Huu ndio ujanja wa Jonas Mkude

Muktasari:

Ndio, jamaa kulikuwa na kila dalili za kutemana na klabu yake hiyo iliyomuibua miaka mitano iliyopita, baada ya kumaliza mkataba wake.

HUENDA mpaka sasa, kila shabiki wa soka bado haamini kilichotokea kwa nahodha wa Simba, Jonas Mkude. Ndio, jamaa kulikuwa na kila dalili za kutemana na klabu yake hiyo iliyomuibua miaka mitano iliyopita, baada ya kumaliza mkataba wake.

Wapo walioamini kuwa huenda angetua Yanga na wengine walijua angesajili Singida United, lakini ghafla jamaa alibadilisha gia angani na kuamua kusalia Msimbazi.

Kitendo cha kusalia Msimbazi, kimemfanya kiungo huyo mkabaji kuwa, mmoja ya wachezaji waliotengeneza fedha ya kutosha katika dirisha la usajili lililofunguliwa karibuni.

Mkude anaonekana bonge la mjanja, lakini kama hujui ni kwamba ujanja wa Mkude unasababishwa na mtu mmoja ambaye hana makeke kabisa, lakini anajua kuifanya kazi. Vigogo wenye maamuzi ya mwisho Simba na Yanga wanamjua vilivyo.

Kama hujui ni kwamba maamuzi magumu ya nahodha huyo wa Simba, kukubali kuwa chini ya usimamizi ya mshauri wake, Richard Kiwale yamemlipa mchezaji huyo. Amini usiamini, hafahamiki sana lakini msimamizi huyo kamtajirisha Mkude kama utani vile.

Mkude alikubali kuwa chini ya usimamizi wa Kiwale tangu akiwa katika timu ya vijana ya Simba, lakini dili mbili alizopiga hivi karibuni chini ya usimamizi wa jamaa huyo zimempa utajiri.

Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kwamba Kiwale amekuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya mikataba jambo ambalo limemfanya Mkude kuwa tofauti na wachezaji wengine, akipiga mkwanja wa maana katika mikataba yake miwili ya mwisho.

Ifahamike kwamba, Mkude amesaini mkataba mpya wa kuendelea kucheza Simba kwa miaka miwili, chini ya usimamizi wa Kiwale ambaye siye maarufu sana miongoni mwa familia ya soka nchini kutokana na kazi yake kuwa ya chini kwa chini.

Miaka minne, Mil 330

Mkude licha ya kuwa chini ya usimamizi wa Kiwale, hakuweza kupata fedha ndefu hadi Desemba 2014 aliposaini mkataba mpya wa kuendelea kucheza Simba kwa miaka mingine miwili.

Kwanza katika mkataba huo, Mkude alipewa kiasi cha Sh 60 milioni mkononi na mshahara wake ulipanda hadi Sh 3 milioni kwa mwezi kutoka Sh 600,000 aliyokuwa akilipwa awali. Fedha hizo zilimfanya kuwa mchezaji mzawa anayelipwa zaidi ndani ya Simba.

Ukipiga hesabu ya mishahara yote ya Mkude katika kipindi cha miaka miwili ya mkataba huo, ni Sh 72 milioni jambo ambalo liliufanya mkataba huo kuwa na thamani juu. Kwa hesabu za haraka, ukichanganya fedha za usajili pamoja na mishahara yake kwa kipindi chote cha mkataba, Mkude alipata jumla ya Sh 132 milioni.

Mkataba huo wa miaka miwili ndio umefikia ukingoni mwaka huu ambapo kutokana na kiwango cha juu cha nahodha huyo, Simba imelazimika kuvunja benki na kutoa fedha ndefu zaidi.

Wakati Mkude anasaini mkataba mpya mwaka 2014, Yanga pia ilikuwa ikimhitaji, lakini Kiwale aliwatuliza na kuzungumza nao ambapo mwishowe ofa ya Simba ilikuwa nono zaidi na kiungo huyo aliamua kubakia Msimbazi.

