Cheki Ronaldo anavyojenga mwili WA kutishia mabeki!

Muktasari:

  • Lakini, usiku wa Jumatano iliyopita alionyesha namna mwili wake ulivyobadilika akiwa bonge la mtu tofauti na miaka 15 iliyopita alipokuwa Manchester United, ambako alionekana kuwa na uzito wa unyoya.

HAPO zamani Cristiano Ronaldo alikuwa mwembambaaa!

Lakini, usiku wa Jumatano iliyopita alionyesha namna mwili wake ulivyobadilika akiwa bonge la mtu tofauti na miaka 15 iliyopita alipokuwa Manchester United, ambako alionekana kuwa na uzito wa unyoya.

Usiku huo, Ronaldo aliamua kuonyesha mwili wake ulivyo kwa sasa baada ya kuvua jezi kushangilia penalti aliyofunga dakika za mwisho kabisa kuifanya Real Madrid kukamatia tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kwa kuisukuma nje Juventus kwa jumla ya mabao 4-3.

Baada ya kuona mwili huo wa Ronaldo, beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand alimwelezea Mreno huyo kuwa sasa amekuwa na mwili mwafaka wa mwanasoka anaopaswa kuwa nao.

Ronaldo alikuwa mwepesi sana alipowasili Old Trafford akitokea Sporting Lisbon kipindi hicho akiwa na miaka 18, lakini akapiga mazoezi ya nguvu wakati sasa akiwa na umri wa miaka 33 na watoto wanne, mwili wake una misuli inayomfanya aonekane kuwa mwanamichezo aliyekamilika.

Mwaka 2004 alipokuwa Man United, mwili wa Ronaldo ulikuwa hauna hata msuli mmoja unaoonekana, lakini kwa sasa mwili wake upo vizuri kinoma. Siri kubwa ni mazoezi!

Ronaldo alivua jezi pia kuonyesha misuli yake katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2015/16, lakini sasa mwili wake umejengeka zaidi, Ronaldo alisema: “Jaribu kufiti kwenye mazoezi kwa kadiri unavyoweza.”

“Unaweza kufanya mazoezi ya kutengeneza tumbo hata ukiwa chumbani kwako, unapoamka asubuhi au unapotaka kulala. Kama ukiifanya hivyo kwa mwendelezo utaona inakuwa rahisi na inageuka na kuwa tabia yako sasa.”

Kwenye chakula pia, Ronaldo anapiga mlo kamili huku akiweka msisitizo zaidi kwenye protini. Anakula samaki mara kwa mara na anapoingia kwenye migahawa kitu ambacho amependa kuagiza zaidi ni nyama steki pamoja na saladi. Anapenda pia kula chipsi, vitunguu na mayai. Matunda kwa sana na anajizuia kula vyakula vyenye sukari.

Lakini, Ronaldo anahakikisha analala mapema. Pia, ili kuamka mapema akidai usingizi unasaidia misuli kujiweka sawa na hilo ndilo jambo muhimu kwa mwanamichezo.