JAMAA WAMEFUNIKA KINOMA

SAWA wapo baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wamelemazwa na tabia ya kupenda kwenda kutengenezea video zao nje ya nchi, lakini sio kwamba hapa Bongo hakuna wakali wa kuwatengenezea kazi zao.

Ni ile kasumba tu ya kufuata upepo na kutaka kujitengenezea wasifu wa kazi zao, ila ukweli Tanzania ina watayarishaji wakali wa video za muziki wanaokimbiza.

Kwa sasa waimbaji wa Bongofleva wameshagundua ujanja wa kufanya ngoma zao mpya wanazotoa kubamba mitaani. Ujanja ni kutoa video kali kunogesha wimbo husika ili upate wafuatiliaji wengi kuanzia kwenye radio hadi kwenye televisheni.

Mwanaspoti linakuletea waongozaji wakali 10 wa video za muziki nchini ambao wanakimbiza, hata kama bado kuna wasanii wengine wanakimbilia nje ya nchi.

1. HANSCANA

Si jina geni kwa mashabiki wa muziki, hiyo ni kutokana na uwezo wake katika utengenezaji wa video kali na pia kufanya kazi nyingi za wasanii.

Hanscana, ni kijana mdogo aliyejizolea umaarufu mkubwa kupitia ubora wa video zake.

Hanscana, ametengeneza video nyingi na kali zikiwemo ‘Utaniua’ ya Jux, ‘Cheche’ ya Ommy Dimpoz, ‘Too Much’ na ‘Muziki’ ya Darasa, ‘Natamba’ ya Aslay, ‘Orugambo’ ya Saida Karoli, ‘Subalkheri Mpenzi’ ya Aslay na Nandy, Dede ya Mimi Mars, ‘Wasikudanganye’ ya Nandy, ‘Sometimes’ ya Baraka da Prince, ‘Amezoea’ ya Lulu diva, kidebe, ‘Ukivaaje Unapendeza?’ na ‘My Life’ ya Dogo janja.

2. ADAM JUMA

Kuna usemi unaosema; ‘Ya kale Dhahabu’. Kauli hii inathibitika kupitia uwezo wa Adam Juma. Asikuambie mtu huyo jamaa ni mkali katika utengenezaji wa video zenye ubora kutoka zamani hadi sasa.

Adam amepata kufanya kazi nyingi na bora na ndiye Direkta aliyeleta chachu na hamasa ya ushindani katika tasnia hiyo.

Mkongwe huyo ametengeneza video nyingi Kama, Utamu ya Dully Sykes ft Ommy Dimpozi na Diamond Platnumz, Mawazo ya Diamond Platnumz, Dar Kugumu ya msanii Marioo na nyinginezo kibao na anaendelea kufunika.

3. PABLO

Pia si jina geni katika tasnia hii ya muziki, katika kipengele cha utengenezaji wa video.

Director Pablo, ametengeneza video nyingi na bora, ambazo zinafanya vizuri katika mtandao wa YouTube na mtaani.

Baadhi ya video zilizotengenezwa na Pablo ni, Mama-Yamoto Band, Nafsi-Salamu TMK, Usingoje-Madada Sita, Wivu Wangu- Y-Tony na nyingine nyingi.

Ubora wa kazi yake ndiyo umemfanya kuwa mmoja wa mhimili mkuu wa muziki wa Tanzania.

4. MSAFIRI

Huyu ni mwongozaji na mtengenezaji wa video kutoka Kwetu Studio, Msafiri Shaaban ‘Travela’ anasifika kwa utengenezaji wa video bora, zinazofanya vizuri mtaani na mitandaoni.

Msafiri amefanya kazi nyingi za wasanii wakubwa na wadogo, baadhi ya video alizotengeneza ni kama, Kivuruge ya Nandy, Pambe ya Christian Bella, C Chafu pozi na Tagi Ubavu ya Billnass, Bongo Bahati Mbaya na Utani Utani ya Young Dee, Siteketei ya Angel Bernard, Ngarenaro ya dogo Janja, Sikinai na Libebe ya Beka Fleva, Moyo Sukuma Damu na Nabembea ya Lameck Ditto, Nisaidie Kushea ya Jay Moe na nyingine nyingi.