Singida, Yanga

Kabla ya Mkude kusaini mkataba mpya wikiendi iliyopita, alimruhusu Kiwale kufanya mazungumzo na klabu tatu za Simba, Yanga na Singida United ili kuona ni ipi ambayo itampa ofa nzuri zaidi. Mkude anamheshimu Kiwale vilivyo.

Singida United ilifanya mazungumzo ya mapema na Kiwale ambapo walikubali kutoa kiasi cha Sh 60 milioni kama ada ya usajili na mshahara mnono. Hata hivyo, Kiwale alimshauri Mkude wasubiri kwanza kwani yawezekana wakapata ofa nono zaidi.

Msimamizi huyo ambaye ana uelewa wa sheria za mikataba baadaye alirejea katika mazungumzo na Simba ambao walionekana kuwa na ofa ndogo, hivyo kumlazimu pia kusikiliza ofa ya Yanga.

Kutokana na ushawishi wake, Mwanaspoti limebaini Simba ilikubali kuweka mezani kiasi cha Sh 80 milioni ambazo zimelipwa mara moja ili kumbakiza nahodha huyo huku mshahara wake wa mwezi ukipanda hadi Sh 5 milioni tofauti na Sh 3 milioni aliyokuwa akilipwa hapo awali.

Kwa hesabu za haraka ni kwamba, mbali na fedha hizo za usajili, Mkude atachota kiasi cha Sh 120 milioni kama malipo ya mishahara katika kipindi cha miaka miwili ya mkataba wake wa sasa hivyo kuifanya thamani ya jumla ya mkataba wake kuwa Sh 200 milioni.

Usimamizi wa Kiwale umemfanya Mkude kuwa mchezaji mzawa ghali zaidi ndani ya Simba akiwafunika hadi nyota watatu wa Azam, Shomari Kapombe, Aishi Manula na John Bocco ‘Adebayor’ ambao wamesajiliwa hivi karibuni.

Nyota hao watatu licha ya kuzidiana katika fedha za usajili, kila mmoja atakuwa akipokea kiasi cha Sh 3 milioni kama mshahara wake wa kila mwezi hivyo kuwa chini ya Mkude ambaye ndiye mchezaji aliyecheza Simba kwa muda mrefu zaidi.

Dili za mwanzo

Licha ya ukweli kwamba Mkude amesaini mikataba hiyo miwili yenye thamani ya Sh 332 milioni, malipo yake ya awali hayakuwa mazuri sana, lakini jamaa huyo alimtia moyo kwamba ipo siku watavuna fedha za kutosha.

Mkataba wa kwanza wa Mkude katika timu ya vijana, alipewa kiasi cha Sh 6 milioni tu na mshahara wa Sh 600,000 kwa mwezi hivyo kuwa mchezaji analiyelipwa kawaida tu ndani ya klabu hiyo.

Mkataba huo ulikuwa na thamani isiyofikia Sh 30 milioni lakini Mkude alikomaa na kucheza kwa kiwango cha juu hadi alipojihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza mwaka 2013 na mwaka 2014 ndipo alipoanza kupata pesa ndefu.

Matatizo ya mkataba

Tofauti na wachezaji wengine, Mkude hajawahi kupata matatizo ya mikataba kutokana na usimamizi wa Kiwale ambaye kwake sheria ya mikataba imelala kichwani. Mikataba yote ya Mkude kabla ya kusainiwa, huwa anaipitia na kutoa ushauri wake kuhakikisha vipengele vyote vyenye utata vinarekebishwa. Mkude hawezi kufanya makubaliano yoyote bila kumshirikisha Kiwale.

Hii imemfanya Mkude kuwa katika sehemu salama wakati ambapo wachezaji wengine wamekuwa wakipata matatizo na uongozi wa Simba. Mfano Kiwale alikuwa amewabana Singida kwamba kama Mkude angesaini, na wangeshindwa kumlipa kwa miezi miwili tu mkataba huyo ungekufa.