Lingard mchezaji mwenye uzito wa mbu huko Russia

HUKO Russia kwenye Fainali za Kombe la Dunia kutakuwa na wanasoka 736 watakaopigana vikumbo kuunasa ubingwa huo wa dunia.

Lakini, wachezaji hao kila mmoja ana sifa yake na hakika hicho ndicho kitu kinachowavutia zaidi mashabiki kutaka kufahamu kuna mastaa wa aina gani watakaokuwapo kwenye mikikimikiki hiyo.

Nchi zinazoshiriki ni 32 na kila moja imejumuisha wachezaji 23 kwenye kikosi chake, lakini sasa unamfahamu mchezaji mfupi kuliko wote, mchezaji mwenye kilo nyingi, au mchezaji mwenye uzito wa unyoya au yule mdogo zaidi na mkubwa zaidi?

Mchezaji mwenye kilo nyingi

Staa wa Panama, Roman Torres, ndiye mchezaji mwenye kilo nyingi zaidi kati ya wale wote waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Staa huyo ana uzito wa kilogramu 99. Torres ni beki, hivyo kwa washambuliaji wenye kilo za kuku wajipange kabisa kwenda kukutaka na mtu mzito. Bao lake dhidi ya Costa Rica ndilo lililoipa Panama tiketi ya Kombe la Dunia huko Russia.

Wachezaji wanaofuatia kwa kuwa na kilo nyingi ni Almuaiouf Abdullah (Saudi Arabia), Jannick Vestegaard (Denmark), Harry Maguire (England) wenye kilogramu 98 kila mmoja, wakati Shinwook Kim (Korea Kusini) ana kilogramu 97.

Mchezaji mwenye kilo chache

Japan hakika ndiyo timu yenye wachezaji wengi wenye uzito mdogo na hapo, kiungo wao wa ushambuliaji, Takashi Inui, ndiye mchezaji mwepesi zaidi kwenye fainali hizo za Russia, akiwa na kilogramu 59 tu. Amejiunga hivi karibuni huko Real Betis akitokea Eibar na ameichezea timu yake ya taifa mara 21. Wachezaji wenyine wenye uzito wa unyoya kwenye fainali hizo ni Jesse Lingard (England) kilo 60, Joao Moutinho (Ureno), Al-Breik Mohammed (Saudi Arabia), Nahitan Nandez, Lucas Torreria (Uruguay) na Dries Mertens (Ubelgiji) ambao kila mmoja ana kilogramu 61.

Mchezaji mrefu zaidi

Mchezaji mrefu kuliko wote kwenye fainali hizo za Russia ni kipa wa Croatia, Lovre Kalinic, ambaye akisimama amekwenda hewani futi 6 na nchi 5 sawa na sentimita 201. Anafuatiwa na Vestegaard, ambaye kilogramu zake 98 zimekaa kwenye urefu wa sentimita 200, sentimita moja tu pungufu. Wachezaji wengine wanaoongoza kwa urefu, ambao kimsingi wote ni makipa ni pamoja na Federico Fazio (Argentina) na Thibaut Courtois (Ubelgiji) ambao kila mmoja ana kilo cha sentimita 199.

Mchezaji mfupi zaidi

Kuna wachezaji watatu wafupi zaidi waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia mwaka huu. Wachezaji hao ni kiungo wa Panama, Alberto Quintero, staa wa Saudi Arabia Al Sherhi Yahya na mkali wa Uswisi, Xherdan Shaqiri, ambao hao wote wanaposimama kilo chao ni sentimita 165 sawa na fupi 5 inchi 4. Wachezaji wengine wanaoongoza kwa ufupi ni winga wa Mexico, Javier Aquino mweye sentimita 166, wakati mchezaji mwenzake Andres Guardado anakimo cha sentimita 167.

mwenye Umri mkubwa

Misri ndiyo timu yenye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi, ambaye ni kipa wao Essam El Hadary ambaye amekwenda kwenye fainali hizo akiwa na umri wa miaka 45 na miezi 4. Wachezaji wengine wenye umri mkubwa ni Rafael Marquez (Mexico) miaka 39, miezi 3 na Sergy Ignashavic (Russia) miaka 38, miezi 10. Ukweli El Hadary atakwenda kuweka rekodi kali kabisa ya kucheza fainali za Kombe la Dunia akiwa na umri mkubwa kama atafanikiwa kupangwa kwenye mechi yoyote kati ya zile itakazocheza timu yake ya Misri.

Mchezaji mdogo zaidi

Akiwa na umri wa miaka 19, kiungo wa Australia Daniel Arzani ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi atakayekuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Wachezaji wengine wenye umri mdogo ni Kylian Mbappe, ambaye naye ana miaka 19 na miezi 5 kama alivyo Arzani, tofauti yao ni kwamba Mbappe ni mkubwa kwa siku tano. Mchezaji mwingine mdogo ni kipa wa Nigeria, Francis Uzoho, mwenye umri wa miaka 19 na miezi 7.