Kambi zinawabeba sana jamaa

Thursday September 7 2017

Jengo la Makao Makuu ya Yanga ambalo miaka ya

Jengo la Makao Makuu ya Yanga ambalo miaka ya nyuma ndio lilikuwa likitumika kama kambi ya timu hiyo, lakini kwa sasa uwanja wake umetelekezwa na haufai kwa matumizi. 

By 0LIPA ASSA

KWA sasa ni utamaduni kwa kila timu kuweka kambi kabla ya mchezo fulani wa Ligi Kuu. Timu hizo huanza kambi mapema kabla ya msimu kuanza na baadaye kuweka kambi kujiandaa na kila mchezo.

Kwa jicho la nje unaweza kuona ni jambo dogo, lakini zinawabeba wachezaji kimtindo. Kambi hizo zi msaada si tu kwa timu bali hata kwa maisha binafsi ya wachezaji ambao hutumia muda wa kuwa kambini  kupunguza gharama za maisha.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na wachezaji kadhaa wa timu tofauti ambapo, wengi wamefichua namna kambi hizo zinavyowasaidia kubana matumizi na kufanya mambo makubwa tofauti na wakiwa nyumbani.

George Kavila-Kagera Sugar

Ni kati ya wachezaji waliodumu muda mrefu Kagera Sugar.

“Kama huna familia, unaweza kutengeneza pesa kwa kukaa kambini maana hakuna muda wa kutoka huku klabu ikikugharimia kila kitu. Lakini, kwa mtu niliye na familia kazi ipo pale pale, utasikia mtoto anaumwa, mke uliyemuacha nyumbani naye ana mambo yake,” alisema.

Victor Hangaya-Mbeya City

Hangaya, ambaye msimu uliopita alikuwa Prisons, amekiri anapokuwa kambini gharama za maisha zinapungua na pesa yake inafanya vitu vya kimaendeleo.

“Ingawa kukaa nyumbani kuna raha yake, lakini gharama inakuwa juu ya matumizi ya pesa kama kuhusu chakula, bili za maji na umeme na mambo mengine.

“Lakini, kambi hupunguza matumizi mengi binafsi. Kwanza sina muda wa kutoka zaidi ya kufanya mazoezi na kurudi kambini na kila kitu kinakuwa juu yao (klabu).

“Maendeleo yangu mengi nimeyafanya kwa fedha ninayosevu kwa kuishi kambini, mfano ni mkulima, hivyo nawekeza pesa zangu huku na kwenye biashara ndogo ndogo, nikipata mapumziko nikuangalia faida ambayo mara nyingi huwa naitumia ninakuwa nyumbani,” aliongeza.

Iddy Moby-Mwadui FC

Beki anayekuja kwa kasi naye amesema kukaa kambini kuna faida ikiwemo kupunguza matumizi mabaya ya pesa.

“Na kama kuna kutumia pesa ni pale tunapocheza mechi za ugenini na siyo kwa gharama kihivyo, unakuwa ni muda mzuri kwa wachezaji kutengeneza uchumi na kufanya mambo ya kimaendeleo.

“Ngumu sana kutunza pesa ninapokuwa nyumbani, majukumu yanajitokeza kila kukicha, lakini kambini nina uwezo wa kufanyia mipango pesa yangu kwani, nakuwa sina muda wa kutoka, labda iwe dharula ya familia kuhitaji msaada wangu,” anasema.

Deus Kaseke-Singida United

Kutokana na uzoefu wa kuzitumikia za Mbeya City na Yanga na sasa akiwa mwajiriwa wa Singida United, Kaseka anasema upo utofauti mkubwa wa gharama kwa mchezaji kuwa kambini au kukaa nyumbani.

Kambini anasema gharama zinakuwa za viongozi wa klabu, kuanzia chakula, matibabu na usafiri huku akisisitiza hata mchezaji aliye na familia, zipo gharama zinazopungua zikiwamo za kwenda mazoezini.

“Lakini pia kuna ubaya wa kukaa kambini muda mrefu, kama vile mazoea yakizidi heshima inapungua tofauti na kukutana kwa nadra, ambapo kila mmoja anakuwa na hekima dhidi ya mwingine,” anasema

Lakini anasema wanapokuwa majumbani, gharama huwa kubwa kwa matumizi kama ya chakula, mavazi, bili za maji na umeme, hospitali, kusaidia ndugu pindi wanapokuwa wanahitaji msaada.

Haji Mwinyi-Yanga

“Unapokuwa kambini kwanza hakuna muda wa kuzurula kwamba, unaweza ukakuta na ndugu na jamii wa kuwapa sapoti ya hapa na pale, hilo linafanya gharama ya maisha kuwa ndogo kwa kuwa kila kitu kinakuwa chini ya utawala wa klabu,” anasema.

“Nyumbani ni nyumbani, kila binadamu ana malengo yake na maisha yake, kuna matumizi ya aina tofauti, wakati mwingine inakuwa ngumu kutunza pesa kikamilifu ili kufanya kitu cha kimaendeleo, ndiyo maana ni rahisi sana kufanya kitu ukiwa kambini,” anasema.

Joseph Kimwaga-Azam

Anaeleza namna kambi zinavyoweza kuwapa urahisi wa kupunguza gharama ya kutumia pesa tofauti na wanapokuwa majumbani mwao, ambapo wanawajibika kulipia bili za umeme na maji na matumizi mengine ya familia.

“Ukiwa kambini unakuwa kwenye utawala mwingine, ambapo mabosi wa klabu ndiyo wanajua mtakula nini, mtalala wapi, mtatibiwaje kama kuna mgon jwa na mambo mengine, wakati mwingine kuna ofa tunapata ikitokea tunafanya vizuri,” anasema.

“Lakini unaporejea nyumbani ni kutumia pesa kwenda mbele, hakuna ofa zaidi ya kutoa pesa vinginevyo uwe na miradi ya kukuingizia kitu cha kuongeza uchumi.”