Hawa makocha tumwaachie Mungu tu!

Muktasari:

  • Lakini, chochote kinaweza kutokea kuhusu Jose Mourinho huko Manchester United juu ya usalama wake katika kibarua cha kuinoa timu hiyo. Wakati hilo likiendelea, kuna makocha hao kama itatokea wataendelea kubaki kwenye timu wanazozinoa kwa sasa, basi hiyo ni bahati kubwa. Yani hatima yao, tumwaachia Mungu tu!

PEP Guardiola ndiye kocha mwenye uhakika kwenye Ligi Kuu England kwa sasa. Mauricio Pochettino ni mwingine mwenye uhakika wake wa kuendelea kubaki kwenye timu anayoinoa kwa sasa hadi kufika msimu ujao, sawa na ilivyo kwa Jurgen Klopp huko Liverpool.

Lakini, chochote kinaweza kutokea kuhusu Jose Mourinho huko Manchester United juu ya usalama wake katika kibarua cha kuinoa timu hiyo. Wakati hilo likiendelea, kuna makocha hao kama itatokea wataendelea kubaki kwenye timu wanazozinoa kwa sasa, basi hiyo ni bahati kubwa. Yani hatima yao, tumwaachia Mungu tu!

Unai Emery (PSG)

Emery hajafutwa kazi hapohapo wakati PSG ilipotupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kwa kipigo kile cha jumla ya mabao 5-2 kutoka kwa Real Madrid ni suala la muda tu limebaki kwa kocha huyo kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Kushindwa kuisaidia PSG kuvuka hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni tatizo kubwa ambalo litakigharimu kibarua chake.

Ni wazi kabisa itakuwa maajabu makubwa kama Emery ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika.

Alan Pardew (West Brom)

Kuna mengi tayari yanasemwa kuhusu usalama wa kibarua chake. Hadi sasa inaelezwa kwamba ni maajabu kuona kocha huyo bado yupo kazini hadi wakati huu. Pardew anaweza asiwe na lawama za moja kwa moja kutokana na kiwango cha ovyo cha West Brom kwa msimu huu, lakini si kitu unachokitarajia kabisa kumwona akiendelea kuwa kocha wa timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika. Kocha huyo amepata ushindi mmoja tu katika mechi 16.

Arsene Wenger (Arsenal)

Arsene Wenger amepita wiki ngumu kabisa huko Arsenal baada ya kikosi chake kukumbana na vipigo vizito viwili mfululizo kutoka kwa Manchester City. Kwanza kwenye fainali ya Kombe la Ligi na pili kwenye Ligi Kuu England, mechi zote hizo kila moja alifungwa Tatu Bila. Kisha akapigwa na Brighton. Jambo hilo liliibua mjadala mzito kuhusu hatima yake kwenye kikosi cha Arsenal kabla ya kuja kuishinda AC Milan kwenye Europa League. Hata hivyo bado hakuna uhakika kama Wenger atabaki na kazi yake msimu ujao.

Zinedine Zidane (Real Madrid)

Kwenye La Liga msimu huu ni kitu isichopenda kabisa Real Madrid kukisikia, hali yao huko ni ovyo wameshindwa kabisa kuonyesha viwango vinavyopaswa kuonyeshwa na wababe hao. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hali si mbaya baada ya kutinga robo fainali na sasa watakabiliwa na mechi dhidi ya Juventus. Matokeo mengine kinyume cha kushinda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuna ubishi inaweza kuondoka na kichwa cha Zidane mwishoni mwa msimu huu.

Jupp Heynckes (Bayern Munich)

Kiungo, Arturo Vidal alikuwa mchezaji wa mwisho kabisa kusisitiza kwamba kocha , Jupp Heynckes ataendelea kubaki kwenye kikosi cha Bayern Munich hadi msimu ujao, labda hilo limetoka kwa mabosi. Kocha huyo mkongwe amefanya vizuri tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Carlo Ancelotti, Oktoba mwaka jana na amewawezesha Bayern kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, kwa umri wa Heynckes ni jambo linaloonekana wazi kuwapo kwa ugumu wa kuendelea baada ya msimu huu kumalizika.

Antonio Conte (Chelsea)

Conte kuondoka Chelsea kabla ya msimu mpya kuanza ni jambo linaloonekana kwamba ni wazi litatokea tu kutokana na uhusiano wake na mabosi wa timu hiyo. Kocha huyo wa zamani wa Juventus amekuwa akilalamika kwamba hapewi pesa za kutosha kufanya usajili na bosi Roman Abramovich haonekani kumpa Conte pesa ya kusajili jambo ambalo linaweka wazi kabisa mwisho wa msimu huu safari ya kuondoka Stamford Bridge itamhusu. Tayari makocha kadhaa wanahusishwa akiwamo Luis Enrique.

Sam Allardyce (Everton)

Everton walimnasa Allardyce wakiwa na matumaini makubwa ya kuwafanya wawe matata kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Kipindi anatua kwenye timu hiyo mambo yalikuwa magumu na akashinda mechi kadhaa kuweka mambo sawa kabla ya kila kitu kutibuka tena. Kwa mwendo wa kusuasua wa Everton kwa sasa unaona wazi kabisa beki huyo hawezi kuwa na maisha marefu kwenye kikosi hicho cha Goodison Park. Hawezi kubaki baada ya msimu huu kumalizika.

David Moyes (West Ham)

Tukio lililotokea hivi karibuni linaloihusu timu hiyo ni wazi kabisa David Moyes atajiona kama amefanya makosa makubwa kwa kukubali kuinoa West Ham United. Mashabiki wa timu huyo walichukua uamuzi hatari wa kuamua kuvamia uwanja na kuleta vurugu katika mechi yao iliyopita. Lakini, kubwa lililofanya hayo ni matokeo mabovu ya timu hiyo yanayowakera washabiki. Kuondokana na hatari kama hiyo, Moyes anaweza kuamua mwenyewe kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.