JICHO LA MWEWE: Msikilize mchambuzi wa soka Rooney

Muktasari:

Jaribu kufikiria aliingia kikosi cha kwanza cha Everton akiwa na umri wa miaka 16. 

WAINGEREZA wa Skysport walimuweka, Wayne Rooney kuwa Mchambuzi katika pambano la Watford dhidi ya Chelsea pale Vicarage Road. Ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa. Nilitega sikio langu kwa umakini mkubwa huku nikitabasamu.

Rooney, mtoto wa kihuni wa Croxteth, Liverpool. Mpira umemwokoa kuwa mhuni wa mtaani. Rafiki zake mpaka leo ni wakorofi kama mabondia. Ni mtoto wa getto hasa. Kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa kulipwa, Rooney hakwenda shule.

Jaribu kufikiria aliingia kikosi cha kwanza cha Everton akiwa na umri wa miaka 16. Unadhani alikwenda shule lini? Hakwenda. Nilitaka kupima kitu wakati Rooney alipoitwa kuchambua mechi ya Watford na Chelsea.

Alichambua vizuri sana. Alikuwa akielezea mbinu za mchezo kwa pande zote mbili. Alikuwa akielezea kwa umakini tatizo liko wapi. Alikuwa akichambua kama kocha na alikuwa anaeleza nini kifanyike kwa pande zote mbili.

Hapa ndipo nilipowakumbuka wachezaji wetu. Kwa nini Rooney aliitwa kwenda kuchambua? Mara nyingi wachezaji wanasikilizwa upeo wao wa soka pale wanapohojiwa katika vyombo vya habari baada ya kumalizika kwa mechi.

Kama Rooney aliitwa ni kwa sababu walimuona anajua kuuchambua mchezo ambao umetoka kumalizika. Ikifikia hatua hiyo wanaanza kuona una dalili za kuwa mchambuzi pindi soka lako linapomalizika. Kabla hata soka la Rooney halijamalizika tayari wameanza kumuita studio.

Kwa nini wachezaji wetu huwa hawawezi kuwa wachambuzi au makocha pindi wanapoachana na soka? Unaweza tu kubashiri kwa kusikiliza mahojiano yao na watangazaji wa televisheni pindi mechi zinapomalizika.

Karibu wote huwa wanarudia maneno yaleyale tena kwa sentensi moja tu. “Mpira huwa una matokeo matatu kwahiyo tumekubali tumefungwa tutarudi kambini kwenda kujipanga” basi. Hakuna jipya. Unawezaje kupata mchambuzi kutoka kwa mchezaji ambaye hajui kilichoendelea katika mechi iliyomuhusu?

Mchezaji kama Rooney akihojiwa atakwambia: “Kipindi cha pili wapinzani wetu walirudi kwa kasi kubwa, hatukuwa tumejiandaa katika mipira ya kona ambayo waliipiga na wakapata bao la kuongoza.

Alipoingia Zlatan Ibrahimovic aliweza kukaa na mpira kiasi cha kushusha presha yao na hivyo kutupa nafasi sisi wengine kufungua uwanja.”

Huyu ni Rooney ambaye anajua kwanini timu yake imepoteza mechi. Anajua kwa nini kipindi cha kwanza waling’ara lakini kipindi cha pili wakapoteana.

Mchezaji wa namna hii ni rahisi kwake kuwa kocha au mchambuzi kuliko wachezaji wetu.

Mchezaji wa namna hii ni rahisi kwake kuusoma mchezo akiwa ndani ya uwanja na kuwaambia wenzake nini cha kufanya kabla hata kocha hajatoa maelekezo.

Mchezaji wa namna hii anaweza kualikwa kwenda studio kama walivyofanya kwa Rooney.

Tatizo liko wapi? Kuna mambo mengi nyuma yake. Binafsi siamini sana katika elimu. Kama nilivyosema awali, Rooney hana elimu kubwa. Muda wake mwingi ameutumia katika kucheza soka kuliko kwenda shule. Tatizo kubwa ni mchezaji wa Kitanzania hakuzwi kama mwanadamu mwenye maadili. Anajikuza mwenyewe mtaani na baadaye anaibuka kuwa staa.

Hapohapo ukichangia kuwa amekosa shule, basi mambo yanakuwa magumu.

Kuna makocha ambao ni wachezaji wa zamani wanashindwa hata kuongea mambo ya maana katika vyombo vya habari kutokana na kukosa upeo tangu wakati anacheza soka. Kocha mmoja, ambaye ni staa wa zamani nchini ni mropokaji mzuri sana.

Majuzi alihojiwa na mwandishi wa mwananchi akaulizwa kama haoni kuwa timu yake ilikuwa imefungwa katika pambano fulani la ligi kwa sababu ya uchovu wa safari kwa wachezaji wake ambao walikuwa wamesafiri kwa kilomita nyingi na kufika siku mbili kabla ya mechi. Akadai haoni uhusiano uliopo baina ya kusafiri na kucheza soka.

Huyu ndiye kocha ambaye unategemea awe mchambuzi wa soka.  Tuna safari ndefu kwa wachezaji wetu kujitambua. Katika mia yupo mmoja tu anayejitambua. Mfano mzuri ni Mbwana Samatta. Sasa hivi anaongea vizuri na nadhani baadaye anaweza kutumika kama mchambuzi katika vituo vyetu vya televisheni.

Bahati nzuri pia ilikwenda kwa wachezaji wa zamani kama Ally Mayai, Aaron Nyanda na hata Boniface Pawassa ambao wakati mwingine unaweza kuelewa wanachoongea. Nadhani kwa sababu ya shule ingawa bado napigwa na bumbuwazi kwanini Rooney na wachezaji wengine wa Ulaya wanaongea vizuri na hawana shule.