Kroos alivuruga matumaini yote ya Arsenal

Muktasari:

  • Alikuwa akiwapigia kelele akiwataka wafuate maelekezo ya kocha, Neuer aliwaokoa na kuwatuliza lakini wakati huohuo kwa Pep ilikuwa ni dakika zilizojaa hasira, kocha alikuwa haelewi kulikoni wachezaji wake walikuwa wakitumia mipira mirefu na badala ya kulinda maeneo yao na kumiliki mpira kama alivyotaka.

TOLEO lililopita kwenye Kitabu cha Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau alianza kwa kuichambua mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal na Bayern ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza hasa jinsi Bayern ilivyobanwa. Endelea…

Alikuwa akiwapigia kelele akiwataka wafuate maelekezo ya kocha, Neuer aliwaokoa na kuwatuliza lakini wakati huohuo kwa Pep ilikuwa ni dakika zilizojaa hasira, kocha alikuwa haelewi kulikoni wachezaji wake walikuwa wakitumia mipira mirefu na badala ya kulinda maeneo yao na kumiliki mpira kama alivyotaka.

Pia, hata uamuzi wake wa kumpanga Javi nyuma ya viungo wa kati na mbele ya mabeki nao haukufanya kazi. Kocha alishindwa kuelewa vipi ana timu ambayo imeshindwa kabisa kufuata maelekezo?

Ni kwa sababu hilo ni soka. Pep alisema siku iliyofuata akiwa katika hali ya utulivu zaidi : “Ni kwa sababu sisi ni binadamu na si roboti, ni kwa sababu tunataka kufanya yetu kwa usahihi lakini kuna wakati hatujui tufanyaje, ni kwamba tumevurunda, kwa sababu mazoezi yalipooza na mechi ilikuwa kali.

“Ni kwa sababu wapinzani wetu nao wana vipaji licha ya kuna watu ambao mara kwa mara wanapenda kukosoa timu nyingine, ni kwa sababu hilo ni soka rafiki yangu.”

Wakati ambao timu yake inashindwa kujiongoza kwa kocha linakuwa jambo linaloendelea kumgusa, ni kama vile halina mwisho, katika mkutano wa baada ya mechi na waandishi wa habari alizungumza kwa dakika 20 zilizokuwa balaa, ingawa kesho yake alipoangalia video aliona kama ni mkutano uliotumia dakika saba na si 20.

“Ndio lakini ilionekana kama jambo lililomgusa na lisilo na mwisho, Manu (Neuer) ndiye aliyefanya kazi kubwa.”

Baada ya Neuer kuokoa penalti, Bayern ilitawala mchezo na kumiliki mpira, Thiago alianza kuja kivingine na timu ikaanza kutumia nafasi, pasi ndefu ya juu kutoka kwa Kroos hadi Robben ilimfanya Wojciech Szczesny kumchezea rafu Robben na hapohapo kipa huyo akalimwa kadi nyekundu na kutoka nje.

Mchezo uliendelea, shuti la Alaba liligonga mwamba na hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare ya bila ya kufungana licha ya krosi 17 ambazo Bayern ilizipiga katika lango la Arsenal.

Kila kitu kilibadilika katika kipindi cha pili, mabadiliko ya mchezaji mmoja yalitosha, alitoka Rafinha akaingia Boateng huku Martinez akasogea katikati na Lahm akawa nyuma yake na mbele ya mabeki wa kati, Thiago naye akawa wingi ya kushoto.

Mabadiliko yalikuwa na mantiki, Lahm alitawala mpira na kuitawala Arsenal, ni mtu mmoja ambaye alivuruga matumaini yote ya Arsenal.

Kroos alikuwa mahiri kipindi cha pili kuliko mchezaji mwingine yeyote, pasi 152 huku asilimia 97 zikiwa sahihi huku pasi aliyosogezewa Lahm ikatengeneza bao muhimu la kwanza kabla Muller hajaandika bao la pili kwa kichwa.

Kama kuna mtu ambaye alikuwa na hofu kuhusu uwezo wa mchezaji huyu kwa kiwango chake, katika mechi hii ameweza kujiweka katika hadhi ya staa wa dunia.

Kuna kitu ambacho Pep alijifunza katika mechi iliyopita, kucheza na timu yenye wachezaji 10 wakati akiwa Barca, amewahi kutumia washambuliaji wengi dhidi ya rundo la mabeki, wachezaji tisa wakiwa wanakaba eneo lao, alihakikisha harudii kosa katika mechi na Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates.

Alichoamua ni kuwajaza viungo mbele huku akitumia mbinu ya kuwajaza mabeki upande mmoja wa uwanja lakini ambao wanarudi kwa haraka upande mwingine.

Kroos alilipata somo hilo vizuri na kuwafanya Arsenal watumie muda mwingi upande mmoja wa uwanja.

Hali hiyo iliifanya Arsenal itumie asilimia 20 na zaidi ya umiliki wa mipira huku ikimudu kupeana pasi chache ukilinganisha na Bayern.

Uwezo wa Lahm kutabiri tukio linalofuata uwanjani, Kroos na soka lake maridhawa na uwezo wa Pizarro kutambua haraka nini kilichotakiwa, yote kwa pamoja yalichangia Bayern kupata ushindi wa mabao 2-0, ni kama ambavyo alisoma mazingira kutokana na uzoefu mchungu wa siku za nyuma dhidi ya timu ya wachezaji 10 iliyopanga kupaki basi. Bayern iliondoka London na ushindi mwingine wa Ligi ya Mabingwa, dalili njema lakini hakuna kilichomshawishi Pep kubweteka hasa baada ya kushitushwa na kilichotokea dakika za awali za kipindi cha kwanza.

Inaendelea

Jummane