Haya ndio maisha ya Lwandamina

Sunday April 15 2018

 

By KHATIMU NAHEKADAR ES SALAAM

KULE Ulaya gumzo kubwa ni ratiba ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo majogoo wa Anfield, Liverpool watavaana na AS Roma huku wababe wawili wa Ulaya, Real Madrid wakimaliza ubishi na Bayern Munich.

Lakini, hiyo sio ishu sana kwani hapa nyumbani Ligi Kuu Bara nayo imefika patamu kwelikweli huku mahasimu Simba na Yanga wakifukuzia ufalme huo kwa kasi. Aah! hata hiyo ishu ya ubingwa nayo kama vipi ipotezee tu, Yanga mambo bado hayajakaa sawa tangu kocha wake George Lwandamina, kuamua kutimka zake kwao na kuiacha timu hiyo.

Mapema wiki hii Lwandamina, ambaye amekuwa na Yanga na kuweka rekodi zake tamu, aliondoka klabuni hapo na kurejea kwao Zambia ambako, anahusishwa na kutua timu yake ya zamani ya Zesco United.

Hata hivyo, Lwandamina maarufu kama Chicken amekiri kuwa huduma yake inawaniwa na klabu nyingi za Ligi Kuu ya Zambia, lakini bado hajafanya uamuzi wowote kwa kuwa ana mkataba na Yanga.

Mwanaspoti linakuletea kwa undani kuhusiana na safari kamili ya Lwandamina kabla na baada ya kutua hapa nchini kuingoza Yanga na kutimka kwake.

Ni nani huyu Lwandamina

Alizaliwa Agosti 5, 1963 katika mji wa Mufulira nchini Zambia na kipaji chake kiliibuliwa na mwalimu mmoja katika Shule ya Msingi Wusakile iliyopo mjini Kitwe alipokuwa akisoma.

Lwandamina akiwa mdogo alipata mzuka zaidi ya kucheza soka baada ya mama yake kumuunga mkono na kumnunulia viatu vya kuchezea huku baba yake akifariki dunia wakati akiwa na miaka 10 tu.

Akiwa darasa la tano alisimama kuendelea na shule kutokana na kukosa ada hivyo, kutumia muda mwingi kucheza soka ambapo, alikuwa straika mmoja matata sana. Baadaye alirejea shuleni katika Shule ya Justin Kabwe, ambako alifaulu kuendelea na masomo katika Skondari ya Ndeke .

Akiwa shuleni hapo alitilia mkazo masomo, lakini baadaye walimu walibaini kipaji chake na kumuomba kuichezea timu ya shule huku akipewa jahada za unahodha kikosini.

Kutokana na kuonyesha soka safi, Lwandamina aliitwa kwenye kikosi matata kilichoundwa na wachezaji kutoka shule za sekondari maarufu kama Copperbelt, ambako alipewa jukumu la kuwaongoza wenzake.

Ni kwenye kikosi hicho ndipo Lwandamina akabatizwa jina la Chicken. Baadaye alijiunga na klabu ya CISB, ambako alicheza sambamba na Kenneth Malitoli na Kapambwe Mulenga. Wakati wa likizo Lwandamina alikuwa akienda kumsalimu mama yake na huku alikuwa akiichezea timu ya Chiwempala Leopards.

Mwaka 1984 akiwa katika mwaka wake wa mwisho shuleni hapo, Lwandamina alikuwa na ofa kutoka klabu mbalimbali, lakini aliamua kujiunga na Mutondo Stars iliyokuwa ikinolewa na Fordson Kabole.

Alipomaliza shule alirejea mjini Mufulira na kuamua kujiunga na Mufulira Blackpool badala ya Wanderers, akiwa na ndoto za kufuata nyayo za Kalusha Bwalya.

Ni kwenye klabu hiyo ndipo Lwandamina alipobadili nafasi uwanjani kutoka mshambuliaji na kuwa beki, ambapo alikuwa kikwazo kwa washambuliaji. Mwaka 1992 alipata majeraha yaliyomfanya kucheza akiwa na maumivu na mwaka 1995 aliamua kustaafu soka. Mbali na Mufulira Blackpool, Lwandamina pia amezichezea Mufulira Wanderes na Mutondo Stars.

