EPL, Inategemea nani atajigeuza Van Damme?

Muktasari:

  • Van Damme angepigwa sana. akawa hoi. Akawekewa sumu katika macho. Mwishowe akaibuka mshindi. Ndivyo itakavyokuwa katika Ligi Kuu England miaka 30 baadaye. Namaanisha msimu huu ulioanza jana.

MIAKA 30 kamili sasa tangu ilipotoka Movie ya Bloodsport. stelingi wetu alikuwa Van Damme. Adui yake alikuwa Bolo Yeung. Nyakati zinakwenda wapi? Mwaka 1988 mpaka leo. Hatupati filamu zenye mvuto tena.

Van Damme angepigwa sana. akawa hoi. Akawekewa sumu katika macho. Mwishowe akaibuka mshindi. Ndivyo itakavyokuwa katika Ligi Kuu England miaka 30 baadaye. Namaanisha msimu huu ulioanza jana.

Sahau kuhusu kilichotokea jana Old Trafford. Una uhakika gani City itachukua ubingwa? Inapewa nafasi, sawa, lakini ni ngumu kutabiri. Timu ya mwisho kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya England ilikuwa Manchester United misimu 10 iliyopita. Kitu kinachoitwa Second Season Syndrome kinawaumiza mabingwa wowote wa England kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Hii ina maana hii. Kwamba unatumia nguvu sana kuchukua ubingwa halafu msimu unaofuata unajikuta umechoka. Unajikuta katika wakati mgumu wa kutetea.

Timu ngumu ni nyingi siku hizi. Zamani Sir Alex alikuwa akimpiku Arsenal tu, basi anachukua ubingwa. Akaja Jose Mourinho wakati Arsene Wenger alivyoanza kuzeeka vibaya. Mourinho alikuwa akimpiku Sir Alex tu, basi anachukua ubingwa. Siku hizi hakuna maisha hayo. Pep Guardiola inabidi apambane. Kilichoitokea Chelsea halafu Leicester ni mfano. Unachukua ubingwa halafu msimu ujao unaondoka Top Four. Kwa heshima zangu zote kwa Pep, najua hawezi kuondoka Top Four.

Halafu kuna hawa Liverpool. wamechukua ubingwa tayari nje ya uwanja. Kila mtu anaamini wanaweza kuwa mabingwa, ikiwemo mimi. Wamekwenda ATM wakachukua pesa nyingi wakaingia sokoni. Wametibu matatizo yao yote.

Tatizo ni kwamba sio lazima waanzie walipoishia. Sio lazima Mohamed Salah awe yuleyule wa mwaka jana. Sio lazima kombinesheni ya Sadio Mane, Roberto Firmino na Salah ianzie palepale ilipoishia. Wakati mwingine soka ni mchezo wa maajabu. Unaweza kutibu miguu iliyosumbua kwa muda mrefu halafu baada ya kupona ghafla kichwa ambacho kilikuwa kizima kwa muda mrefu kikaanza kukusumbua.

Lakini, pia inabidi wawe na akili iliyokomaa katika kutwaa ubingwa (strong mentality). Liverpool ina akili iliyokomaa katika Ligi ya Mabingwa. Ina kitu fulani hivi ambacho hakielezeki. Inaweza kukosekana kwa muda mrefu katika michuano hiyo lakini ikirudi inafika nusu fainali, au fainali, au kuchukua kabisa ubingwa wenyewe.

Uzuri wa Ligi ya Mabingwa ni mbio za Usain Bolt. Ni mbio fupi. Ligi ya England ni mbio za Haile Gebrselassie wa Ethiopia. Ni Marathon. Zinahitaji ukomavu wa akili sana. Kuna wakati unapigwa ngumi za Mike Tyson lakini bado unasimama na kukimbia. Liverpool itaweza?

Kuna rafiki zangu, Manchester United. Wamenunua mchezaji mmoja tu timilifu. Fred. Mbrazil huyu. Ametokea Shakhtar ya Ukraine. Mwingine ni dogo na jina lake linafanana na Dogo. Anaitwa Diogo. Huyu bado hajathibitisha sana ubora wake kwa sababu ni kinda. Jose Mourinho amenuna kwa United kutoongeza watu wa nguvu. Mashabiki wamenuna. Lakini bado nasisitiza, katika timu yenye Anthony Martial, Romelu Lukaku, Marcus Rashford, Paul Pogba, Fred, Antonio Valencia, Nemanja Matic, Juan Mata, Alexis Sanches na wengineo, mbona nawaona wachezaji wanaoweza kukupa ubingwa?

