Hawa jamaa hawasemwi!

Muktasari:

  • Kwa sababu hiyo ya soka kuwa mchezo wa watu, kuna wachezaji wamefanikiwa kukutana na wenzao wa mataifa mbalimbali na kujikuta wakijifunza lugha nyingi zaidi.

SOKA limekuwa kitu kinachowaunganisha watu kutoka pande zote za dunia. Ndiyo maana kwa sasa kuna timu 32 zinashiriki fainali za Kombe la Dunia huko Russia na kuvutia mashabiki kutoka kila kona hata kama nchi zao hazipo kwenye michuano hiyo.

Kwa sababu hiyo ya soka kuwa mchezo wa watu, kuna wachezaji wamefanikiwa kukutana na wenzao wa mataifa mbalimbali na kujikuta wakijifunza lugha nyingi zaidi.

Hii ndiyo orodha ya watu wa mpira ambao wanazungumza lugha zaidi ya tano kwa ufasaha!

5.Petr Cech- Lugha 5

Kipa, Petr Cech aliwahi kusema amekuwa akizungumza lugha tatu tofauti na mabeki wake kwenye kikosi cha Arsenal. Kipa huyo mkongwe ana uwezo wa kuzungumza lugha tano kwa ufasaha. Ukiweka kando lugha ya taifa lake la Czech,anazungumza pia Kingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kihispaniola.

Alisema:”Nazungumza Kihispaniola na mabeki Hector Bellerin na Nacho Monreal. Kifaransa na Laurent Koscielny na nimekuwa nikizungumza pia na Mjerumani Per Mertesacker. Wakati mwingine wachezaji huo hawaelewi, lakini unapozungumza kwa lugha anayoifahamu inakuwa rahisi.”

4.Jose Mourinho- Lugha 6

Kwenye ubora wake, Kocha Jose Mourinho amebeba mataji 23 makubwa.

Lakini, hilo limekuwa rahisi kwake kulifikia kwa sababu imekuwa rahisi kwake kuzungumza na wachezaji wake kikosini kwa lugha zao. Kocha huyo Mreno ana uwezo wa kuzungumza lugha sita kwa ufasaha. Mourinho anazungumza Kireno, Kingereza, Kifaransa, kitaliano, Kihispaniola na Kikatalunya. Kutokana na kujua lugha nyingi jambo hilo lilimfanya apachikwe jina la mkalimani, kitu ambacho hakipendi kwelikweli.

3.Zlatan Ibrahimovic- Lugha 6

Mwenyewe anajiita mungu wa Miami. Kwenye maisha yake ya soka, straika wa kimataifa wa zamani wa Sweden amecheza kwenye timu nyingi sana huko Ulaya, Ibrahimovic ameweza kujifunza lugha nyingi na hivyo kumfanya awe na uwezo wa kuzungumza lugha sita kuifasaha, ambazo ni Kiswidishi, Kibosnia, Kifaransa, Hispaniola, Kiitaliano na Kingereza.

2.Henrikh Mkhitaryan- Lugha 7

Huwezi kusema umeorodhesha majina ya wachezaji wanaozungumza lugha nyingi kisha ukaliacha jina la staa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan. Miki anazungumza kwa ufasaha tena bila ya kusitasita Kijerumani, Kingereza, Kitaliano, Kireno, Kifaransa, Kirusi na lugha ya kwao, Kiarmenia.

1.Romelu Lukaku- Lugha 8

Ndiyo hivyo, straika wa Manchester United, Romelu Lukaku, pengine ndiye mwanasoka anayezungumza lugha nyingi zaidi. Fowadi huyo wa zamani wa Everton anazungumza lugha nane, hadi Kilingala kimo unaambiwa. Si unajua staa huyo ana asilia ya DR Congo, ameamua tu kuitumikia Ubelgiji kwenye soka la kimataifa. Wazazi wake ni Wakongo, hivyo amejifunza Kilingala, lugha ambayo ni mchanganyiko tu wa Kifaransa na Kiswahili. Lukaku anazungumza pia Kingereza, Kihispaniola, ambavyo alijifunza shule, huku akizungumza pia Kireno, Kijerumani na lugha nyingine kubwa zinazofahamika duniani. Kwa kifupi tu, straika huyo anazungumza lugha nane.