5. JOOWZEY

Dairekta Joowzey, ni miongoni mwa vijana wadogo wanaofanya kazi kubwa ya kuhakikisha video za wasanii wa Tanzania, zinakuwa bora na zinafika mbali zaidi.

Joowzey, ametengeneza video nyingi na zenye ubora unaohitajika, hasa kipindi hiki ambacho teknolojia imekuwa sana.

Video ambazo Joowzey, ametengeneza ni kama, Sitamani ya Mimi Mars na Young Lunya, Ngoma ya Barnaba, Mpe Habari ya Stereo, Mimina ya Gigi Money, Listen ya Steve R&B, Anita- Alicious Theluji kutoka Kongo, Sidhani ya Meda akiwa na Timbulo, Coconut ya Dully Sykes na Washangaze ya Neema Mudosa akiwa na Goodluck Gozbert.

6. NICKLASS

Ni jina ambalo halijakaa sana katika vichwa vya watu, lakini Nicklass ni moja kati ya waongozaji bora wa video nchini.

Nicklass ni miongoni mwa waongozaji na watengenezaji wa video zenye ubora, na amefanya kazi nyingi za wasanii wakubwa na wadogo.

Baadhi ya video alizotengeneza Nicklass ni kama, Zimbabwe ya Roma, Mikono Juu ya Ney wa mitego, Mwaaah ya Moni na Country Boy ‘moco’, Hivi Ama Vile ya Roma na stamina wanaounda kundi la Rostam na Usimsahau Mchizi ya Roma na Moni Centrozone.

7.KHAFAN

Anafahamika zaidi kama Dairekta Khalfan, japo majina yake kamili ni Khalfan Khalmandro. Ni mmoja wa watengenezaji wa video nchini.

Kazi zake zenye ubora ndizo zilizofanya Khalfan, kuwa miongoni mwa watengenezaji wa video bora nchini ambao Mwanaspoti imekuletea.

Khalfan, ametengeneza video nyingi zikiwemo, Sophia ya Ben Pol, Main Chick ya Maua, Sema ya Madee akiwa na Nandy, Upofu ya Nuh Mziwanda, Bolingo ya Bob Junior na nyingine nyingi.

8. DEO ABEL

Udogo wake katika tasnia hii sio tija, kwani kazi zake ni kubwa na zenye ubora zaidi. Deo Abel, ni mwongozaji na mtayarishaji wa video za wasanii, ambaye amekuja kwa kasi kutokana na ubora wa kazi anazofanya. Baadhi ya video alizotengeneza ni, Bombardier ya Dully Sykes, Only You ya Amber Lulu, Niwe Dawa ya Nini akiwa Ney wa Mitego, Kasheshe ya Bigway, Tunasafisha ya Edu Boy, Amber Lulu na Belle 9 na pia ametengeneza video nyingi za wasanii tofauti.

9.NISHER

Mwongozaji Nisher, ni miongoni mwa waongozaji wakongwe ambao wameleta mapinduzi ya video bora nchini.

Nisher, ametengeneza video nyingi za wasanii wa Bongo na wa nje pia.

Mkali huyo anasifika kwa mtindo wake kutumia moto katika video zake, kwani asilimia kubwa ya video zake ametumia moto.

Ametayarisha video kama Arosto ya Weusi na Chin Bees, Unanichora ya Joh Makini akiwa na Ben Pol, Naiee ya Edu boy na Billnass na Nje ya Box ya Weusi.

10. IVAN

Ukiwataja watengenezaji wa video bora nchini, huwezi kumuacha Director Ivan.

Ni kijana mwenye uwezo mkubwa katika tasnia hiyo ya utayarishaji wa video,na ni mtayarishaji anayekuja kwa kasi na, mwenye chachu kubwa ya ushindani.

Ivan, ametengeneza video nyingi zikiwemo, Sale Sale ya Dayna Nyange na milele ya Sam wa Ukweli.