Rekodi zake/Yanga yamuona

Kama ilivyo kwa makocha wengine, Lwandamina naye amezinoa klabu kibao japo Zesco United ndio inafahamika zaidi kutokana na kushinda mataji kibao ikiwemo kuifikisha nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016. Zesco United ilitolewa na Mamelod Sundows ambayo ilikuja kubeba taji hilo. Klabu zingine ambazo Lwandamina amezinoa ni Mufulira Wanderers, Green Buffaloes, Kabwe Warriors, timu ya Taofa ya Zambia, Red Arrows na sasa Yanga.

Wakati Chicken akiipeleka Zesco nusu fainali Afrika, mabosi wa Yanga walianza kufuatilia njia zake kutokana na kuvutiwa na kikosi alichotengeneza ndani ya Zesco United, ambayo ilikuwa ikizichapa timu za Ukanda wa Afrika Kaskazini. Wakati huo Yanga ilikuwa ikishiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ikiwa chini ya Mholanzi Hans Pluijm.

Yanga ilianza kumpigia hesabu Lwandamina ilitokana na kuanza kuyumba kwa kikosi cha Pluijm, ambaye alifanikiwa kushinda mechi moja pekee akipoteza nne na kutoa sare moja katika hatua ya makundi wakimaliza timu ya mwisho katika kundi lao. Kinara wa kundi hilo alikuwa TP Mazembe ambayo ilikwenda kubeba taji hilo kwa kuichapa MO Bejaia ya Algeria.

Mabosi wa Yanga chini ya uongozi wa Yusuf Manji walipanga kutaka kufika mbali zaidi kimataifa kwenye msimu unaofuata hasa ikizingatiwa katika ligi ya ndani walikuwa na kila dalili ya kuwa bingwa hivyo, kuamua kumchukua Lwandamina ili aje kuipa mafanikio hayo.

Hata hivyo, safari ya Lwandamina kutua Yanga haikuwa nyepesi hata kidogo kutokana na Zesco kuwa bado wakihitaji huduma yake. Lakini, ofay a Manji mara nyingi huwa haimuachi mtu salama, ambapo Lwandamina aliamua kutua nchini.

Pia, inaaminika kuwa sababu kubwa ya Chicken kuachana na Zesco United ni kutokana na klabu hiyo kutothamini kazi yake.

Anatua Bongo kimafia

Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye Lwandamina alitua nchini na habari njema zaidi ni kuwa, ujio wake huo ulifichuliwa na Mwanaspoti lililokuwa gazeti pekee lilimuibua wakati akiwasili nchini Oktoba 23, 2016, alipokuja kwa mazungumzo ya mwisho na mabosi wa Yanga.

Kufichuliwa kwa ujio huo kulileta tafrani kubwa nchini Tanzania na Zambia, ambapo hapa Dar es Salaam kocha aliyekuwepo Yanga wakati huo Pluijm alianzisha vurugu akidai kutoheshimiwa huku kule Lusaka nako mabosi wa Zesco walicharuka wakiona wametorokwa.

Hata hivyo, Lwandamina aliondoka nchini bila kusaini mkataba na kurudi Zambia ambapo, alirejea baadaye na kusaini mkataba wa mwaka mmoja akitambulishwa rasmi Novemba 25 na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akichukua nafasi ya Pluijm, ambaye alipewa kibarua cha Mkurugenzi wa Ufundi ikiwa ni cheo kipya, lakini muda mfupi baadaye akatua zake Singida United.

Rekodi yake Yanga

Katika msimu wa kwanza ambao Lwandamina aliiongoza Yanga na kuipa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na miezi sita pekee, yakiwa ndiyo mafanikio yake makubwa akichangia msimu nusu kwa nusu na Pluijm.

Hata hivyo, msimu uliofuata Yanga ilianza kuyumba kiuchumi na kuifanya kazi ya kocha huyo kuwa ngumu hasa baada ya misukosuko aliyoipata Manji na kuamua kujiuzulu na timu kukumbwa na migomo ya wachezaji mara kwa mara na kusababisha kushuka kwa kiwango cha timu hiyo.

