Babu Seya karudi, Wenger yuleyule

Muktasari:

Babu Seya na mwanaye Papii wanarejea uraiani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004. Wakati vitu vingi vikiwa vimebadilika, kocha wa Arsenal bado ni Arsene Wenger. 

HAKUNA marefu yasiyo na ncha, ni maneno ya Wahenga. Mungu awarehemu popote walipo. Siku hizi hakuna Wahenga tena.

Usemi wao umetimia kwa nguli wawili wa muziki nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Papii Kocha. Kwa kauli moja tu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, wametoka jela. Kiti cha urais kina nguvu, asikwambie mtu.

Nyota hao walifungwa miaka 13 iliyopita, enzi hizo Rais wa Tanzania alikuwa Benjamin Mkapa. Kilo ya Sukari ilikuwa Sh250. Mambo mengi yamebadilika na mapya kutokea wakati ambao, wakali hao wa muziki wa dansi walikuwa jela.

Asikwambie mtu, jela siyo sehemu nzuri kwenda, labda itokee bahati mbaya tu. Hakuna maisha magumu kama ya kuishi ndani ya kuta ndefu zilizozungushwa kila upande, ni dunia nyingine.

Babu Seya na mwanaye Papii wanarejea uraiani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004. Wakati vitu vingi vikiwa vimebadilika, kocha wa Arsenal bado ni Arsene Wenger. Taji lake kubwa la mwisho alishinda wakati Babu Seya na Papii wakiwa bado uraiani.

Pamoja mashabiki kubeba mabango ya kuashiria kwamba hawamtaki Mfaransa huyo, bado ameendelea kusalia klabuni hapo, hadi Babu Seya amemkuta tena. Inashangaza sana.

Umewahi kujiuliza ni mambo gani yametokea kwenye michezo tangu Babu Seya alipokwenda gerezani mpaka sasa anarejea tena uraiani ambako vyuma vimekaza kwelikweli? Tutazame machache.

TFF MARAIS WATATU

Tangu Babu Seya alipohukumiwa mpaka sasa, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limekuwa chini ya marais watatu. Wakati nguli huyo anafungwa, Leodeger Tenga ndiyo kwanza alikuwa anaingia TFF.

Tenga akaiongoza TFF kwa miaka tisa na kupata mafanikio kiasi ikiwamo Taifa Stars kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwaka 2009. Tenga akaisuka TFF kuwa taasisi imara, wakati bado nguli huyo na mwanaye wakiwa jela.

Jamal Malinzi naye akashinda urais wa TFF mwaka 2013, akaupeleka mpira wetu hapa ulipo sasa. Akaibadili TFF alivyojisikia. Timu ya Taifa ikapoteza mvuto hadi kufikia hatua ya basi la wachezaji kupigwa mawe na mashabiki. Malinzi naye yupo gerezani akituhumiwa kwa kesi ya utakatishaji fedha, Mungu amsaidie huko.

TFF sasa imetua kwenye mikono ya Wallace Karia, ambaye ameanza kujipambanua na kuirejesha kwenye mstari tena. Ndiyo kwanza ana siku 100, lakini kasi yake inavutia, huenda akafanya makubwa. Maisha yamekwenda kasi.

AZAM YAANZISHWA, YABEBA NDOO

Wakati Babu Seya na Papii wanakwenda gerezani, familia ya Said Salim Bakhresa haikuwa na mpango wa kuanzisha timu ya soka. Miaka mitatu baadaye wazo likaja. Azam FC ikaanzishwa na msimu wa 2008/09 ikaanza kushiriki Ligi Kuu.

Azam ikajenga uwanja wake na kuweka kila kitu kinachostahili kuwepo kwenye timu ya soka. Azam ikaanza kupambana na Simba na Yanga ndani ya Ligi Kuu Bara. Miaka mitatu baadaye ikamaliza nafasi ya pili. Azam inayotajwa kuwa timu tajiri zaidi nchini, ikabeba taji la Ligi Kuu Bara mwaka 2014. Ikabeba tena taji la Kagame mwaka 2015, tena kwa rekodi ya kutoruhusu goli. Ikatwaa pia mataji matatu ya Kombe la Mapinduzi.

Azam ikawa timu inayotumia fedha nyingi zaidi Ligi Kuu, ikatikisa na sasa imeanza kubana matumizi na ndiyo wawili hao wametoka gerezani. Siku zimekwenda kwa kasi sana.

