Simba, Gor Mahia kanyaga twende

KABLA ya swala ya Magharibi wakati waumini wa Kiislama wakijiandaa kufungulia, huenda bingwa mpya wa SportPesa Super Cup 2018 atajulikana rasmi.

Ipo hivi. Wakati tayari mashabiki wa soka wa hapa Nakuru, Kenya na huko nyumbani wakishajua nani ni mshindi wa tatu kati ya Singida United na Kakamega Homeboyz, kazi kubwa itakuwa katika mchezo huo wa fainali utakaopigwa kuanzia saa 9 alasiri.

We hebu vuta picha kidogo, bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara anakutana na bingwa wa Ligi Kuu ya Kenya. Ni ubabe mwanzo mwisho. Ni utemi wa kufa mtu.

Ni leo Jumapili Simba itakapovaana na Gor Mahia. Ni shoo ya kibabe. Ni msisimko wa ajabu. Unaambiwa mshindi wa mechi hiyo mbali na kuweka kapuni Dola 30,000 pia atajihakikishia nafasi ya kwenda nchini England kucheza na Everton. Ni furaha iliyoje.

England? Kwa Prince Harry. Kwa Malkia Elizabeth. Kwa Harry Kane na Wayne Rooney. Unaenda tu kirahisi kwa kushinda mchezo wa fainali. Ni ajabu na kweli.

SportPesa Super Cup imeyafanya maisha kuwa rahisi. Mwaka jana Everton ilitua Bongo ikacheza na Gor Mahia pale Taifa. Mwaka huu ni Gor Mahia ama Simba, mmoja anakwenda England.

Jiji la Liverpool. Jiji linalopokea meli zote kubwa duniani. Jiji la soka. Jiji la kihistoria. Nani anakwenda? Anajua Mwenyezi Mungu pekee.

Simba iko vizuri, lakini Gor Mahia iko vizuri zaidi. Mbinu za makocha na kasi ya wachezaji. Ubunifu wa baadhi ya wachezaji pamoja na hali ya hewa vitaamua nani anakwenda England leo majira ya jioni tu.

Mwanaspoti ambalo limeweka kambi mjini hapa kwa zaidi ya siku tisa sasa, linakuletea orodha ya mambo sita yatakayoamua ubingwa wa SportPesa Super Cup.

Kerr, Masoud

Nani mwenye maamuzi makubwa kwenye mechi ya leo Jumapili kama makocha wa Simba na Gor Mahia. Kaimu kocha mkuu wa Simba, Masoud Djuma amebeba hatma ya Wanasimba wote.

Ndiye aliyeongoza mazoezi ya wachezaji wote tangu pambano la nusu fainali. Ndiye anayepanga nani acheze na nani akae benchi. Ndiye atakayetoa mfumo ambao Simba itatumia kwenye mchezo wa leo na maelekezo yote uwanjani.

Huyo ndiye Masoud Djuma, kipenzi cha Wanasimba. Huyu ndiye aliyeshika hatma ya Simba kushinda mechi ya leo.

Upande wa pili atakuwepo Mwiingereza, Dylan Kerr. Kocha huyu ndiye aliipa Gor Mahia taji la Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita. Ndiye ameipeleka kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ndiye mwenye uchawi wote. Wachezaji wote wa Gor Mahia wanacheza kwa kutegemea akili yake. Ndiye anayeamua timu icheze vipi, ishambulie vipi na pia ibadilike vipi.

Kerr ameshika hatma kubwa ya Gor Mahia leo Jumapili. Kosa moja tu kutoka kwake linaweza kugharimu mchezo mzima. Ubaya zaidi ni kwamba ameipania Simba kinoma, timu yake ya zamani.

Meddie Kagere

Ni kweli timu zote zina wachezaji 11. Ni kweli kila timu itapanga mshambuliaji mmoja hadi watatu, lakini kuna Meddie Kagere.

Huyu ndiye nyota wa Gor Mahia mpaka sasa. Ana utulivu mkubwa mno anapokuwa mbele ya lango. Huyu ndiye aliyeipeleka Gor Mahia fainali. Alifunga mabao yote wakati Gor ikiilaza Singida United 2-0.

Huyo ndiye Meddie Kagere, mzaliwa wa Uganda anayecheza timu ya taifa ya Rwanda. Ndiye anayeongoza kwa mabao kwenye michuano hiyo akiwa amefunga mara tatu mpaka sasa.

Kagere ni hatari. Anajua kucheza na nafasi, kumiliki mpira na kupiga mashuti. Mabao yake yote matatu amefunga kwa staili tofauti. Sio mtu wa kumuacha karibu na lango hata kidogo. Huyu anaweza kupeleka kilio Msimbazi.

Safu ya kiungo

Siku zote nguvu ya Simba ipo kwenye safu ya kiungo. Timu yao inaweza kuzidiwa kila mahali lakini sio katikati ya uwanja. Hapo kuna Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Haruna Niyonzima.

Habari mbaya, safu ya kiungo ya Gor Mahia pia iko vizuri. Viungo wao watatu, Wendo Ernest, George Othiambo na Humphrey Mieno wako vizuri.

