Kadi ziliwakosesha pambano la fainali ligi ya mabingwa

Muktasari:

Alessandro Costacurta, alioneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Monaco ile iliyokuwa na wanaume wa shoka, Gilles Grimandi na Christopher Wreh. Hata hivyo, kukosekana kwake hakukuizuia AC Milan, kutinga fainali. Kibaya zaidi ni kwamba, adhabu hiyo, haikumnyima tu kucheza fainali, bali ilimnyima fursa ya kutimiza ndoto ya kucheza mechi tatu ‘hat-trick’ mfululizo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MILAN, ITALIA.PAMBANO la fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya zinanukia pale Kiev. Kuna wachezaji ambao wana kadi moja ya njano na wanatembelea mstari mwembamba kiasi kwamba wanaweza kukosa pambano hilo kama wakipewa kadi nyingine ya njano. Wapo wachezaji mahiri ambao wamewahi kulikosa pambano hilo kwa kadi mbili za njano.

Alessandro Costacurta, AC Milan v Barcelona (1994)

Alessandro Costacurta, alioneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Monaco ile iliyokuwa na wanaume wa shoka, Gilles Grimandi na Christopher Wreh. Hata hivyo, kukosekana kwake hakukuizuia AC Milan, kutinga fainali. Kibaya zaidi ni kwamba, adhabu hiyo, haikumnyima tu kucheza fainali, bali ilimnyima fursa ya kutimiza ndoto ya kucheza mechi tatu ‘hat-trick’ mfululizo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Franco Baresi, AC Milan v Barcelona (1994)

Baada ya kumshuhudia beki wake, Alessandro Costacurta akikosa mechi ya nusu fainali kutokana na kuoneshwa kadi, Milan tena ilijikuta ikimpoteza beki mwengine kwa jina la Franco Baresi, unamtambua mwanaume huyu? Baresi alikosa mechi ya fainali, kati ya AC Milan na Barcelona kutokana na kuwa na kadi nyingi za njano baada ya kulimwa kadi ya tano ya njano, kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Monaco. Kwa bahati nzuri, kwenye benchi alikuwepo Paolo Maldini. Ikitumia mfumo wake wa kujenga ukuta imara ya ulinzi, wenye mabeki wanne, kinara wa ulinzi akiwa Maldini, AC Milan iliweza kuwazuia Romario, Stoichkov na Bakero. Barcelona ikala bakora 4-0!

Roy Keane, Man United v Bayern Munich (1999)

Unajua ni jinsi gani Roy Keane alikuwa amejiandaa kwa ajili ya fainali? Ulipokuwa mdogo uliwahi kujiandaa kwa ajili ya safari, halafu mama yako akatoka huko anakotoka na kuahirisha safari? Hiki ndicho kilichomtokea Roy Keane. Keane, aliingia katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Juventus akiwaza fainali tu. Alicheza soka katika kiwango cha juu kiasi cha kufunga bao la kwanza la United huku akiisaidia United kuichapa Juventus. Dakika za mwisho wakati presha ya mechi ikipanda alipewa kadi ya njano ambayo ilikuwa ni ya pili kwa michuano hiyo. Akalikosa pambano la fainali dhidi ya Bayern Munich pale Nou Camp.

Paul Scholes, Man United v Bayern Munich (1999)

Kama ilivyokuwa kwa Roy Keane ndivyo ilivyokuwa kwa Paul Scholes. Katika pambano hili gumu la nusu fainali dhidi ya Juventus alipambana sana kuipeleka United nusu fainali lakini jasho lake pia lilimkuta akiambulia kadi ya njano ambayo ilikuwa ya pili katika michuano hiyo. Alilikosa pambano la fainali dhidi ya Bayern Munich pale Nou Camp.

Michael Reiziger, Ajax v Juventus (1996)

Reiziger ataendelea kujilaumu mwenyewe kwa kitendo cha kitoto alichokifanya mwaka 1996. Nani anakubali kupata kadi mara mbili, katika mechi ya kwanza na mechi ya marudiano dhidi ya vibonde Panathinaikos? Matokeo yake alilikosa pambano la fainali dhidi ya Juventus na hivyo kushindwa kuwasaidia wenzake katika mchakato wa kutetea taji hilo mara ya pili mfululizo.

Kama angecheza, basi hiyo ingekuwa mechi yake ya mwisho katika jezi ya Ajax kwa sababu baada ya hapo alitimkia AC Milan.

Pavel Nedved, Juventus v AC Milan (2003)

Mmoja kati ya mastaa bora wa muda wote Juventus. Alikuwa kinara katika pambano la nusu fainali kati ya Juventus dhidi ya Real Madrid.

