Kichuya mjanja kinoma, afuata nyayo za Msuva

GHAFLA alama za nyakati zimerudi nyuma, gia ya kwenda mbele inakosekana inayopatikana ni ile ya kurudi nyuma, hiki ndicho unachoweza kusema katika kisa cha usajili wa winga Mrisho Ngassa ambaye anakaribia kusaini kukipiga na Yanga.

Yanga inamrudisha Ngassa ili kuwaongezea nguvu katika kikosi chao baada ya kuona ana kitu cha kutaka kukiongeza katika kikosi chao hasa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho.

Sitaki kuwalaumu sana waliofikiria hili kwa kuwa naona wana sababu za msingi kufikiria akili hiyo ya kurudi nyuma lakini pia hebu tuangalie kipi kimesababisha la wao kufikia hapo?

Ngassa ameonyesha kitu tofauti katika kipindi ambacho amekuwa na Ndanda, tatizo ambalo naliona ni kushindwa kwa vijana kuthibitisha ubora wao mbele ya Ngassa.

Kikosi cha Yanga kina jumla ya mawinga watano ambao naweza kuwagawanya katika makundi mawili tofauti tukianza na kushoto ambako kuna Geofrey Mwashiuya, Emmanuel Martin na kulia kuna Yusuf Mhilu,Juma Mahadhi na Baruani Akilimali.

Siwatetei viongozi wanaofikiria hivyo kwa kuwa hata wao walitakiwa kuielekeza mbali zaidi akili zao katika kutafuta kitu kipya zaidi kitakachokuwa na tija kuliko kile kitakacholetwa na Ngasa katika timu yao.

Usajili wa Ngassa unakuja kutokana na vijana hawa watano kushindwa kuthibitisha uwezo wa ujana wao kwa kutotumia nafasi ya kukosekana kwa wakongwe katika nafasi zao na kuwalazimu watu kuanza kufikiria kwa kurudi nyuma.

Hakuna anayekataa kwamba vijana hawa watano wana vipaji lakini tatizo wameshindwa kutumia nafasi ya kucheza soka la ushindani na kujihakikishia nafasi katika kikosi chao.

Mahadhi na wenzake wamekuwa na soka la kupanda na kushuka kwa mechi hii kucheza vizuri lakini mechi ijayo wakakupandisha presha kwa kiwango kibovu mkiasi cha kuweza kukukera kuwatazama.

Vuta picha ya Mahadhi aliyeanza kwa nafasi adimu katika mchezo mgumu dhidi ya TP Mazembe alifanya kitu tofauti kiasi cha kuwakosha watu na kuona endapo angeongeza kasi ile katika mechi 10 mfululizo sidhani kama leo angekuwa na hesabu za kucheza soka ndani ya nchi yetu.

Badala yake akasifiwa na kuhamisha maisha yake katika mitandao ya kijamii akiwa mzuri wa kubadilisha mavazi na staili za nywele, hakuwa tena Mahadhi mzuri wa uwanjani ghafla akapoteza imani kwa waliokuwa wanamumini.

Hali hiyo ikatokea tena kwa Mwashiuya alifanya vizuri katika mechi tatu za mkataba wake ulivyoanza Yanga, viongozi wake wakavutiwa wakamuongezea hata fedha kidogo naye akapita katika njia hiyo hakuongeza juhudi uwanjani akaamua kuoa na maisha mengine yakaendelea.

Vijana hawa ambao tulitarajia wangekuwa ni kizazi cha soka la kisasa wakakutana tena na Ngassa. Ilikuwa wamnyime kabisa nafasi Ngassa asifikiriwe kuja Yanga lakini katika mchezo baina ya timu yao na Ndanda ya ‘Anko Ngassa’ ajabu zaidi akaonekana staa mzuri kuliko wao.

Jibu fupi tunalolipata hapa ni kwamba vijana wamekuwa na viwango kama homa za vipindi kwa kushindwa kutumia nafasi ya kujituma na kupandisha viwango vyao kujihakikishia nafasi klabu haiwezi kuendelea kuwasubiria wao eti mpaka akili yao itakapoamua kucheza mpira.

Yanga ni kama mzee aliyeachana na mke wake na kupata mke mpya, lakini mke mpya anashindwa kujitunza na kuthibitisha ubora wake kisha akawa mkali kwa kumuona mumewe anamuangalia barabarani mke wa zamani tena kwa matamanio ya kurudiana naye.

Mahadhi na wenzake wanapaswa kutambua muda hauwasubiri wao wanachotakiwa ni kuheshimu alama za nyakati ni ajabu mchezaji anapata nafasi ya kupendwa na kocha wake kisha akampa nafasi ya kucheza uwanjani kisha anapoteza nafasi na kuanza kulaumu.

Kocha wa sasa Yanga, Mwinyi Zahera ameshaweka bayana kwamba anawakubali Mwashiuya, Mahadhi na Akilimali akitaka apewe muda wa kuwabadilisha lakini Zahera pekee hawezi kufanikiwa katika hili ikiwa wao wenyewe hawatakuwa na akili ya kutaka mafanikio zaidi. Naona dalili ya mbali kama itakuja hata Zahera atachoka na kuhitaji kitu kipya tofauti na wao kwa kuwa sasa hawajui kwa undani kama ilivyokuwa kwa viongozi wa klabu yake ambao sasa wanatamani kumrudisha Ngassa aje awaokoe wakichoshwa na subiri ya kina Mahadhi.

Rafiki yangu mmoja alijaribu kuwatetea akisema Mahadhi asingeweza kuonyesha uwezo mkubwa mbele ya Simon Msuva na sasa ni wakati wake kuonyesha uwezo lakini nilimuul;iza ni kipindi kipi ambacho Mahadhi anakitaka aonyeshe huo uwezo kama sasa wakati Msuva hayupo na bado ameshindwa kuitendea haki nafasi anayopata katika timu yake.