Kujitoa Kagame, Yanga haina hoja-1

Tuesday June 12 2018

 

MABINGWA wa kihistoria wa Tanzania, Yanga SC, wamegonga tena vichwa vya habari ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kuandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiomba kujitoa katika michuano ya Kagame Cup.

Sababu ambazo mabingwa hao wamezitoa hazina mashiko hata kidogo, kwa kifupi ni za kitoto mno.

Wamedai, eti wanajitoa kwa sababu ya ugumu wa ratiba inayowakibili ambapo kwa jicho la kawaida unaona kabisa hicho ni kisingizio cha kipuuzi kinachodhihirisha ni namna gani klabu hii inaongozwa na watu wasio makini na pengine unaweza kudhani labda wanafikiria kwa kutumia nyayo badala ya ubongo.

Kama hoja ni ushiriki wa michuano ya Afrika, Yanga iko kundi moja na Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya katika Kombe la Shirikisho Afrika, lakini wapinzani wao hao wamethibitisha kushiriki Kagame mwishoni mwa mwezi huu.

Mchezo unaofuata kwa Yanga kwenye Kombe la Shirikisho utakuwa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, iliyoshiriki michuano ya Sportpesa, michuano ambayo Yanga iliondolewa mapema na kupata muda wa kupumzika wa kutosha kujipanga upya.

Kwa hoja hizo, utabaini Yanga haikuwa na sababu za kiutu uzima za kujitoa, zaidi ya kuleta malumbano yasiyo na maana na kutaka kuhamishia soka letu midomoni badala ya miguuni.

WAMEIOGOPA SIMBA

Tangu Desemba mwaka jana pale Cecafa ilipotoa taarifa rasmi michuano ya Kombe la Kagame itarudi tena mwaka 2018 baada ya kusimama tangu ilipofanyika 2015, Yanga ilijua itashiriki. Tangu Aprili mwaka huu Yanga ilipofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ilijua fika mashindano yote yanawahusu, wakathibitisha kushiriki.

Lakini ratiba ya Kombe la Kagame ilipotoka tu na kupangwa kundi moja na Simba, hapo ndipo macho yakawatoka na harufu ya damu ikawanukia...ndio wakaja hivi vioja badala ya hoja.

YALE YALE

Mwakaa 2008 Yanga ilikataa kucheza na Simba kwenye mashindano haya haya, kutafuta mshindi wa tatu.

Hadi leo, Yanga hawajawahi kutoa sababu zozote za maana za kutotokea uwanjani siku ile zaidi na kudai kuwa, ilisalitiwa na wapinzani wao, waliokuwa wamekubaliana mambo fulani ya masilahi, kitu ambacho watani zao waliwaruka hawakuafikiana hilo.

MALUMBANO SC

Yanga ni klabu iliyowekeza zaidi kwenye malumbano dhidi ya mamlaka za soka kuliko ilivyowekeza kwenye soka lenyewe, we fuatilia mtiririko wa matukio yao hapo ndipo utabaini Mzee wa Upupu ninamaanisha nini.

1. YANGA vs FAT

Mwaka 1965, Chama cha Soka Tanzania, FAT, kilianzisha Ligi ya Taifa, kabla ya hapo kulikuwa na Ligi ya Dar es Salaam pekee. Yanga ilikuwa ikisusia ligi hiyo kwa miaka mitatu ya kwanza, 1965 hadi 1967, kwa sababu hizi hizi za kitoto.

1965

Yanga na Simba (wakati huo ikiitwa Sunderland) zilipangwa kukutana Juni 7, 1965 lakini dakika chache kabla ya mchezo, Yanga wakamgomea mchezaji mmoja wa Simba, Emmanuel Mbele ‘Dubwi’ wakisema alikuwa amefungiwa.

Hata hivyo, nao Sunderland walikuwa wakiwapinga wachezaji wawili wa watani zao hao.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa ligi, Abdul Hussein aliingia kati na kupatika kwa utatuzi wa wachezaji wote na timu hizo kukubali kiroho safi kucheza mchezo huo.

Hata hivyo, wakati mpira unataka kuanza, Yanga wakagoma tena safari hii wakija na hoja ya kumkataa mwamuzi wa pambano hilo na kumlazimisha aliyekuwa Rais wa FAT, Balozi Maggid akaamua kumteua aliyekuwa Kocha Mkuu wa kwanza Mzungu wa timu ya taifa, Milan Celebic, achezeshe...ndipo Yanga wakakubali kucheza, ambapo timu hiyo ilipata bao la kungoza kupitia kwa Mawazo Shomvi.

Kwa kuwa mchezo ulichelewa kuanza, hivyo ulichelewa kuisha kiasi cha giza kutanda ilhali mchezo ukiendelea.

Refa Celebic, aliamua kuvunja pambano hilo kabla ya dakika 10 na Sunderland kukata rufaa ili mechi hiyo irudiwe na FAT kweli iliridhia hoja za wakata rufaa na kuamuru pambano lirudiwe tena na Yanga wakagoma na kujitoa kwenye ligi.

Itaendelea Jumanne ijayo.....