Hawa iko siku watakumbukwa

Tuesday October 10 2017

 

MWISHONI mwa miaka ya 80’ na mwanzoni mwa 90, iliibuka bendi ya muziki wa Rock Marekani iliyoitwa Nirvana.

Ilianzishwa 1987 na muimbaji na mpiga gitaa, Kurt Cobain, na mshikaji wake, Krist Novoselic na 1989 ikatoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa Bleach kupitia lebo ya Sub Pop.

Baadaye wakapata dili kwenye Lebo ya DGC Records, hapo ndipo namba ikatoka rasmi na wimbo wa ‘Smells Like Teen Spirit’ kutoka kwenye albamu yao ya pili ya Nevermind iliyotoka 1991, uliwapatia umaarufu mkubwa.

Hata hivyo, kinara wa bendi hiyo, Kurt Cobain, hakuwa na furaha akiamini ujumbe wake pamoja na maono yake ya kisanii vinatafsiriwa vibaya na jamii. Kurt Cobain, alijihisi jamii haimuelewi!

Hali hii ikamtesa na kumsababishia msongo wa mawazo na kutumbukia kwenye dawa za kulevya. Hatimaye 1994, akajiua akiwa na umri wa miaka 27 tu.

Aliacha ujumbe aliomuandikia rafiki yake wa utotoni, Toddah.

Alianza kwa kuandika

“Kwako Toddah.”

Halafu akaandika.

“Sijawahi kupata ile raha ya kusikiliza pamoja na kutengeneza muziki sambamba na kuusoma na kuuandika kwa miaka mingi. Najihisi nina hatia kubwa zaidi maneno haya kuhusiana na vitu hivi.”

Maneno haya ndiyo yaliyotoa mwanga na kuwafumbua watu macho kwamba Cobain alijiua, kwa kuunganisha na yale aliyokuwa akiyasema wakati wa uhai wake.

Kurt Cobain alilalamika kutoeleweka katika jamii ambayo alikuwa akiitumikia, akajiua.

Kutoeleweka kunaumiza sana, hasa unapoamini unachokifanya ni sahihi na unakifanya kwa dhati ya moyo wako wote!

Hapa nchini, kwenye tasnia mbalimbali ikiwemo ya michezo, kuna watu kadhaa ambao wamejitolea kwa nyoyo zao zote kufanya mambo kupitia nafasi zao, lakini kwa bahati mbaya, taasisi hizo hazikuwaelewa...wakajikuta wakiumia moyoni na baadaye kuondoka kwa shingo upande!

1. DK TIBOROHA NA YANGA

Msomi huyu ni mtu wa mpira kweli kweli. Amefanya kazi kwa miaka mitano kwenye akademi ya klabu ya Malmo ya Sweden, alikotokea Zlatan Ibrahimovic.

Akiwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Tiboroha, alikuja na mipango ya kuifanya Yanga ijitegemee. Alifanya mazungumzo na makampuni kadhaa kwa ajili ya udhamini na yalikubali.

Aliongea na kampuni moja ya ndege, ili iwe inaisafirisha Yanga kwenye mechi zake za Ligi Kuu kwa sharti nembo ya kampuni hiyo iwepo kwenye jezi za Yanga.

Aliongea na kampuni moja ya kutengeneza jezi ili itengeneze na kuuza jezi za Yanga. Makubaliano yalikuwa jezi ziuzwe kupitia matawi ya Yanga tu, nchi nzima. Jezi moja iuzwe Sh 20,000 nusu iende kwa mtengenezaji na nusu iende klabuni. Katika zile 10,000 za klabu, kila tawi litakalouza jezi litapewa 3,000 kwa kila jezi moja halafu elfu. Anasema lengo lake lilikuwa kuyawezesha matawi kiuchumi kwa sababu Yanga ni mali yao.

“Matawi haya yakiwezeshwa kiuchumi, Yanga itafaidika zaidi kwa sababu wanachama ndiyo wateja wetu. Wakiwa na uwezo kifedha, watanunua bidhaa zetu zaidi. Kimsingi ni kama ilikuwa tuwakopeshe halafu warudishe kwa mlango mwingine.”

Lakini viongozi wake (kiongozi wake) hawakumuelewa. Anasema siku alipopeleka makubaliano haya kwa bosi wake, ndiyo ikawa mwisho wa kuongea naye. Bosi akawa hapokei simu yake wala hajibu barua pepe, mpaka alipofukuzwa. Hakueleweka...akaondoka!

2. KILOMONI NA SIMBA

Joto la mabadiliko halijawahi kumuacha mtu salama. Labda hivi ndivyo unavyoweza kuuelezea mkasa wa Mzee Hamisi Kilomoni.

Mzee huyu ambaye ametoa mchango mkubwa kuifikisha Simba hapa ilipo, alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo. Viongozi wa klabu walikuwa na lengo zuri, la kuleta mabadiliko ya mfumo endeshi wa klabu. Kimsingi kwa mazingira ya sasa, lazima mabadiliko yaje.

