Kocha wa Brazil aropoka First Eleven yake siku 120 kabla

Neymar Da Silva

Muktasari:

  • Tite alionekana kudokeza mastaa wake, Roberto Firmino anayekipiga Liverpool na Thiago Silva ambaye ni nahodha wa PSG

RIO DE JANEIRO, BRAZIL

IJUMAA  iliyopita, kwa bahati mbaya, Kocha wa Timu ya Taifa ya Brazil, Tite,  alijikuta akiropoka kikosi chake cha kwanza kitakachokuwa kinaanza mechi za Kombe la Dunia kule Russia zikiwa zimebaki siku 120 kabla.

Tite mwenye umri wa miaka 56, amefanikiwa kukitengeneza kikosi kikali cha Brazil baada ya nchi hiyo kuchemsha katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika katika ardhi yao miaka minne iliyopita na hapana shaka atakuwa anapata wakati mgumu kupanga kikosi chake.

Akizungumza Ijumaa, Tite alionekana kudokeza mastaa wake, Roberto Firmino anayekipiga Liverpool na Thiago Silva ambaye ni nahodha wa PSG,  hawapo katika kikosi ambacho kitakuwa kinaanza, lakini ni miongoni mwa wachezaji 15 ambao watakuwepo safarini Russia.

“Wachezaji 11 watakaoanza ni Alisson, Marcelo, Miranda, Marquinhos, Daniel Alves, Paulinho, Renato Augusto, Casemiro, Neymar, Coutinho na Gabriel Jesus,” alisema Tite wakati alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari cha nyumbani kwao, Brazil.

Brazil inatazamiwa kutumia mfumo wa 4-3-3 wakati itakapoanza kampeni hizo za Kombe la Dunia na mechi yake ya kwanza inatazamiwa kuwa dhidi ya Uswisi katika Kundi E ambalo inatazamiwa kulivuka kiurahisi kama mambo yakienda sawa.

Katika kikosi hicho, wachezaji wengine wawili ambao aliwataja ni kiungo wa Manchester City, Fernandinho na kiungo wa pembeni wa Chelsea, Willian, ambao wote wanatamba katika Ligi Kuu England kwa sasa.

Kutokana na kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ambazo zinataka kila timu isafiri na wachezaji 23 kuelekea katika michuano hiyo, kikosi cha Tite kwa sasa kinahitaji wachezaji wanane tu kwa ajili ya kujazia nafasi zilizobaki baada ya yeye mwenyewe kuwataja 15 wa awali.

Katika orodha hii bado kuna mastaa wengi hawajatajwa kama vile kipa namba moja wa Manchester City, Ederson, ambaye amekuwa akitamba katika Ligi ya England baada ya kuhamia hapo akitokea Benfica katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Inaonekana kuwa chaguo la Tite ni kipa namba moja wa AS Roma, Alisson, ambaye amekuwa akiwaniwa na klabu za Liverpool na Real Madrid baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika michuano mbalimbali ya klabu hiyo ya Italia.

Mwingine ambaye bado jina lake halijajitokeza kwa Tite ni beki wa kushoto wa Manchester City, Danilo, ambaye nafasi yake katika kikosi cha Kocha Pep Guardiola imekuwa si ya kudumu na amekuwa akibadilishana mara kwa mara na Fabian Delph wakati huu mwenye namba yake, Benjamin Mendy, akiwa majeruhi.

Beki wa Chelsea, David Luiz, naye amekosekana katika kikosi cha wachezaji 15 wa Tite na kwa hali ilivyo sasa, haitashangaza kama Tite atamuacha safarini Russia kwa vile amekuwa hapati nafasi ya kudumu katika kikosi cha Kocha Antonio Conte.

Winga mpya wa Tottenham, Lucas Moura, ambaye amekuwa akiitwa mara nyingi katika kikosi cha Brazil, naye amekosekana katika orodha ya wachezaji 15 wa kwanza wa Tite na atalazimika kufanya kazi nzuri ya kuingia katika orodha ya wachezaji 23 kama Kocha Mauricio Pochettino atakuwa akimtumia vema.

Winga wa Juventus, Douglas Costa, naye amekosekana katika kikosi cha kwanza cha Tite na licha ya kuonyesha makali yake, lakini nafasi yake imekuwa haba kwa vile anacheza nafasi moja na staa wa nchi hiyo, Neymar.

Hata hivyo, Costa ana nafasi ya kuwepo katika wachezaji 23.

Beki wa Atletico Madrid, Filipe Luis, naye atakuwa na matumaini ya kukumbukwa na Tite katika orodha ya wachezaji watakaokwenda Russia Juni baada ya jina lake kukosekana katika orodha ya kwanza. Hii ni sawa na ilivyo kwa staa wa Bayern Munich, Rafinha, ambaye jina lake halijaonekana.

Baada ya kuvurugwa katika michuano iliyopita katika ardhi yao Brazil ambapo walichapwa mabao 7-1 na Ujerumani, Brazil inaonekana kupania kufuta aibu katika michuano hii na imekuwa timu ya kwanza kufuzu katika michuano hii.

Itakwenda katika michuano hii ikiwa na nia ya kusaka taji lake la sita katika historia baada ya kutwaa mara tano mpaka sasa katika miaka ya 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002. Nafasi yao kama wababe wa dunia ipo hatarini kwa sasa mbele ya Ujerumani ambayo imechukua michuano hiyo mara nne kama ilivyo kwa Italia. Hata hivyo, Italia haijafuzu michuano hii.

Kundi lake litakuwa na nchi za Costa Rica, Uswisi na Serbia. Habari zaidi kuhusu kikosi chao itajulikana wakati itakapocheza mechi za kirafiki dhidi ya Russia na Ujerumani Machi mwaka huu.