Clasico 5 Bernabeu

Muktasari:

  • Kuna mechi kali baina ya Madrid na Barcelona ambazo zimepigwa Santiago Bernabeu lakini zifuatazo zinaweza kuwa tano kali zaidi kupigwa katika zama hizi katika uwanja huo.

KESHO ni El Clasico. Moja kati ya mechi kubwa zaidi duniani katika ngazi ya klabu. Ni Real Madrid dhidi ya Barcelona pale Santiago Bernabeu.

Kuna mechi kali baina ya Madrid na Barcelona ambazo zimepigwa Santiago Bernabeu lakini zifuatazo zinaweza kuwa tano kali zaidi kupigwa katika zama hizi katika uwanja huo.

Real Madrid 4-1 Barcelona, 7 Mei 2008

Barcelona ilikuwa katika msimu mbovu zaidi pale Hispania na ilikwenda katika mji mkuu wa Hispania huku ikilazimika kujipanga na kutoa heshima kwa wachezaji wa Madrid waliokuwa wametoka kutawazwa ubingwa wa La Liga.

Hata hivyo, kikosi cha Kocha Frank Rijkaard kilijikuta katika majanga zaidi katika Uwanja wa Santiago Bernabeu. Mkongwe, Raul Gonzalez ndiye aliyeanzisha madhara katika lango la Barcelona kwa kufunga bao la kwanza kabla ya mabao ya Arjen Robben, Gonzalo Higuaín na penalti iliyopigwa na Ruud van Nistelrooy.

Barcelona ilifanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Thierry Henry. Ilikuwa siku mbaya kwa Barcelona.

Real Madrid 0–3 Barcelona, 19 Novemba 2005

Moja kati ya mechi iliyoshuhudia kipaji binafsi cha mchezaji mmoja katika histoa ya La Liga. Kiungo mchezeshaji wa Brazil, Ronaldinho alikuwa katika ubora wake katika pambano hili ambalo Barcelona ililitawala kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Mshambuliaji wa Barcelona, Samuel Etoo aliipatia Barcelona bao la kuongoza lakini Ronaldinho akafunga bao la pili na la tatu kwa juhudi binafsi. Ulikuwa ushindi mtamu wa amri kwa Barcelona kupitia juhudi za mchezaji mmoja kama mkongwe wa Uholanzi, Johan Cruyff alivyofanya wakati Barcelona ikiibomoa Real Madrid mabao 5-0 mwaka 1974.

Wakati Ronaldinho alipokuwa akitolewa nje kabla ya pambano hilo kumalizika, mashabiki wa Real Madrid walionekana wakisimama na kupiga makofi ya kumpongeza Ronaldinho licha ya kuiharibu timu yao. Inatokea mara chache sana.

Real Madrid 2-6 Barcelona, 2 Mei 2009

Katika pambano hili, Real Madrid ingeweza kupunguza pengo lake na Barcelona kufikia pointi moja tu. Ilionekana kama vile ingekuwa siku njema kwao wakati mshambuliaji wa Argentina, Gonzalo Higuain alipofunga katika dakika ya 14 tu. Lakini Thierry Henry alisawazisha bao hilo haraka haraka. Baadaye kidogo, nahodha, Carles Puyol alifunga kwa kichwa na kuipatia Barcelona bao la kuongoza. Kuanzia hapo kikosi cha Kocha Pep Guardiola hakikutazama nyuma. Kilipiga soka maridadi ambalo liliwapa uhalali wa kutangaza ubingwa katika dimba la Santiago Bernabeu.

Lionel Messi alifunga bao la tatu lakini Sergio Ramos akaweka matumaini hai ya kusawazisha kwa kufunga kwa kichwa. Hata hivyo, ilikuwa imechokoza hasira za Barcelona ambayo ilifunga mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Henry na Messi kabla ya beki, Gerard Piqué kufunga bao la sita kwa umaridadi mkubwa.

Real Madrid 4–2 Barcelona, 10 Aprili 2005

Wakati Barcelona ikitishia kuondoka na ubingwa wa La Liga, staa wa England, David Beckham aliinyanyua Real Madrid kwa ushindi mzuri dhidi ya watani hao na hivyo kuibua upya mbio za ubingwa. Kwanza ilianzia kwa Zinedine Zidane ambaye alifunga bao la kuongoza katika dakika ya saba tu na baada ya dakika 20 staa wa kimataifa wa Brazil, Ronaldo de Lima aliongeza bao la pili kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa vizuri na Beckham. Samuel Eto’o alipunguza deni kubwa lililokuwa linaikabili Barcelona kwa kufunga bao la kwanza la Wakatalunya hao lakini mkongwe Raul Gonzalez akatanua uongozi wa Madrid kwa kufunga bao la tatu. Kama vile haitoshi, Beckham aliendelea na kazi yake ya kupika mabao kwa kumtengenezea Muingereza mwenzake, Michael Owen bao la nne kabla ya Ronaldinho kufunga bao la pili kwa Barcelona zikiwa zimebakia dakika 20 kabla ya pambano hilo kumalizika.

Real Madrid 3-4 Barcelona, 23 Machi 2014

Hapana shaka pambano hili lililozaa mabao saba linabakia kuwa moja kati ya mechi za kuvutia zaidi katika historia ya Clasico. Barcelona iliingia katika mechi ikiwa nyuma kwa pointi nne dhidi ya wapinzani wao Madrid na ilikuwa katika hatari ya kutupwa nje ya mbio za ubingwa. Bahati nzuri ilipata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo wake maridadi, Andrés Iniesta. Real ilirudi mchezoni kwa kasi na kupata mabao mawili kupitia kwa staa wake wa kimataifa wa Ufaransa, Karim Benzema, huku mabao yake yote mawili yakiwa yamefungwa na Ángel di María, lakini Barcelona kupitia kwa mchawi wake wa Kiargentina, Lionel Messi ilisawazisha bao hilo. Madrid ikarudi tena mchezoni kwa kufunga kwa penalti kupitia kwa Cristiano Ronaldo lakini baadaye Barcelona ikazawadiwa penalti mbili ambazo zote zilipigwa na Lionel Messi na kutinga katika nyavu za Madrid. Vijana wa Kocha Tata Martino waliondoka na pointi zote tatu Bernabeu.