Ambokile: Staa wa Mbeya City anayewatega vigogo

Muktasari:

Tangu kufunguliwa kwa dirisha dogo kuna baadhi ya majina ya wachezaji ambayo yanahusishwa kusajiliwa na klabu za Simba na Yanga. Nyota hao ni pamoja na Mohammed Rashid wa Tanzania Prison, Mohammed Ibrahim wa Simba, Eliud Ambokile Mbeya City na wengine wengi.

DIRISHA dogo la usajili limefunguliwa na kila timu ina nafasi ya kuboresha kikosi chake kwa kuongeza baadhi ya majembe katika sehemu ambazo zina mapungufu, pia zina nafasi ya kuwaacha wachezaji ambao wameshindwa kufanya vizuri.

Tangu kufunguliwa kwa dirisha dogo kuna baadhi ya majina ya wachezaji ambayo yanahusishwa kusajiliwa na klabu za Simba na Yanga. Nyota hao ni pamoja na Mohammed Rashid wa Tanzania Prison, Mohammed Ibrahim wa Simba, Eliud Ambokile Mbeya City na wengine wengi.

Ambokile ndiye staa wa Mbeya City msimu huu akiwa ameifungia timu hiyo mabao manne mpaka sasa huku akicheza kwa kiwango cha juu kwenye kila mchezo.

Mwanaspoti limemtafuta na kupiga naye stori mbili tatu ili kufahamu namna alivyojiimarisha na kuwa staa msimu huu.

SIYO WA MCHEZO

Kila mchezaji huwa na malengo yake kabla ya kuanza kwa msimu ili kuona anafika mbali. Yeye anasema kabla ya kuanza kwa msimu huu alitamani kuwa miongoni mwa wachezaji watakaofanya vizuri na anafurahi hilo limetimia.

“Kilichonifanya niwe hapa nilipo sasa ni kujituma na kusikiliza kila ambalo kocha anataka nilifanye nikiwa kwenye mechi na hata mazoezini, bila ya kusahau nidhamu ya kile ambacho naambiwa nifanye,” anasema nyota huyo mwenye uwezo mkubwa wa kukokota mpira na kupiga mashuti.

“Ni msimu wangu wa pili, kwa hiyo nina uzoefu ingawa si mkubwa wa kwakiasi hicho lakini umechangia kucheza kwa kujiamini na kuonyesha uwezo wangu halisi. Licha ya kwamba mnaona nafanya vizuri lakini kwangu bado sijafikia pale ninapotamani kufika,” anasema.

POPOTE FRESHI

Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Nsanzurwino amekuwa akimpanga kama winga wa kushoto au kulia lakini licha ya kumpanga huko ameweza kufunga magoli manne na kuwa nyota wa timu hiyo aliyefunga zaidi.

Anasema mchezaji anatakiwa awe na uwezo wa kucheza katika nafasi yoyote kwani kila kocha huwa na mtazamo wake kwa hiyo kama anakupanga sehemu unashindwa kucheza utakuwa anakaa benchi tu.

“Kocha ndio anaona zaidi kuwa akinipanga kama mshambuliaji wa kati au kama winga nitafanya vizuri. Kwangu naona sawa kucheza popote na kufunga kunatokea tu ukiwa katika eneo sahihi ambalo unatakiwa kutulia. Mfano Saimon Msuva alikuwa mfungaji bora akitokea pembeni,” anasema.

Wakati ligi inaanza mwezi Agosti ilikuwa si rahisi kufikiria kuwa Ambokile angekuwa moja ya wachezaji nyota msimu huu kwani jina lake lilikuwa geni zaidi miongoni mwa wacheza soka nchini lakini kwa sasa anafahamika kila kona.

“Siri ya kufahamika nafikiri ni baada ya kucheza vizuri tena kwa kujituma na kuweza kufunga hayo magoli manne ambayo baadhi ya wachezaji wa gharama hawajaweza kufanya kama nilivyofanya mimi,” anasema.

“Hata kama nikishindwa kufunga nimekuwa mchezaji wa kujituma zaidi na kujitolea ili kuisaidia timu yangu kupata matokeo jambo ambalo linaendelea kuniweka katika kikosi cha kwanza,” anasema Ambokile.

RAPHAEL, KENNY PENGO

Ambokile anasema moja ya sababu za timu yao kushindwa kusimama imara msimu huu ni kukosekana kwa viungo wao mahiri Raphael Daud aliyejiunga na Yanga na Kenny Ally aliyejiunga na Singida United.

“Walikuwa muhimili mkubwa katika kikosi chetu na walihusika katika kuisaidia timu yetu kufanya vizuri msimu uliopita,” anasema.

“Kama tungekuwa na Raphael na Kenny tungeweza kufanya vizuri zaidi msimu huu hasa ukichanganya na nguvu ya wachezaji wapya ambao wamesajiliwa. Uwepo wao ungeweza kunibeba hata mimi nifunge zaidi,” anaeleza.

AMKUBALI MO IBRAHIM

Ambokile anasema kila mchezaji anapocheza kuna baadhi ya wachezaji ambao anavutiwa kuwaona wakicheza pengine kwa viwango vyao na uwezo wao wa kufunga, kukokota mpira, kuchezea mpira na vingine vingi.

“Navutiwa mno na kiungo wa Simba Mohammed Ibrahim ‘MO’ ambaye naamini ni moja ya viungo bora tuliokuwa nao hapa nchini kwani ana kila kitu ambacho kiungo yoyote anatakiwa kuwa nacho,” anasema.

“Ukiachana na ‘MO’ siwezi kuacha kuwataja tena Raphael na Kenny kwani hawa jamaa wanacheza kama pacha na wana kila sababu ya kuwa viungo bora nchini,” anasema.

ALIPOTOKEA

Ambokile alianza elimu ya msingi katika shule ya Madugugu mwaka 2002-08, alijiunga na Sekondari ya Mwakipesile mwaka 2009-12, kabla ya kuchaguliwa na Shule ya Ivumwe ambayo alihitimu elimu yake ya kidato cha sita mwaka jana.

“Nikiwa nasoma mwaka 2013, nilikuwa nacheza mpira katika timu ya Luenda Fc, ambayo ilikuwa Ligi Daraja la Pili hapo ndio mara ya kwanza viongozi wa Mbeya City waliponiona na kuonyesha nia ya kunihitaji,” anasema.

“Nilipomaliza elimu yangu ya kidato cha sita viongozi wa Mbeya City walinifuata ili nikafanye majaribio katika timu yao na walinikubali na kunisajili katika timu yao ya vijana ambayo sikucheza hata nusu msimu wakanipandisha,” anasema.