SIMBA UWEKEZAJI MPYA

Kwa bahati nzuri, hili la Simba, Babu Seya na mwanaye wamelikuta la moto kabisa. Ni mabadiliko ndani ya klabu ya Simba ambayo tayari imethibitisha mwekezaji mkubwa atakuwa Mohammed Dewji ‘MO’ na timu hiyo itaendeshwa kwa mfumo wa hisa.

Wakati wawili hao wanawekwa ndani, Simba ilikuwa timu masikini tu Ligi Kuu. Ilitegemea michango ya wanachama ili kujiendesha. Ilitegemea pia fedha kidogo za wadhamini.

Vigogo wanne; marehemu Juma Salum, Hassan Dalali, Ismail Rage na Evans Aveva wamekuwa marais wa timu hiyo lakini hakuna kilichobadilika. Hadi Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ nao wamepelekwa gerezani, Babu Seya na mwanaye bado walikuwa huko.

MANJI AIBUKA, ATIKISA

Wakati Babu Seya na Papii wanafungwa, bilionea Yusuf Manji hakuwa mtu anayefahamika sana, lakini alikuwa na hela zake nyingi tu.

Miaka miwili baadaye Manji aliingia Yanga kama mfadhili. Akaanza kuwajaza minoti. Akalipia viingilio ili mashabiki wafurike uwanjani kwenda kuishangilia timu yao. Manji akawa tishio. Yanga yote ikamtazama.

Manji akapanda akawa Mwenyekiti wa klabu hiyo mwaka 2012 kabla ya kujiuzulu mwezi Mei mwaka huu. Katika kipindi cha miaka 11 ndani ya Yanga, Manji aliisaidia timu hiyo kutwaa mataji saba ya Ligi Kuu na kufika hatua ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Manji akapata kesi akawekwa ndani, ikafutwa na akatoka lakini bado Babu Seya na Papii walikuwa huko. Maisha yamekwenda kasi sana.

SIMBA, YANGA MAKOCHA KIBAO

Miaka 13 ya Babu Seya na Papii gerezani, imeshuhudia timu za Simba na Yanga zikibadili makocha kama nguo, wengine hadi wamesahaulika.

Katika kipindi hicho Simba imefundishwa na James Siang’a (Kenya, marehemu sasa), Patrick Phiri (Zambia), Twalib Hilal (Oman), Mosses Basena (Uganda), Milovan Cirkovic (Serbia), Amri Said na Selemani Matola (Tanzania).

Wengine ni Mfaransa Patrick Liewig, mzawa Abdallah Kibadeni, Zdravko Logarusic (Croatia), Patrick Phiri tena, Goran Kopunovic (Serbia), Dylan Kerr (England), Jackson Mayanja (Uganda) na sasa ina Mkameruni Joseph Omog, ambaye wanamtafutia sababu ya kumtimua tu.

Yanga imefundishwa na Jackson Chamangwana (Malawi), Milutin Sredjovic ‘Micho’ (Seribia), Dusan Kondic (Seribia), Kostadin Papic (Serbia), Tom Saintfiet (Ubelgiji), Erne Brandts (Uholanzi) na Hans Van Pluijm wa Uholanzi pia.

Wengine ni Mbrazili Marcio Maximo, Pluijm tena na sasa George Lwandamina ambaye mtihani wake mkubwa ni kuhakikisha Wana Jangwani hao wanafanya vizuri kimataifa.

SOKA LA TANZANIA

Pamoja na mabadiliko yote, soka la Tanzania bado lipo chini. Tangu Babu Seya amefungwa mpaka anaachiwa huru, soka la Tanzania limeendelea kuwa chini. Tunakosea wapi?

Kwenye viwango vya Fifa ndiyo aibu kabisa. Timu ya Taifa inafungwa kama mlango. Kilimanjaro Stars nayo imekuwa magumashi tu, na kocha wake Ammy Ninje anaongea viingereza vingi visivyo na tija uwanjani. Balaa tupu aisee!

Bado ipo haja ya kufanya mapitio ya wapi soka la Tanzania limekwama. Licha ya kwamba Serengeti Boys ilishiriki michuano ya Afrika kwa vijana. Licha ya kwamba Stars ilifuzu CHAN mara moja, bado soka la Tanzania lipo chini.

Babu Seya na Papii karibuni tena duniani. Tanzania ya sasa ni ya viwanda. Karibuni tuijenge nchi. Soka letu ndiyo kama mtakavyosikia.