Mieno amewahi kucheza Azam FC na kila mtu anafahamu makali yake. Ana utulivu mkubwa akiwa na mpira na hata asipokuwa nao. Anaweza kupanga timu na kuichezesha kwa muda wote wa mchezo.

Wendo ndiye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi iliyopita dhidi ya Singida United. Hebu pata picha, Kagere alifunga mabao mawili lakini jopo la makocha kutoka Everton lilimchagua Wendo kuwa mchezaji bora wa mechi.

Kiungo huyo ni hatari. Anakaba kama hakuna kesho. Anamiliki mpira na kupiga pasi fupi na ndefu. Gor Mahia yote inategemea utimamu wake. Yuko vizuri.

Salamba, Rashid

Mastraika wawili wapya wa Simba, Mohammed Rashid na Adam Salamba nao wamebeba hatma ya timu yao kwenye mchezo wa fainali.

Rashid ameanza kwenye mechi zote mbili za awali za Simba kwenye mashindano haya lakini hakuweza kufunga bao. Bado anaonyesha kuwa na kiu ya kufanya kitu. Anamiliki mpira vizuri na kutengeneza nafasi.

Bahati mbaya kwake ni kwamba bado hajafunga bao lolote mpaka sasa. Mabao yake 10 aliyoifungia Prisons msimu uliopita bado hajaweza kuyahamishia Msimbazi.

Upande mwingine kuna mtu anaitwa Adam Salamba. Huyu hakuwepo hapa tangu mwanzo. Aliongezwa baada ya Simba kushinda mchezo wa robo fainali. Alicheza dakika chache kwenye pambano lililopita dhidi ya Kakamega Homeboys.

Salamba anatarajiwa kuanza kwenye mechi ya leo dhidi ya Gor. Ana nguvu na kasi kubwa. Ana uwezo wa kupambana na kupiga mashuti.

Watu wote wa Simba wanamtazama kama mtu atakayewasahaulisha kuhusu staa wao, Emmanuel Okwi.

Nyoni na Bukaba

Nyota hawa wawili wa Simba nao wamebeba hatma kubwa ya mchezo wa leo Jumapili. Hawa ndiyo mabeki wa kati wa Simba. Hawa ndiyo roho ya Simba. Makosa yoyote kutoka kwao yatasababisha timu yao ipoteze mchezo.

Nyoni ndiye beki bora wa Simba mpaka sasa. Ana utulivu mkubwa. Anacheza mipira ya juu na chini. Anakaba kwa akili na wakati mwingine anatumia nguvu. Huyu ndiye Nyoni, nyota wa zamani wa Azam.

Upande wake wa pili yuko Paul Bukaba. Sio mchezaji mwenye uzoefu mkubwa sana. Alijiunga na Simba mwaka jana akitokea nchini Burundi, lakini uwezo wake ni wa juu. Ana akili kubwa ya kukaba.

Japo kuna nyakati chache anapotea uwanjani, lakini ni beki mzuri. Ana changamoto kubwa ya kupambana na kina Meddie Kagere na Jacque Tuyisenge. Ni mzigo wa lawama.

Anakutana na watu wenye nguvu. Watu wanaocheza soka la kindava. Watu ambao wako fiti kwa muda wote wa mchezo. Watu ambao hawana masihara na goli. Ni wazi kuwa Bukaba ana kazi nzito.

Manula, Odhoji

Makipa hawa wawili wana kazi kubwa kwenye pambano la leo Jumapili. Kuna nyakati timu zao zitazidiwa katika maeneo yote na kutegemea uwezo wao wa kupangua mashuti.

Bahati nzuri wote ni makipa wazuri. Shaban Odhoji amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha Gor Mahia hivi karibuni.

Ana uwezo mkubwa wa kupanga safu yake ya ulinzi pamoja na kuona mashuti ya mbali. Anacheza vizuri pia mipira ya krosi na ni nadra kumwona ametoka halafu asicheze mpira. Ni kipa mzuri.

Kazi pia itakuwa kwa Manula. Kipa namba moja nchini Tanzania. Ameonyesha uwezo wa juu kwenye mechi mbili zilizopita. Anacheza mashuti ya mbali na karibu. Ni mzuri pia kwenye mikwaju ya penalti. Huyu ndiye Manula.

Ikitokea pambano la leo Jumapili limekwenda kwenye changamoto ya mikwaju ya Penalti, Manula ndiye atakuwa tegemeo zaidi. Ana uwezo mkubwa wa kushika mipira hiyo ya mita sita. Sio mtu wa mchezo mchezo.

Yote kwa yote, pambano la fainali leo Jumapili litakuwa la kukata na shoka. Timu bora katika mechi kali. Atakayeteleza tu itakula kwake.

Hali ya hewa nayo itakuwa na nafasi yake ya kuchangia matokeo ya ushindi kwa timu moja ama kuikandamiza timu nyingine. Mfano pambano la nusu fainali kati ya Gor Mahia na Singida United liliharibiwa na mvua.