HISIA ZANGU: Blair anatamani soka, Kimenya anatamani mengine

Muktasari:

  • Alikuwa anautamani umaarufu wake na utajiri wake.

JINSI maisha yanavyochekesha. Niliwahi kusoma mahala jinsi ambavyo Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair alivyokuwa anatamani maisha ya staa wa zamani wa England, David Beckham.

Alikuwa anautamani umaarufu wake na utajiri wake.

Katika soka ukijipanga unapata pesa nyingi kuliko Mwanasiasa yeyote yule. Labda Mwanasiasa huyo awe ni yule wa aina ya Donald Trump. Mwanasiasa ambaye anaingia katika siasa tayari akiwa tajiri. Wanasiasa wa aina ya Tony Blair ni tofauti. Wana pato la kawaida.

Daktari mwenye hadhi ya juu wa Uingereza huwa anasubiri miaka miwili kuingiza kiasi cha pesa ambacho Wayne Rooney anaingiza ndani ya wiki moja. Ni maisha yanayoshangaza sana ambayo yanamfanya kila mwenye mtoto aliye na kipaji cha kucheza soka achangamkie fursa.

Huwa navutiwa na uchezaji wa mlinzi wa kulia wa Prisons, Salum Kimenya. Ni bonge la beki. Anajua kweli kweli. Anakaba vizuri, anapandisha timu vema. Simba na Azam zimekuwa zikimtamani kwa muda mrefu.

Kimenya hataki kuondoka Prisons kwa sababu anazofahamu mwenyewe. Lakini pia inasemekana anataka kuondoka kwa dau kubwa la shilingi milioni 30 kwa sababu anahofia akiondoka atapoteza kazi yake. Inahitaji akili ya kawaida kumuelekeza Kimenya baadhi ya vitu.

Kwa mfano, kama Kimenya ana umri mdogo au umri wa kati kama miaka 25, anaweza kutengeneza kiasi kikubwa cha pesa, mara nne ya mafao yake ya kazi ya uaskari pindi atakapostaafu. Inategemea na jinsi anavyojiamini katika kazi yake.

Leo ukimuuliza Mwinyi Kazimoto kama anajuta kuacha kazi ya jeshi na kwenda kucheza Simba kisha Uarabuni, sidhani kama anajuta. Ni wazi kwamba Mwinyi amekusanya pesa nyingi kuanzia pale mpaka leo. ni pesa ambazo asingezipata kama angeamua kubaki jeshini na kustaafu.

Inawezekana Simba inatoa ofa la chini ya shilingi 30milioni kwa Kimenya. Lakini kwa mkataba wa miaka miwili, kama Kimenya akiendelea kuwa staa anaweza kujikuta akisaini mkataba mpya kwa shilingi milioni 40 na zaidi. Inategemea na umri wake wa sasa.

Lakini kama ilivyomtokea Mwinyi, inawezekana Kimenya akafungua milango ya kwenda nje kupiga pesa zaidi. Inategemea tu na jinsi anavyoyaweka malengo yake na mpira wake.

Kumekuwa na tabia ya kudanganyana kwa wachezaji wengi nchini ambao wanacheza timu za jeshi, au wanataka kuingia timu za jeshi kwa sababu ya ajira. Sina tatizo na maamuzi binafsi ya mtu lakini kumekuwa na upotoshaji pale mchezaji mwenye kipaji anapoambiwa ‘asiache kazi kwa sababu ya mpira’. Kwani mpira sio kazi? Wachezaji ambao wanang’ang’ania ajira tofauti na soka ni wale ambao hawajiamini na uwezo wao au hawajiamini na malengo yao. Kusubiri mafao ya shilingi milioni 35 uzeeni wakati unaweza kutengeneza shilingi milioni 60 ndani ya miaka mitatu ni dalili ya uoga.

Chukulia mfano mchezaji kama Mbwana Samatta angeacha kazi ya Upolisi au Uandishi wa habari leo angekuwa na majuto yoyote kwa kitendo chake cha kuacha kazi? Hapana. Pato lake la wiki linaweza kuwa mshahara wa mwaka mzima wa Polisi.

Sio tu katika soka, kuna watu wa fani mbalimbali ambao baada ya kugundua vipaji vyao waliwekeza zaidi katika kusaka pesa kupitia katika vipaji vyao kuliko kuajiriwa. Ukikutana na akina Mpoki na Jotti leo watakwambia jinsi ambavyo leo wana pesa nyingi baada ya kukimbia kung’ang’ania ajira zao.

Kitu cha msingi kwa wachezaji wetu, hata wale ambao hawatoki katika ajira mbalimbali, ni kuhakikisha kuwa wanatumia vema pesa walizochuma katika soka kwa sababu soka ni moja kati ya ajira za muda mfupi zaidi duniani.

Kitu kingine kibaya zaidi kwa wanasoka wa sasa ni kudhani kuwa ujenzi wa nyumba ni kila kitu katika maisha yao. Wengi wakishajenga nyumba wanaridhika. Hawajui kwamba kuna maisha mengi ya kuishi mbele ya safari ambayo hayatahusisha nyumba.

Wanahitaji kuwekeza katika miradi mbalimbali endelevu kwa ajili ya kujiandaa na maisha marefu baada ya soka. Hata wanasoka wa nchi nyingine wanapambana zaidi katika masuala haya. Wengine wanapambana kurudi katika elimu kwa sababu kuna maisha marefu baada ya soka.