HAWA WAKITUA TU ITAPENDEZA ZAIDI

Muktasari:

Wakati dirisha hilo likikaribia, hii hapa orodha ya mastaa wanaosakwa na klabu vigogo wa Top Six kwenye Ligi Kuu England na kama makocha wa timu hizo atafanikiwa kuwanasa basi itapendeza sana.

London, England. DIRISHA la usajili wa Januari linazidi kukaribia kabisa, ni mwezi tu na siku kadhaa zimebaki kabla ya timu hazijaruhusiwa kufanya usajili wa kuuza na kununua wachezaji kwa mara nyingine. Wakati dirisha hilo likikaribia, hii hapa orodha ya mastaa wanaosakwa na klabu vigogo wa Top Six kwenye Ligi Kuu England na kama makocha wa timu hizo atafanikiwa kuwanasa basi itapendeza sana.

Arsenal, Nabil Fekir

Habari kubwa kuhusu usajili wa Arsenal kwenye dirisha lijalo la Januari ni kuhusu mpango wao wa kumchukua Raheem Sterling kutoka Manchester City. Kwenye dirisha lililopita, Arsenal walitaka kufanya mabadilishano na Man City, wao wawape Alexis Sanchez na wao wamchukua Sterling, ikashindikana.

Lakini, katika dirisha lijalo la usajili, kocha Arsene Wenger ametajwa kuwa na mipango ya kumsajili staa wa Olympique Lyon, Nabil Fekir, ambaye thamani yake inatajwa kuwa ni Pauni 60 milioni. Arsenal wanaonekana kuwa siriazi katika mpango wa kupata saini ya mchezaji huyo huku wakimsaka pia kinda wa Kiingereza, Bobby Duncan, anayecheza kwenye kikosi cha Man City, akiwa mpwa wa gwiji la Liverpool, Steven Gerrard.

Chelsea, Alex Sandro

Kocha, Antonio Conte anapiga hesabu za kuboresha kikosi chake katika dirisha lijalo la usajili wa Januari ili kuendelea kupambana na hali yake katika kuufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England. Mchezaji ambaye Conte anamtaka ni yuleyule aliyeanza kumsaka tangu kwenye dirisha lililopita, wing-back wa Juventus, Alex Sandro. Staa huyo wa Kibrazili ameripotiwa kwamba, atamgharimu Conte pesa isiyopungua Pauni 60 milioni. Mchezaji mwingine anayemsaka Conte ili kumwongeza katika kikosi chake hicho cha Stamford Bridge ni kiungo fundi wa mpira wa Paris Saint-Germain, Javier Pastore, huku akitajwa pia Lucas Moura kutoka kwa wababe hao hao wa Ufaransa.

Liverpool, Thomas Lemar

Kocha, Jurgen Klopp ameambiwa wazi na RB Leipzig kwamba hataruhusiwa kumchukua kiungo Naby Keita katika dirisha la Januari, jambo litakalomfanya kufikiria kufanya usajili wa mchezaji mwingine au wachezaji wengine katika kukipa nguvu kikosi chake ili wapambane sambamba kabisa katika kuukimbizia ubingwa wa Ligi Kuu England.

Shida kubwa ya Klopp ipo kwenye safu ya kiungo na mahali hapo ndipo anapopafanyia kazi ili kupata wachezaji wa maana, huku kwenye orodha yake ya wachezaji wanaowindwa huko Anfield, ambao wanaweza kusajiliwa Januari ni Christian Pulisic, Thomas Lemar na Leon Goretzka. Mastaa wengine ambao Klopp anawataka ni Morgan Gibbs-White wa Wolves na Kai Havertz wa Bayer Leverkusen.

Man City, Alexis Sanchez

Kwa ilivyo Manchester City kwa sasa ni ngumu kufikiri kwamba, kocha Pep Guardiola ataingia sokoni katika dirisha la Januari kufanya usajili wa staa mwingine wa kuingia kwenye timu yake. Ukiitazama Manchester City kwa sasa unaona ipo fiti karibu kila idara hasa kutokana na kucheza mechi 15 sasa bila ya kupoteza huku wakiongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Lakini, Guardiola anapiga hesabu za kumwongeza staa wa Arsenal, Alexis Sanchez kwenye kikosi chake huku huduma ya mchezaji huyo ikipatikana huko Etihad basi huenda ikamlazimisha Raheem Sterling kwenda upande mwingine. Sterling amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu, akifunga mabao 10, lakini Guardiola anaweza kukubali kumtoa ili amchukue Sanchez, ambaye alishindwa kumnasa katika dakika za mwisho kabisa katika dirisha lililopita.

Man United, Saul Niguez

Kutokana na kikosi chake kukabiliwa na majeruhi kibao, kocha Jose Mourinho ameshaanza kufikiria mpango wa kuboresha kikosi chake kuhakikisha kinaendelea kukimbizana na wapinzani wao kwenye mchakamchaka wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England. Mipango ya Mourinho kwenye dirisha hilo lijalo ni kumsajili staa wa Atletico Madrid, Saul Niguez, ambaye anaonekana wazi kabisa atakuwa tayari kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Old Trafford. Mourinho anafahamu wazi itakuwa ngumu kupata saini ya mchezaji kama Antoine Griezmann katika dirisha la Januari, labda hadi hapo itakapofika mwisho wa msimu ambapo, hata bei ya Mfaransa huyo itakuwa imepungua pia kutokana na kipengele kilichoelezwa katika mkataba wake. Staa mwingine anayewindwa na Mourinho kwenye dirisha hilo la Januari ni Carlos Soler wa Valencia.

Tottenham, Richarlison

Kuwafikiria Tottenham Hotspur kwamba watafanya usajili katika dirisha la Januari ni jambo gumu kidogo kutokana na idadi ya wachezaji waliopo kwenye timu hiyo, kuona kuna wengine kibao bado hawajapata nafasi ya kucheza.

Lakini, kocha Mauricio Pochettino ameweka wasiwasi juu ya straika wake, Harry Kane na kutaka kumpatia mchezaji mwingine wa kusaidiana naye na kuokoa jahazi wakati Mwingereza huyo anapokuwa mgonjwa.

Ripoti zinadai kwamba, Pochattino anamtaka staa wa Watford, Richarlison, ambaye amekuwa muhimu kweli kweli huko Vicarage Road tangu alipotua kwenye dirisha lililopita. Spurs pia inahusishwa na mpango wa kumsajili winga matata wa Real Sociedad, Mikel Oyarzabal.