Labda macho yangu yameanza kuzeeka. Tatizo ni Jose mwenyewe. Anaivuruga timu. anagombana na kila kitu kilicho mbele ya macho yake. Waamuzi, wachezaji wake, wachezaji wa timu pinzani, mabosi wake, na kila mtu anayemuona mbele yake. Mbona Manchester United ni nzuri tu?

Jose ataivuruga timu ambayo licha ya kutofanya usajili mkubwa lakini bado ina washindi ndani yake. Tatizo ni fomesheni yake na tabia yake nje ya uwanja. Kama akituliza akili na kuwakubali mastaa wake, wakamkubali pia, wakampigania, United inaweza kuwania ubingwa au kuuchukua kabisa.

Kuna hawa Arsenal. Kwanini watu wanawapuuza? Kwa sababu wamewakariri. Walikaa na kocha mmoja kwa miaka mingi na baadaye mashabiki wa timu pinzani wanaipa timu mpya yenye kocha mpya, sura ya kocha wa zamani. Ni kosa.

Naweza kuweka pesa kubashiri Arsenal itashika nafasi tatu za juu. Ina kocha ambaye staili yake ya soka ni ya Pep. Lakini katika misimu mitatu iliyopita, Arsene Wenger alinunua wachezaji wengi wazuri. Tatizo alibakia kuwa mwenyewe tu.

Ni me andika zaidi ya mara mia, tatizo la Arsenal lilikuwa Arsene. Leo ina kocha mpambanaji, kijana, ana ari na hamasa. Na zaidi ana wachezaji wazuri. Lolote linaweza kutokea. Watu watashangaa lakini mimi sitashangaa Arsenal ikiwa bingwa, au ikiwa ya pili au ikiwa ya tatu.

Unai Emery alichukua mataji matatu ya Europa mfululizo. Sio kitu kidogo. Unai Emery akiwa na hiyohiyo Sevilla alishika nafasi ya tatu nyuma ya Real Madrid na Barcelona mara mbili mfululizo. Aliwashangaza watu kwa kutumia bajeti ndogo sana. Kilichoibeba timu ni ujuzi wake.

Usiwachukulie poa Arsenal. Watawashangaza watu wengi. Staili za soka za Pep na Jurgen Klopp ndio staili ya soka ya Unai. Anahitaji muda kidogo lakini ni kocha mwafaka kwa Arsenal, na ni katika wakati mwafaka. Hapana shaka. Chelsea? Ililianza dirisha vibaya lakini imeimarika baadaye. Ghafla inaelekea kumbakisha Eden Hazard. Ni jambo kubwa katika hii timu kuliko kununua mchezaji mpya. Kwanza unambakisha Hazard na mengineyo yanafuata.

Lakini ghafla ina mastaa watatu hatari katika eneo la kiungo. N’Golo Kante, Jorginho na Mateo Kovacic. Timu yao sasa imeundwa hapo baada ya msimu uliopita kuhangaika na kina Bakayoko. Lakini pia kocha mpya, Maurizio Sarri ni mtu mwenye mbinu katika soka la kasi na la kushambulia ambalo litawafurahisha Hazard na Willian.

Tatizo ni Alvaro Morata na Olivier Giroud tu basi. Watabeba majukumu ya kufunga mabao 20 kwa msimu? Walau mmoja wao tu. Tusubiri.

Tottenham wanoanekana kukaa kimya. Wameweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya EPL kutonunua mchezaji tangu pazia la uhamisho lianzishwe rasmi mwaka 2003. Nadhani uwanja umewabana. Wamejaribu kupigapiga chenga dirisha hili lakini nadhani Mwenyekiti wao, Daniel Levy amepeleka pesa katika ujenzi wa uwanja.

Ataishia kuwania Top Four tu. pia ana kina Lucas Moura na Fernando Llorente ambao hawakutumika sana msimu uliopita. Labda watakuja kumsaidia. Vyovyote ilivyo, ubingwa hautapatikana kiurahisi. Wala Top Four haitapatikana kiurahisi. Aliyekariri Arsenal haitakwenda Top Four atashangazwa, Chelsea itabakia nje ya Top Four naye atashangazwa.

Aliyekariri City au Liverpool mojawapo itachukua ubingwa anaweza na United haitawania ubingwa anaweza kushangazwa pia. Bingwa atapatikana kwa kupigana pambano la Van Damme. Atalazimika kuwa hodari zaidi njiani. Haitakuwa rahisi sana.

haitakuwa kama msimu uliopita bingwa alipatikana kwa tofauti ya pointi 18.

Bingwa inabidi apatikane kwa mateke ya mwisho kidogo. Kama Jean-Claude Van Damme.