Lakini Kilomoni mara zote alilalamika uongozi haukumshirikisha kujua mfumo ukoje. Alichotaka ni kukaa na uongozi umuoneshe (yeye na wadhamini wenzake) pendekezo (proposal) la mabadiliko ili, kama mdhamini, aelewe inakoelekea klabu.

Kilomoni alikuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini. Majukumu yao ya msingi ni kulinda mali ya klabu. Haiwezekani klabu inaingia kwenye mabadiliko makubwa kiasi hicho akiwa hajui lolote. Kulikuwa na ugumu gani kwa viongozi wa Simba kukaa naye (na bodi nzima kwa ujumla) kumuelewesha mpaka aelewe?

Mzee akahisi kuna ujanja unafanyika wa kuiuza klabu kwa tajiri fulani. Akiwa kama mtu aliyetumia ujana wake wote kuijenga Simba bila kulipwa chochote, lazima aumie anapoona mali aliyoitolea jasho, akiamini ni ya wanachama wote, leo inauzwa kwa mtu mmoja.

Mzee Kilomoni aliichezea Simba miaka ya 1950 (Simba ikiwa na umri wa chini ya miaka 20) akastaafu. Akawa Naibu Katibu Mkuu, aliyekuwa Katibu Mkuu alikuwa mtumishi serikalini hivyo hakutulia ofisini. Kazi zote za kiofisi zikawa zinafanywa na Kilomoni.

Ndiye aliyekuja na wazo la kujenga ofisi za makao makuu ya klabu. Wakati huo Simba ikiwa imepanga chumba kimoja tu Mtaa wa Kongo kama makao makuu yao.

Akalisimamia wazo laa kuhamasisha wanachama jengo likakamilika. Leo anaona klabu inauzwa, kwanini asipige kelele?

Kumbe kimsingi, Simba haiuzwi ila kilichotakiwa ni viongozi kumuelewesha tu. Viongozi hawakumuelewa mzee anataka nini. Wanachama, ambao wengi wao hata hawaijui historia ya mzee huyu, nao hawakumuelewa anataka nini. Wakamtafsiri hataki mabadiliko, wakamtimua kwenye bodi ya udhamini na kumsimamisha uanachama kwa tishio kali la kufukuzwa kabisa endapo hatafuta kesi aliyoifungua mahakamani.

Kufungua kesi ya mpira kwenye mahakama za kawaida ni kosa, lakini kuna makosa mengine husababishwa na mazingira na hata hukumu zake huzingatia mazingira.

Kwa mfano, mchezaji wa zamani wa Yanga, Herry Morris Ng’onye alitoroka Yanga na kwenda Uarabuni kusakata soka la kulipwa. Lakini akakwama kutokana na kukosa ITC, akarudi. Yanga wakataka kumfungia lakini wadau wengi wakamuombea msamaha, akiwemo kiongozi mmoja wa DRFA alipohojiwa na Maulid Kitenge wa Radio One. Alisema, ‘kuiba ni kosa, lakini wanapokamatwa watu wawili wameiba mbuzi, mmoja alitaka amuuze ili apate hela za disco na mwingine alitaka ampatie supu mkewe aliyetoka kujifungua, kwa kushauriwa na daktari, huyu wa supu unaweza kumuonea huruma’.

Mzee Kilomoni hakufungua kesi kwa kukataa mabadiliko, ila alijaa hofu ya kuuzwa kwa klabu hii, ambayo wao wanaichukulia kama urithi wa vizazi na vizazi. Alitakiwa tu aeleweshwe. Lakini hakuna aliyemuelewa!

3. PLUIJM NA YANGA SC

Msimu wa 2015/16 ulikuwa wa kihistoria kwa Yanga. Ilishinda ubingwa wa Ligi Kuu ikipoteza mchezo mmoja tu (rekodi yao). Ilishinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports na ilifika hatua ya makundi ya Afrika. Kukazia hapo, ilipata ushindi wa kwanza katika historia ya miaka zaidi ya 80 ya klabu hiyo kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afrika, walipoifunga Mo Bejaia ya Algeria, 1-0.

Ilimaliza ligi ikiwa na pointi 73 ni rekodi hapa nchini. Tangu ligi ya Tanzania ianze 1965. Kabla ya hapo, rekodi ilikuwa pointi 70 ambazo Yanga wenyewe walizipata 2006.

Mafanikio yote haya yaliambatana na soka la uhakika chini Mholanzi huyo. Lakini ulipoanza msimu mpya wa 2016/17, mambo hayakuanza vyema kwa Yanga na mbuzi wa kafara akawa moja kwa moja, Hans van der Pluijm.

Mabosi wa Yanga hawakuelewa timu yao ilikuwa imecheza mfululizo mwaka mzima bila kupumzika hivyo wachezaji walikuwa na uchovu.

Wakati Ligi ya Tanzania msimu wa 2015/16 inamalizika mwezi Mei, hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Caf ikaanza. Hatua ya makundi iliendelea mpaka msimu mpya wa 2016/17 ulipoanza. Wachezaji kama binadamu, walichoka hivyo haikuwa kosa la kocha timu kuanza kwa kusuasua.

Lakini mabosi wake hawakumuelewa, Hans akaondoka.

Usikose uhondo huu, makala haya yataendelea tena wiki ijayo.