KWAKO MWALIMU KASHASHA-Ingia toka ni lazima tujifunze

Muktasari:

  • Lakini ukitarajia matokeo chanya ingawa nafasi ya kupata matokeo hasi ikiwa inapewa kipaumbele cha pili.

WAHENGA pamoja na wasomi wa tangu enzi za pilato na wengineo , wanaamini kuwa shujaa yeyote katika jamiii anapatikana kutokana na ujasiri wa kuthubutu kutenda jambo gumu zito na linaloumiza mwili na kuchosha akili.

Lakini ukitarajia matokeo chanya ingawa nafasi ya kupata matokeo hasi ikiwa inapewa kipaumbele cha pili.

Tulikuwa tunaendelea kupata burudani ya michezo mbalimbali ya Ligi Kuu 2017|2018, klabu zote 16 zinaendelea kupambana na hali zao ngumu kila timu kivyake, lengo la msingi tangu mwanzoni mwa msimu lilikuwa ni kupigania ubingwa au ufalme wa kandanda hapa nchini.

Kila timu ilipiga hesabu zake, ili kujiandaa kwa kufanya kila kitu ambacho wenye timu walifikiri kingewasaidia kufikia malengo. Yapo mambo mengi ya msingi ambayo yanastahili kutazamwa ili timu ipate tafsiri ya kuweza/kuruhusiwa kushiriki Ligi Kuu au ligi za madaraja mengine, mathalani kufanya usajili, kuwa na uongozi, kiwanja au viwanja pamoja na kuwa na vifaa vinavyokubalika.

Soka ina changamoto nyingi hivyo kila timu kupitia viongozi wake, wanalazimika kuzifahamu na kuzibaini mapema ili kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.

Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, limebebea dhamana ya kuongoza, kusimamia na kuratibu maendeleo ya mchezo huu. Hivyo afya na ustawi wa soka unategemea ubunifu, miongozo, maelekezo na mipango inayotolewa na TFF.

Kwa upande mwingine, klabu kama wadau wakuu na wabia wa shirikisho wana wajibu wa kuhakikisha mpira unachezwa.

Uhai wa soka katika nchi yoyote duniani unategemea shughuli za kila siku zinazohusu mchezo huu katika klabu kuanzia ngazi zote na hatimaye kuwepo kwa mafanikio katika nchi kwa hapa nyumbani. Soka ni mchezo unaokumbana na mageuzi ya mara kwa mara kulingana na mahitaji ya wakati uliopo, lakini sambamba na mabadiliko hayo soka inachezwa kwa kipindi kirefu ingawa maendeleo tuliyoyapata siyo makubwa sana. Kwa hapa nchini, kipimo cha juu cha mafanikio katika klabu ni kucheza Ligi Kuu. Mtindo na njia zakupata timu za kucheza Ligi Kuu umekuwa na mwonekano tofauti tofauti lakini kwa miaka yote, harakati za kuyafikia mafanikio haya zimeanzia katika ngazi ya wilaya, mkoa na hatimaye kanda na mwisho kabisa Taifa. Ushiriki wa klabu kwa kupitia kwenye mchakato mrefu kiasi hiki, unatoa fursa kwa timu kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu wa kutosha kwa vingozi kuwa waledi na kuzielewa mbinu nyingi mbalimbali za kuongeza timu, lakini wachezaji hao wanajenga uzoefu mkubwa kutokana na kushiriki kwenye ligi za madaraja tofauti tofauti.

Mtindo wa sasa wa Ligi Kuu wa kucheza nyumbani na ugenini kwa kushirikisha timu 16 kwa msimu huu, kabla ya mabadiliko yanayotarajiwa msimu ujao utakaojumuisha timu ishirini, ikiwa na maana kuwa mwisho wa msimu huu timu mbili (2) zitateremka daraja na kuruhusu timu nyingine sita (6) kupanda daraja. Na kwa mujibu wa utaratibu mpya, tayari timu zitakazopanda kutoka daraja la kwanza zimekwisha kujulikana ambazo ni Biashara (Mara), Alliance (Mwanza), JK Tanzania (Pwani), African Lyon (Dar es Salaam), Coastal Union (Tanga) na KMC ya Dar es Salaam.