Ikishiriki mashindano ya Afrika, Yanga ilikosa afya ya mafanikio na kutolewa mara mbili katika mashindano mawili tofauti mara ya mwisho akitolewa na Zanaco ya kwao Zambia, ambayo ilitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Msimu huu ndiyo ulikuwa wa kwanza kwa Lwandamina, ambapo licha ya kuanza mwanzo lakini bado tatizo la ukata liliendelea kuikumba Yanga ikishindwa kufanya usajili wa maana.

Akomaa na Simba matajiri

Msimu huu Lwandamina licha ya Yanga kuonekana kuwa mbovu, lakini katika hali isiyotarajiwa ameikaba koo Simba iliyokuwa na maisha ya kitajiri wakitofautiana kwa pointi chache kwenye msimamo.

Presha ya Yanga iliwafanya matajiri wa Simba kufanya uamuzi mgumu wa kumtimua aliyekuwa kocha wao Mcameroon Joseph Omog na kazi kupewa Mfaransa, Pierre Lechantre.

Kama alivyokuja ndivyo alivyoondoka

Jumanne, Lwandamina aliamua kuondoka kurejea kwao katika safari ambayo hakuaga wala kujulikana ingawa siku moja baadaye alilifungukia Mwanaspoti kila kitu. Lwandamina alizungumza na Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Ndola, Zambia ambapo alisema haridhishwi na mambo yanavyokwenda klabuni hapo huku akitoa sababu sita za kuondoka.

Katika madai yake hayo Lwandamina alieleza mambo hayo huku akimtuhumu Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, kuwa chanzo cha yeye kuondoka.

Hata hivyo, Mkwasa alilieleza Mwanaspoti kuwa suala la kocha huyo linaendelea kujadiliwa ndani ya vikao na kwamba, atatoa ufafanuzi karibuni.

Alichofanikiwa Yanga

Akiwa Yanga, Lwandamina alitengeneza kikosi kisichotabirika ambapo, licha ya changamoto za majeruhi mara kwa mara na ukata lakini bado kikosi chake kilionekana kupambana uwanjani.

Usajili alioufanya Yanga kwa kuwasajili Emmanuel Martin, Raphael Daud, Pius Buswita, Papy Kabamba Tshishimbi, Ibrahim Ajib, Gadiel Michael, Ramadhan Kabwili, Haji Shaibu ‘Ninja’ na Yohana Mkomola na makipa Ramadhan Kabwili na Youthe Rostand walimbeba zaidi kocha huyo katika msimu huu.

Mbali na hao pia aliwapandisha makinda kadhaa ambapo, kati yao Yusuf Mhilu alionekana kuwa na tija zaidi ambapo sasa ndiye winga anayeisaidia timu hiyo katika mechi sita alizoanza sasa na kuanza kumbeba Lwandamina.

Mkata umeme amuharibia

Usajili pekee uliomharibia Lwandamina ni ule wa kiungo mkabaji, Justine Zullu kutoka Zambia aliyepewa jina la mkata umeme ambaye alishindwa kufanya kile kilichotarajiwa na baadaye mkataba wake ukavunjwa.

Hata hivyo, usajili wa ambao Wanayanga watajivunia Yanga ikiwa chini ya Lwandamina ni kumnasa Papy Kabamba Tshishimbi, ambaye alimuona wakati akija nchini kwa mara ya kwanza na klabu yake ya zamani ya Mbambane Swallows ya Swaziland iliyokuwa ikipambana na Azam FC.

Baada ya kumuona kiungo huyo Lwandamina aliwaita mabosi wa Yanga na kuwataka kumsajili haraka ambapo, pia alisafiri mpaka Swaziland kumuangalia kwa mara ya pili kisha kufanikiwa kumsajili msimu huu na aliibeba zaidi timu hiyo.

Deni kwa Wanayanga

Deni kubwa ambalo Lwandamina ameliacha ndani ya Yanga ni kwamba kocha huyo hajawahi kuifunga Simba hata kwa bahati mbaya zaidi ya kupata sare moja kisha akapoteza mara tatu, lakini pia hajawahi kutwaa taji la FA.

Pia, ameiacha timu ikiwa kwenye vita ya kutetea taji la Ligi Kuu Bara, ambapo wameachwa kwa pointi nane na Simba mpaka sasa. Lwandamina ameondoka wakati Yanga pia ikikabiliwa na mchezo mgumu ugenini dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia kusaka nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.