

Timu zetu zote kwa upande wa wanaume ziljaribu bahati, ya wakubwa (Taifa Stars) imecheza michezo kwa ajili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Urusi lakini ilitolewa mapema katika hatua ya makundi ikawa safari imekomea hapo.

Baada ya mkakati huo kushindwa, TFF kwa kushirikiana na wadau wengine wakahamishia nguvu zao kwenye kufuzu fainali za CHAN (wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani Afrika) mwakani ambako pia fainali zaijazo huko Morocco zimetushinda.

Licha ya juhudi hizo kushindwa bado timu za vijana U20, U17 nazo zilipambana kupata nafasi ya kuitangaza nchi lakini mambo bado yakawa magumu tulipata faraja kidogo, timu yetu ya vijana Serengeti boys U-17 ilikaribia kucheza fainali za dunia huko India, lakini bila kutarajia ikafungwa kwenye fainali za Afrika huko Gabon mwezi wa April na kuikosa nafasi ya kuweka rekodi ya kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza ambayo ingekuwa ni historia katika soka la Tanzania.

Kama hiyo haitoshi, timu zetu za wanamke Twiga Stars na Tanzanite hadithi ilikuwa ni hiyo hiyo ya kutupwa nje ya mashindano, na kibaya zaidi timu ya Tanzanite U-17 ilitolewa kwa aibu baada ya kuchapwa na vijana wenzao wa Nigeria kwa jumla ya mabao 10 katika michezo miwili nyumbani na ugenini.

Kwa ngazi ya vilabu mambo nako hayakuwa mazuri baada ya wawakilishi wetu katika mashindano ya kimataifa kufanya vibaya na kutolewa katika hatua za awali kabisa Yanga wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika (Champions League) na Azam wakipeperusha bendera yao na ya nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Confederation Cup).

Mazingira na picha halisi ya ushiriki wa timu zetu zote katika michezo ya kimataifa mwaka huu hayakuwapa furaha na raha wapenda soka katika nchi yetu licha ya imani na matumaini makubwa waliyokuwanayo hapo mwanzoni mwa mwaka huu.

Kutokana na matokea mabaya ya timu zetu katika michezo mbalimbali tuliyocheza matokeo yake yamedhihirishwa na utaratibu wa FIFA wa kutoa alama na kuzipanga nchi zote wanachama 205 kwa kuonesha zipo katika nafasi gani katika viwango vya ubora wa soka duniani, haikutushangaza sana kuona tunafunga mwaka tukiwa kwenye nafasi ya 146 duniani, inaumiza na kusikitisha sana lakini tufanyeje imekwishatokea.

Kama nchi na taifa lenye uhuru kwa muda mrefu tukiwa tumesherehekea miaka 56 ya Uhuru wetu Decemba 9, tuna kila sababu ya kukaa chini na kuingalia kwa kina hali hii.

Ninafahamu hakuna mtu wa mpira au mwanamichezo yeyote anayeweza kusimama na akazungumza kwa kujiamini kwamba tuna maendeleo ya kuridhisha katika michezo husani soka la kimataifa.

Ni wazi kwamba tunayo mipango mingi ya kuleta mapinduzi makubwa katika namna na njia mpya za kuendesha na kusimamia mpira, lakini sishawishiki sana kupata matumaini makubwa ya mafanikio ya kutosha kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa na utamaduni wa kupanga sana na kutenda kidogo, na mara nyingi tukishindwa hakuna anayoonekana kuwa tayari kueleza sababu za kushindwa kwetu, lugha pekee inayoonekana kutawala kutoka kwenye mamlaka ni, bahati mbaya lakini vijana wamepambana tutarekebisha dosari wakati ujao.

TFF mpya tunafunga mwaka bila chochote, tunakwenda kusherehekea Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, tutarajie nini? Kwa kujipanga na kuweka vipaumbele vyetu katika michezo huenda 2018 makabati ya TFF yakapata kitu cha kuhifadhi.