HAWAWEZI: Kwa Salamba, Kaheza tutakuwa watalii wa kale

USAJILI wa timu za Ligi Kuu unaendelea kwa kasi ya ajabu. Mbali na kuripoti habari hizo, nimekaa pembeni pia nikifanya tathmini. Natazama zaidi uwezo wa wachezaji wanaohama kutoka timu ndogo kwenda kubwa. Natazama kwa makini kwelikweli.

Haijawahi kutokea Tanzania ikawa na uhaba wa wachezaji wazuri kama kipindi hiki. Baada ya usajili wa wachezaji sita ama saba tu, wachezaji wote wazuri walikuwa wamemalizika kwenye ligi, hasa wa eneo la ushambuliaji.

Wachezaji wazawa wa viwango vya juu wamekuwa wachache mno. Wengi wana viwango vya kawaida na wengine ndio kwanza hawajitumi kabisa. Inashangaza sana.

Baada ya usajili wa wachezaji hao wachache wazuri kutoka hapa ndani, timu sasa zitalazimika kusaka wachezaji wachache kutoka nje ya nchi. Idadi inayoruhusiwa ni wachezaji saba tu.

Wanasema imewekwa sheria ya kuwalinda wachezaji wazawa. Imewekwa sheria ya kuzuia wachezaji wengi wa kigeni kuja nchini ili kupata wazawa wengi watakaoibeba Taifa Stars. Ni ajabu na kweli.

Hivi ni kweli wachezaji wa kigeni ndio wanazuia Taifa Stars isifanye vizuri? Hapana. Wachezaji wa kigeni hawajawahi na hawatawahi kuwa tatizo kwa Taifa Stars. Tatizo ni sisi wenyewe.

Hatuna wachezaji imara wa ndani wanaoweza kupambania Taifa Stars. Kama mchezaji anaogopa kushindana na wageni ili apate nafasi ya kucheza kwenye timu yake, ndio ataweza kuisaidia Taifa Stars iifunge Algeria? Hapana. Haitakaa iwe hivyo.

Nimeona Simba inajiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani. Inafanya kile inachoita ‘usajili wa nguvu’. Ndiyo huu usajili wa kina Adam Salamba, Marcel Kaheza na wengineo. Sijui ila inachekesha sana.

Hatuwezi na hatutaweza kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa kwa kuwategemea kina Salamba. Ni wachezaji wazuri kweli, ila kwa ligi yetu. Kwenye Ligi ya Mabingwa hawawezi kuwa na jipya sana.

Niliwatazama kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup pale Kenya. Kulikuwa na tofauti kubwa sana kati ya wachezaji wa Kenya na Tanzania.

Wachezaji wengi wa Tanzania ni laini. Wachezaji wengi wa Tanzania ni wa kawaida kwa sasa, huwezi kuwafananisha na wa Kenya wala Uganda.

Uliitazama ile Gor Mahia? Ina wachezaji watano tu wa kigeni. Wachezaji wengine wote ni wazawa. Wachezaji wazawa wa Kenya wako fiti. Huwezi kuwafananisha na hawa kina Kaheza na Mohammed Rashid.

Wachezaji wa Kenya wana viwango vya juu, tofauti kabisa na wa Tanzania. Sasa pale Uganda wachezaji wa KCCA ndiyo habari nyingine kabisa. Timu yao inafanya vizuri kimataifa sasa lakini kwa kutegemea wachezaji wazawa tu.

Kwanini wanaweza? Wachezaji wao wazawa wako fiti. Wachezaji wazawa wa Uganda wana vipaji vikubwa na wanavifanyia kazi. Ni kama unavyowaona kina Shafiq Batambuze wa Singida United na Emmanuel Okwi wa Simba. Kwa Tanzania bado tuna safari ndefu. Straika mzawa anafunga mabao manane ama zaidi kwenye Ligi Kuu Bara halafu anashindwa kufunga bao lolote dhidi ya timu za Kenya katika mechi tatu mfululizo.

Washambuliaji wa Tanzania walipocheza na mabeki wa Kenya walionekana kuwa kawaida sana. Labda kama angekuwepo John Bocco. Wengine sasa wako kawaida sana.

Kama kweli tuna nia ya dhati ya klabu zetu kufanya vizuri kimataifa, ni vyema tukaongeza idadi ya wachezaji wa kigeni hadi kufikia 10. Hii itazisaidia timu zetu. Hakuna namna nyingine.

Kumbukumbu zangu zinaonyesha kuwa Taifa Stars ilifuzu mashindano ya CHAN mwaka 2008 wakati ambapo Ligi Kuu ilikuwa ikiruhusu wachezaji 10 wa kigeni. Baada ya hapo wakaanza kupunguzwa na timu ya taifa ikawa ovyo zaidi. Yaani ovyo kwelikweli

Tuwaache wachezaji wetu wapambanie nafasi na wale wa kigeni. Tusikubali wachezaji wetu wawe legelege tu kisa tunawalinda kwa ajili ya timu ya taifa. Kwa mwendo huu tutakuwa hapa hapa na hatutafika popote kisoka.

Nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inafanya vizuri kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika na CHAN licha ya kwamba, ligi yao inaruhusu wachezaji zaidi ya 11 wa kigeni.

Kwanini wanafanikiwa? Ni kwasababu rahisi tu. Wachezaji wao wengi wanakwenda kucheza nje ya nchi. Wachezaji wa ligi ya ndani nao wanapambana kuweza kucheza kutokana na ushindani mkubwa wa wageni.

Mchezaji mahiri anapaswa kushindana mchana na usiku. Huyu Ibrahim Ajibu huenda angekuwa mahiri zaidi kama pale Yanga kungekuwa na mastraika wanne wa maana. Angepambania nafasi yake. Angeacha maringo.

Wachezaji wetu wazuri hawajitumi kwa kuwa tu wana uhakika wa nafasi kwenye timu zao. Akiwatazama wachezaji wenzake wa Kitanzania wako hivyo hivyo. Kwanini ahangaike?

Tunaweza kuongeza hamasa kubwa ya ligi yetu kama tutakuwa na orodha kubwa zaidi ya wachezaji wa kigeni. Tutaongeza hamasa kubwa ya wachezaji wa ndani kama tutaruhusu wageni wengi waje kucheza.

Habari njema ziadi ni kwamba kwa sasa wachezaji wengi wa Taifa Stars pia watakuwa wakitokea nje. Wamefika sita sasa baada ya Himid Mao naye kwenda Mirsi.

Kwa wachezaji saba wa kigeni, naiona Simba ikienda kutalii kwenye michuano ya Afrika na kurejea. Hatuwezi kufika popote na wachezaji hawa wazawa, labda wabadilike sana.