Hawajui chenga, lakini kwa kupasia nyavu balaa

SOKA bana lina raha yake, kila mtu anakuwa na makali yake na ndio maana umekuwa mchezo unaowavutia watu wa aina tofauti duniani kote.

Kutokana na utamu wake huo, matajiri wanakubali kuwekeza pesa zao nyingi kwenye mchezo huo kwa sababu umekuwa biashara yenye faida, soka linalipa.

Lakini, kwenye mchezo huo, yatafanyika mashindano mengi, likifika Kombe la Dunia kila mchezaji anakuwa na hamu ya kwenda kuiwakilisha nchi yake katika michuano hiyo hasa kama watakuwa wamefuzu kucheza mikikimikiki hiyo.

Mwaka huu fainali za Kombe la Dunia zitafanyika Russia, ni kama siku 20 hivi zijazo ndio mambo yataanza. Huko watakutana mastaa wa aina tofauti, lakini miongoni mwa wakali utakaowashuhudia huko ni wale washambuliaji ambao hawajui kupiga chenga, wao wanachokifanya wanapokuwa ndani ya uwanja ni kuhakikisha mipira inagusa nyavu kuleta pointi tatu na hatimaye timu kwenda kubeba ubingwa.

Hawa hapa washambuliaji ambao wao wanapokuwa uwanjani wala hawajishughulishi na mambo ya kupiga chenga, labda itokee tu. Hawajui chenga, lakini kufunga tu hawajambo!

Romelu Lukaku, Ubelgiji

Kuna mashabiki wa Man United ambao mpaka keshokutwa hawakubali kama Lukaku ana hadhi ya kuchezea klabu yao, wana sababu zao.

Pia, wapo ambao huona kuwa mchezaji huyo ana mchango mkubwa katika mafanikio ya timu yao msimu huu. Ndiye kinara wa ufungaji katika mashindano yote pale Man United, pia amekuwa msaada kule Ubelgiji licha ya kuonekana kama mchezaji mzito katika kufanya mijongeo.

Huyu bwana yeye hana mbwembe kama za akina Cristiano Ronaldo, Neymar au Lionel Messi, yeye anachojua ni kufunga tu. Yupo katika kikosi bora cha Ubelgiji kwa sasa na ana nafasi ya kuendeleza moto wake wa kupasia nyavu kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Diego Costa, Hispania

Ulikuwa ukishuhudia alichokuwa anakifanya pale Chelsea? Alizaliwa kwa ajili ya kufunga mabao tu, habari za kupiga vyenga kusumbuana na mabeki alikuwa anamwachia Eden Hazard, Willian na Cesc Fabregas, yeye alichokifanya ni kukimbia tu kwenye eneo muhimu kwenda kusimama kusubiri mipira ije aisukumie wavuni.

Costa alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Chelsea kwa muda mfupi kabla hajatibuana na kocha Antonio Conte na kumwondoa kwenye kikosi chake kwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake.

Staa huyo amerudi zake Atletico Madrid, ambako amekwenda kuonyesha kiwango kikubwa na jina lake kujumuishwa kwenye kikosi cha Hispania kitakachokwenda kwenye fainali za Russia. Kwenye fowadi ya La Roja atapigania nafasi na wakali kama Rodrigo Moreno, Iago Aspas na wengine.

Olivier Giroud, Ufaransa

Ni kipenzi cha kocha Didier Deschamps huko kwenye kikosi cha Ufaransa. Baada ya kujiunga na Chelsea kwenye dirisha la Januari jambo hilo lilidaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kocha huyo wa Ufaransa, kwa sababu pale kwenye kikosi cha Arsenal alikuwa akisugua tu benchi.

Uzuri wa straika Giroud ni kwamba hahitaji dakika 100 kuonyesha uwezo wake, wee muweka tu benchi, lakini akiingia lazima aweke kwenye kamba.

Jambo hilo limemfanya kocha Deschamps kuamua kwenda naye huko Russia na kuacha washambuliaji wengine akiwamo Alexandre Lacazette.

Tofauti na washambuliaji wengine, Giroud, anafahamu vyema vipimo vya goli na ni hatari zaidi kwa mipira ya juu, anapiga vichwa balaa.

Mario Gomez, Ujerumani

Huwezi kuliweka kando jina la Mario Gomez kutoka kwenye hii orodha ya wachezaji ambao wao chenga sio mtaji wao kabisa na wanachofahamu ni kuupeleka tu mpira kwenye nyavu ili mashabiki washangilie na timu ipate ushindi.

Shughuli yake aliyoonyesha VfB Stuttgart ilimfanya kocha wa Ujerumani kumjumuisha kwenye kikosi chake akaonyeshe makali kwenye fainali za Kombe la Dunia ambapo kikosi hicho kitakwenda kujaribu kutetea ubingwa waliobeba miaka minne iliyopita kule Brazil.

Huko Russia washambuliaji wengine wa Ujerumani ambao wao wanajua kufunga na si kupiga chenga ni Thomas Muller na Timo Werner.