INAWEZEKANA: Bila shaka Coutinho atang’ara

Muktasari:

Ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa mbele na pia winga wa kushoto. Barcelona ilipomuuza Neymar ilitambulika wazi kuwa hakuna mchezaji duniani hivi sasa mwenye uwezo wa kuvaa viatu vyake.

MSOMAJI kutoka mwanzo wa dirisha la usajili mpaka dakika za mwisho ilikuwa wazi Barcelona ingemsajili kiungo na nyota wa Liverpool, Philippe Coutinho.

Ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa mbele na pia winga wa kushoto. Barcelona ilipomuuza Neymar ilitambulika wazi kuwa hakuna mchezaji duniani hivi sasa mwenye uwezo wa kuvaa viatu vyake.

Lakini, Coutinho ni mchezaji angalau angeirudishia Barcelona heshima na kuipa uwezo wa kuendelea kuwa kati ya klabu bora kabisa barani Ulaya.

Na Barcelona ilikuwa tayari kumsajili mchezaji huyu kwa zaidi ya Pauni 100. Lakini, Liverpool ni klabu yenye malengo makubwa. Ni klabu yenye historia ndefu na hivi sasa ipo njiani kurudi katika ubora wake.

Msimu huu Liverpool ina fursa ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa. Na kwa mtazamo wangu klabu hiyo itahitaji kuendelea kushiriki katika Ligi ya Mabingwa kama itataka kuendelea zaidi kimpira kwa kuwa wachezaji bora duniani wanataka kushiriki katika Ligi ya Mabingwa.

Klabu kama Manchester United imeshaonyesha nia ya kuingia katika nne bora na hata kushinda Ligi Kuu huku klabu kama, Tottenham, Chelsea, na Manchester City zote zina uwezo wa kumaliza ligi katika nafasi bora kuliko Liverpool.

Hakika tumeshawahi kuona wachezaji wanaotaka kuhama klabu zao wanagoma kucheza au wanakataa kujituma kama klabu zao hazijawaruhusu kuhama pale wanapotaka. Lakini, dirisha hili la usajili ambalo limefungwa wiki mbili zilizopita halikuwa la kawaida.

Mwakani, Kombe la Dunia litachezwa Urusi. Ni ndoto ya kila mchezaji wa soka kuwakilisha nchi yake katika mashindano haya makubwa na yenye mvuto wa kipekee. Hivyo, wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kuhama klabu zao wataendelea kujituma msimu huu ili wapate nafasi katika timu zao za taifa hata kama wana hasira na klabu zao.

Coutinho aliiomba klabu yake imwachie aende Barcelona na kutokana na Liverpool kukataa ombi hilo mchezaji huyu atakuwa ameumizwa na matendo ya klabu yake kumkatalia.

Lakini Coutinho hawezi kususa kwa sababu klabu yake haijamtendea haki, badala yake atafanya kila analoweza Liverpool ifanye vizuri na kuendelea kuwa katika hali nzuri kimpira kwa sababu kama sivyo, basi huenda atakosa nafasi yake katika Timu ya Taifa ya Brazil. Bila shaka Coutinho ataendelea kuwa kileleni katika Ligi Kuu ya England msimu huu.