VIWANGO: Waamuzi hawa achana nao kabisa

NI kweli Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018 imeanza kusahaulika tangu ilipofikia tamati mwishoni mwa mwezi uliopita kwa Simba kubeba taji ililolisotea kwa muda mrefu.

Hata hivyo, asikuambie mtu, kuna waamuzi waliofunika katika ligi hiyo kiasi kwamba haikuwa ajabu kubaki midomoni mwa mashabiki wa soka kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Kwa sasa mashabiki wanasubiri kwa hamu kujua nani na nani watakaobeba tuzo mbalimbali za msimu uliopita, kuanzia kwa klabu yenye nidhamu, Mchezaji Bora, Kipa Bora na Mwamuzi Bora.

Mwanaspoti ambalo limekuwa likifuatilia soka la Tanzania kwa muda mrefu hususan Ligi Kuu Bara, linakuletea orodha ya waamuzi watano waliofanya makubwa msimu uliopita kwa kuchezesha kwa kiwango cha juu na kuwa gumzo kwa mashabiki wa soka.

EMMANUEL MWANDEMBWA

Ni mwamuzi ambaye huwa haendeshwi na kelele za mashabiki na mara nyingi huonesha ukomavu wa kutokuyalea matatizo ya kinidhamu muda wote anapukuwa uwanjani.

Mwandembwa ni mwamuzi mwenye beji ya FIFA, aliyopewa Novemba 2017 na baada ya hapo alichaguliwa kwenda kuchezesha michuano ya vijana Cecafa 2018 iliyochezwa Burundi na Serengeti Boys kubeba ndoo ikiwazidi ujanja vijana wenzao wa U17.

Baada ya kuonekana anafanya vizuri katika michuano hiyo na hata katika mechi za ligi alizokuwa akichezesha, aliaminiwa na kupewa pambano la marudiano la watani wa jadi, Simba na Yanga na kulitendea haki kwa kulichezesha kwa ufasaha.

Kuonyesha kuwa msimu uliopita ulikuwa wa Mwandembwa mwamuzi huyo alipewa pambano la fainali ya Kombe la FA lililoshuhudiwa Mtibwa Sugar ikiwazidi ujanja Singida United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Katika waamuzi wenye viwango wanaofanya vema kwa sasa miongoni mwa waamuzi wa Ligi Kuu, Mwandembwa amefunika na kadri akikomalia ufanisi si ajabu kuja kuona akipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

FRANK KOMBA

Huyu ni mwamuzi wa pembeni na mara nyingi huwa ni msaidizi namba moja wa refa ambaye anacheza mchezo wowote ambao atakuwepo.

Komba naye anamiliki beji ya FIFA na amekuwa akiitumia vizuri fani yake kwa kutoa maamuzi sahihi muda mwingi, japo kuna wakati huchemka kwani hakuna aliyekamilika.

Msimu huu Komba alikuwa katika mechi mbili kubwa ile ya Yanga dhidi ya Azam ya duru la pili lililoisha kwa Jangwani kulala mabao 3-1 na ile ya mabingwa Simba na Yanga nayo mzunguko wa pili akimsaidia Mwandembwa.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilichamgua Komba kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha fainali za Afrika za Vijana U17 zilizochezwa mwaka jana kule Gabon.

Komba ni miongoni mwa waamuzi wasomi akiwa na taaluma ya sheria na ni wakili wa kujitegemea.

ELLY SASII

Hakuna mwamuzi anayewakuna mashabiki kama Elly Sasii ambaye alichaguliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuchezesha mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho na hata mechi nyingi za timu ya taifa alichezesha kama Tanzania dhidi ya Botswana.

Sasii ni miongoni mwa waamuzi vijana ana beji ya FIFA iliyopelekea kuaminiwa na kuchezesha mechi nyingi za kimataifa kuanzia ngazi ya klabu hata timu za taifa.

Katika mechi ya Simba dhidi ya Yanga mzunguko wa kwanza iliyomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 msimu huu, Sasii ndiye aliyekuwa kati akiwahukumu nyota 22 wa timu hizo na a alichezesha vizuri licha ya kuwa na mapungufu ya hapa na pale.

Sasii ni miongoni mwa waamuzi wanaotumia mno busara uwanjani sambamba na kuzingatia sheria na kuwakuna mashabiki wa timu wanazozichezesha.

SOUD LILA

Alipata beji ya FIFA mwaka 2014 naye ni mwamuzi wa pembeni na amekuwa akifanya vizuri kama maamuzi yake kiasi cha kumfanya awe anachaguliwa mara kadhaa kuchezesha baadhi ya mechi za kimataifa katika ngazi ya klabu hata timu za taifa.

Lila alikutwa kashfa isiyo na mashiko ya upangaji matokeo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya LLB Academic ya Burundi dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda kwa mechi iliyomalizika Rayon kushinda kwa 1-0 ugenini.

Mbali na shtuma hiyo Lila amekuwa akiendelea kufanya kazi yake kwa umakini na msimamo na kupewa kazi ya kuwa mwamuzi msaidizi katika mechi ya Simba dhidi ya Yanga na kwa hali ilivyo inaonekana kuwa anaweza kupona katika shutma hiyo.

Lila anaingia katika orodha ya waamuzi wenye viwango katika Ligi Kuu Bara kwani kila mechi ambayo huchezesha huwa anafanya kazi yake ipasavyo.

JONESIA RUKYAA

Unaweza kumwita ni mwanamke wa shoka. Ni miongoni mwa waamuzi wa chache nchini wa kike waliokuwa na misimamo katika maamuzi yao na anamiliki beji ya FIFA pia.

Rukyaa amezidi kujipambanua kimataifa baada ya kupewa fursa ya kuchezesha fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizofanyika Cameroon na alifanya kazi hiyo kwa uadilifu wa kiwango cha juu.

Mechi yake ya kwanza kubwa kuchezesha tangu alipoanza fani hiyo ilikuwa ni ya Mtani Jembe ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa iliyopigwa Disemba 13, 2014.

Yanga ilifungwa mabao 2-0 na baada ya hapo akachezesha mechi ya mzunguko wa pili Simba na Yanga 2015.

Rukyaa aliteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), kuchezesha fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake zitakazofanyika Ureno.

Mbali na kukutana na heka heka hasa kwa kadi yake nyekundu ya Abdi Banda alipokuwa Simba dhidi ya Yanga na sakata la kati tatu za Mohammed Fakhi katika mchezo wa msimu uliopita kati ya Kagera Sugar na Simba lakini amezidi kukomaa na kuimalika zaidi ya hapo awali. Rukyaa amekuwa akichezesha mechi za kimataifa katika ngazi ya klabu na timu za taifa na amekuwa akichanya vizuri jambo ambalo linamfanya kuingia katika orodha ya waamuzi Bongo wanaofanya vizuri.