Chelsea inawakanganya matajiri wanaoiwania

Muktasari:

  • Hawana uhakika iwapo kocha wao, Antonio Conte atabaki kwa msimu ujao, mtu ambaye msimu uliomalizika alikuwa akilalamika sana juu ya wakubwa wa Stamford Bridge kutonunua wachezaji nyota na kusema hata yeye mwenyewe hajui atakuwa wapi msimu ujao.

CHELSEA wapo njia panda baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi huku wakikosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), huku pia wakivuliwa ubingwa na Manchester City.

Hawana uhakika iwapo kocha wao, Antonio Conte atabaki kwa msimu ujao, mtu ambaye msimu uliomalizika alikuwa akilalamika sana juu ya wakubwa wa Stamford Bridge kutonunua wachezaji nyota na kusema hata yeye mwenyewe hajui atakuwa wapi msimu ujao.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa kocha, kuna wachezaji ambao wameamua kusita kutia saini mikataba mipya, tena wachezaji waandamizi kama golikipa chaguo la kwanza, Thibaut Courtois anayetaka kwenda Real Madrid iliko familia yake, pia Eden Hazard anayetakiwa pia na Real Madrid.

Kwa jumla hakuna kinachoendelea sana kwa sababu ikiwa hujui nani anakuwa kocha msimu unaofuata na kocha hajui nani anabaki, hali inakuwa ngumu, hasa kinapokuwa ni kipindi cha usajili kikiambatana na fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi ambako wachezaji wengi hodari wanakuwa.

Hata hivyo, yote hayo tisa, kumi ni umiliki wa klabu na mipango mikubwa ya kiuchumi. Ni muda sasa tangu visa ya mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich iishe na Serikali ya Uingereza kusita kumpa mpya kiasi cha yeye kuamua kwenda kuomba Israel ambako alifanikiwa.

Mrusi huyu amekuwa mwathirika wa ‘vita’ ya kidiplomasia baina ya Urusi na Uingereza, hasa baada ya jasusi wa zamani wa Urusi na bintiye kudhuriwa kwa kuwekewa sumu na watu wanaochukuliwa na Uingereza kuwa ni Warusi, tena ndani ya ardhi ya Uingereza.

Pia Serikali ya Waziri Mkuu Theresa May imedhamiria kuwabana mabilionea wa Urusi walio nchini Uingereza bila kujali wanatengeneza ajira na kukuza uchumi, ikitaka kuja na kifungu cha sheria kuwabana waeleze asili ya utajiri wao. Ni katika hali hiyo, ameibuka tajiri mkubwa zaidi Uingereza, Jim Ratcliffe akitaka kuinunua klabu ya Chelsea. Inaelezwa tayari amewasilisha dau kwa tajiri huyo, akikadiria Pauni 20.05 bilioni, ndicho kiasi kinachofaa.

Ratcliffe ni shabiki wa Manchester United, na ununuzi wa Chelsea unaonekana utaondoa ushindani wa kweli baina ya klabu hizo mbili kubwa England, kati ya zile sita, nyingine zikiwa ni Manchester City, Arsenal, Liverpool na Tottenham Hotspur.

Zipo taarifa Abramovich hajakubali kuuza klabu kwani bado anapambana kuona iwapo atapata visa, lakini ugumu wa mambo unadhihirika kwa sababu mradi wa ufumuaji na ujenzi upya wa Uwanja wa Stamford Bridge, ikiwa ni pamoja na hatua za awali za makadirio na michoro, zimesitishwa kabisa.

Kwa hiyo hali ilivyo, wafanyakazi wakiwamo makocha na wachezaji hawana hata uhakika iwapo mwajiri wao atakuwa nao, ataruhusiwa kuingia na kuendelea na uwekezaji wake, ataendesha akiwa nje ya nchi au atamuuzia mtu au kampuni nyingine. Hiyo si hali yenye kutia afya kisoka.

Abramovich amemiliki klabu hiyo kwa miaka 15 sasa na inaelezwa licha ya Ratcliffe, kuna watu na kampuni nyingine kadhaa zinaitaka klabu hiyo maana imeshajijenga vya kutosha na sasa ni kiasi cha kuiendesha. Wachina nao wamo kwenye kutafuta dili hilo la Chelsea.

Ratcliffe, mmoja wa watu ambao Malkia Elizabeth II aliwatunukia cheo cha heshima ya ushujaa katika huduma kwenye biashara na uwekezaji, tayari anamiliki klabu nchini Uswisi na utajiri wake ni zaidi ya mara mbili wa huo alio nao Abramovich.

Huwa anakwenda kwenye mechi za nyumbani za Chelsea, kwa sababu nyumbani kwake ni karibu na Stamford Bridge, pia huenda Cobham – uwanja wa mazoezi wa Chelsea kuwatazama.

Hivi karibuni gazeti la Sunday Times katika orodha yake ya matajiri, lilimweka Ratcliffe kuwa na utajiri wa Pauni 21 bilioni wakati Abramobich anao wa Pauni 9.3 bilioni. Ukweli, ikiwa itauzwa, Chelsea itagharimu zaidi ya Pauni 1 bilioni. Kampuni ya Ratcliffe iitwayo Ineos iliweka rekodi ya mauzo ya Pauni 45 bilioni na imeajiri watu zaidi ya 18,500 katika nchi 22. Kwa hiyo kutoa Pauni 2 bilioni kuipata Chelsea ni kama tone la maji baharini kwa bwana huyo.

Ratcliffe aliyekulia kwenye nyumba za halmashauri kule Failsworth — mji mdogo ulio kati ya Manchester na Oldham — aliulizwa hivi karibuni juu ya elimu yake, lakini alichojibu ni ajabu; “Nilicheza tu soka, kabisa. Hicho ndicho nilikuwa napenda tu.”

Akiwa rafiki wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, Abramovich aliinunua Chelsea 2003 kwa dili la Pauni 140 milioni, akachukua na madeni yote ya klabu Pauni 80 milioni hivi na amerejesha mamilioni ya fedha klabuni badala ya kuchukua kama faida kama afanyavyo mmiliki wa Arsenal, bilionea wa Kimarekani, Stan Kroenke.

Serikali ya Uingereza inawaandama mabilionea wa Urusi, akiwamo Abramovich ambaye alikasirishwa kwa kunyimwa hata kuingia nchini kushuhudia mechi ya fainali ya Kombe la FA baina ya Chelsea na Manchester United na Chelsea walichukua kombe hilo.

Sasa hivi ameshapata uraia wa Israel. Serikali ya Uingereza imesisitiza Mrusi huyo hawezi kufanya kazi nchini kwa kutumia pasi ya Israel, japokuwa anaweza kuja kutembea tu kwa muda mfupi akitumia pasi hiyo. Dirisha la usajili litafunguliwa hivi karibuni, wachezaji wakitafutwa na kuuzwa huku ukiwapo pia uwezekano wa makocha kubadili klabu, lakini kwa Chelsea, hakika wana zaidi ya kazi, maana kuna mshindiliano wa mambo.