Hata hivyo, uimara wake ulisababisha apewe kadi ya njano kutokana na kumchezea rafu kiungo wa Madrid, Muingereza Steve McManaman. Alilikosa pambano la fainali dhidi ya AC Milan pale Old Trafford ambapo liliamuliwa kwa matuta huku Milan ikishinda.

Eric Abidal, Barcelona v Man United (2009)

Mechi ya nusu fainali kati ya Chelsea na Barcelona pale Stamford Bridge ilikuwa na burudani nyingi na ubabe mwingi. Barcelona ilipata bao katika dakika za mwisho kupitia kwa Andres Iniesta.

Hata hivyo, pambano hilo lilikuja na gharama zake katika kikosi cha Kocha Pep Guardiola wakati Eric Abidal alipolimwa kadi nyekundu kwa kile kilichodaiwa kumchezea rafu Mfaransa mwenzake, Nicolas Anelka. Alilikosa pambano la fainali dhidi ya Manchester United pale Rome.

Dani Alves, Barcelona v Man United (2009)

Hakuwa Abidal pekee, hata beki wa kulia wa Barcelona, Dani Alves naye alijikuta akiwa mtazamaji katika pambano la fainali dhidi ya Manchester United baada ya kupewa kadi ya njano katika pambano dhidi ya Chelsea ikiwa ni kadi yake ya pili katika michuano hiyo. Matokeo yake Guardiola alilazimika kumchezesha beki wa kati, Carles Puyol kama beki wa kulia. Katika nafasi ya Puyol alichezeshwa staa wa Ivory Coast, Yaya Toure. Pamoja na haya bado, Barcelona iliichapa United mabao 2-0 kupitia kwa Samuel Eto’o na Lionel Messi.

Thiago Motta, Bayern Munich v Inter Milan (2010)

Wengi huenda waliliona tukio la Thiago Motta, kukosa mchezo wa fainali kati ya Bayern Munich na Inter Milan, kama tukio la kawaida na wala hawakuona uzito wa tukio lenyewe.

Lakini kwa wapenzi wa soka na hasa watu wa mpira wanaojua maana ya mpira, tukio lile lilikuwa ni tukio kubwa sana. Kumkosa mtu kama Motta ilikuwa ni kosa la jinai. Kwanini? Thiago Motta ndiye aliyeiongoza Inter Milan, kuwasasambua wazee wa tiki-taka pale Camp Nou. Thiago alitumia nguvu zote kuhakikisha anaifanya Barcelona ionekana kama ya kawaida sana. Lakini kwa bahati mbaya, mwanaume huyu, alijikuta akilimwa kadi nyekundu, baada ya kumuangusha Sergio Busquets. Mungu sio Athumani, Inter Milan ile ya Jose Mourinho, licha ya kutinga fainali bila Thiago Motta, ilifanikiwa kuivuruga the Bavarians 2-0, na kuchuka ubingwa.

David Alaba, Bayern Munich v Chelsea (2012)

Hili lilikuwa ni moja kati ya matukio ya kushangaza katika historia ya soka, ambao mwamuzi alijikuta akitoa kadi nyekundu kwa mchezaji kimakosa.

Huu ulikuwa ni uzembe wa mwamuzi wa mchezo. Ilikuwa ni katika mechi ya nusu fainali, Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kutokana utelezi uwanjani Alaba alijikuta akiteleza na kwa bahati mbaya mpira ukamgonga mkononi ndani ya boksi. Mwamuzi alimpa kadi nyekundu na Alaba alilikosa pambano la fainali dhidi ya Chelsea pale Allianz Arena huku timu yake ikichapwa kwa matuta.

Branislav Ivanovic, Bayern Munich v Chelsea (2012)

Mwaka 2012, Branislav Ivanovic, alikuwa hashikiki, hakamatiki. Aliiongoza Chelsea kuichambua Barcelona vilivyo pale Camp Nou. Hata hivyo, wakati vijana wa Roberto di Matteo wakishangilia kutinga fainali, habari mbaya zilikuwa zinawasubiri. Shujaa wao (Ivanovic) alipata kadi ya pili ya njano na kwa maana hiyo alikuwa analikosa pambano la fainali dhidi ya Bayern Munich.

John Terry, Bayern Munich v Chelsea (2012)

Katika usiku uleule wa kihistoria Allianz Arena, sio Ivanovic tu ambaye alikosekana katika pambano la fainali, hata nahodha, John Terry alikosekana pia baada ya kupewa kadi ya njano katika pambano la nusu fainali dhidi ya Barcelona kwa kumchezea rafu winga wa Barca, Alexis Sanchez.

Baada ya pambano kumalizika kwa ushindi wa Chelsea, Terry alienda katika vyumba vya kubadilishia nguo na kuvaa jezi zake kisha akaenda kupokea kombe.