Kujulikana kwa timu zilizopanda ni dalili ya timu nyingine kushuka na kuelekea daraja la kwanza, hii pia ni muelekeo wa kuhitimisha miezi kumi ya ligi kuu tangu mwezi wa nane mwaka jana yapo mengi ya kujifunza kutokana na msimu huu ikiwa ni pamoja na ugumu wa ligi yenyewe, ushindani, ratiba.

Pamoja na yote, kimsingi wa yote haya yatawasaidia kuwa macho zaidi ili yasiwe ni sababu ya timu kuteremka daraja.

Kwa misimu kadhaa tumeshuhudia baadhi ya timu zinapambana kwa nguvu zote ili kupanda daraja na kucheza ligi kuu lakini zimekuwa zinanusa tu na kuondoka baada ya kushiriki msimu mmoja, hili ni tatizo na ni moja ya sababu ya kudumaa kwa maendeleo ya soka nchini.

Wadau mbalimbali wa soka, waandishi wa habari, wahariri, wachambuzi, watangazaji na wapenzi wa mpira kwa muda mrefu wameendelea kupaza sauti, kuwakumbusha na kuwashauri wamiliki wa timu kuwa na mipango yenye malengo ya mbali na inayotekelezeka pindi wanapopata maono ya kuendesha/ kuanzisha timu za soka. Kwa kuwa kushawishika kuanzisha timu ni hatua moja, kufanikiwa kuunda timu ni hatua nyingine lakini kuwa na malengo au sababu za kuwa na timu ikasimamiwa na kuiendeleza ni kitu kingine.

Wimbi la timu kupanda Ligi Kuu na kisha kuteremka baada ya kucheza kwa msimu mmoja hapa nyumbani limekuwa ni jambo la kawaida, haipendezi watu / wananchi/ shirika ama idara ya serikali kuanzisha timu ambayo inapata maendeleo kiasi cha kupanda Ligi Kuu na kucheza msimu mmoja, kwa sababu yapo malengo ya msingi ambayo yanatakiwa kufikiwa kabla ya kuanzisha timu.

Inawezekana mtu au kikundi cha watu wakaanzisha timu kwa nia ya kujiburudisha au kufanya iwe ni timu ya ushindani, kwa ujumla ni vizuri kuwa na tafsiri sahihi ya nia na makusudi ya kuwa na timu. Kwa namna yoyote ile, katika zama hizi michezo ni gharama sana, siyo jambo rahisi au jepesi kutengeneza timu kwa kuwa kuna mahitaji mengi na nguvu nyingi za kutumia akili, mali na pesa hivyo vyote ni mchakato huu wa uwekezaji na ili kujenga timu hususani ya ushindani lazima kufikiria kwa kina haya yote.

Katika msimu huu zipo dalili mbaya kwa timu ya Njombe Mji ambayo imepanda daraja na mwenzake Lipuli. Endapo juhudi za kuinusuru Njombe Mji isiteremke zitashindikana, maana yake ni kwamba wakuu wa timu hiyo watalazimika ama kuachana nayo kabisa au wajipange upya kwa ajili ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza mwakani 2018/2019, ni kazi ngumu sana, ingawa hawana jinsi kwa mujibu wa kanuni za shirikisho, vinginevyo waiache ipotee kabisa.

Inawezekana timu za namna hii zinakuwa na nia ya kucheza kwa muda mrefu kwenye ligi kubwa lakini dosari ndogo ndogo wakati wa kuzianzisha, uzembe na migogoro inayodhoofisha uwezo wa kiutendaji pamoja na kukosa vyanzo vya mapato ya uhakika ni miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo njiani.

Ni busara kwa kila mwenye nia ya kuwa na timu ayazingatie mapema maadili na maarifa ya kuendesha timu kabla ya kufanya uamuzi wa kuanzisha timu, vinginevyo mchango wa timu kama hizi zinazopanda na kushuka ni mdogo sana katika maendeleo ya soka hapa nchini.

Msimu ujao wa ligi kwa vyovyote vile utakuwa mgumu zaidi kufuatia idadi ya timu kuongezeka hadi 20, ina maana ratiba itakuwa ndefu zaidi, gharama zitaongezeka hivyo viongozi, watendaji, wachezaji na TFF wajiandae kikamilifu.