Fainali ya NBA ilikua bab'kubwa

KIFYAGIO! Ndicho kilichotokea katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Kikapu Marekani, alfajiri ya jana baada ya Golden State Warriors kushinda 108-85 dhidi ya Cleverland Cavaliers na kutetea taji lao kwa ushindi wa jumla 4-0.

Warriors baada ya kushinda mechi mbili za kwanza kwenye uwanja wao wa Oracle Arena ilitarajiwa itapata wakati mgumu ugenini kwa Cavaliers ambao hutumia Uwanja wa Quicken Loans Arena katika mechi mbili zilizofuata, ila haikuwa hivyo badala yake walifanikiwa kushinda mfululizo na kuandikisha ushindi wa bila kufungwa ‘Sweep’ tofauti na ilivyotarajiwa.

Ushindi wa Warriors umeifanya timu hiyo kushikilia taji hilo kwa mara ya tatu ndani ya misimu minne mbele ya Cavaliers wakirudia rekodi yao ya kuwa timu ya mwisho kupoteza hivyo mwaka 2007 dhidi ya San Antonio Spurs na mwaka huu kupoteza mbele ya Golden State Warriors.

Nyota Kevin Durant alichaguliwa Mchezaji mwenye thamani zaidi wa mchezo wa fainali (MVP) ikiwa ni msimu wa pili mfululizo kubeba tuzo hiyo baada ya msimu uliopita kushinda tuzo hiyo.

Tuzo ya Mchezaji mwenye thamani zaidi msimu huu ‘MVP of the season’ ilibebwa na nyota James Harden wa Houston Rockets aliyeng’ara vilivyo na timu hiyo iliyofungwa kwa mbinde fainali ya ukanda wa Magharibi dhidi ya Golden State Warriors waliolazimika kusubiri mchezo wa saba kujua hatma yao.

WARRIORS WALISTAHILI

Hii ni sababu mojawapo iliyowabeba Warriors kutetea ubingwa wao msimu huu mbele ya Cavaliers ambao haikuwa na wachezaji wazuri kulinganisha na wapinzani wao. Uwepo wa wachezaji zaidi ya watatu wenye kiwango cha daraja la kwanza ambao ni Stephen Curry, Klay Thompson, Draymond Green na Kevin Durant imekuwa chachu ya timu hiyo kushinda taji hilo kiurahisi mbele ya Cavaliers.

Mbali na nyota hao, lakini ushirikiano wao mzuri uliwabeba kwani kuna wakati timu ilipobanwa kila mmoja aliweza kutumia ubora wake binafsi kuisaidia timu hususani mchezo wa kwanza na mchezo wa tatu ambao kama sio juhudi zao fainali ingeendelea hadi mchezo wa sita au saba.

CAVALIERS LAINI SANA

Sababu nyingine iliyobeba Golden State Warriors kubebea taji mfululizo ni ushindani kiduchu wa wapinzani wao Cavaliers ambayo msimu huu hawakuwa na kiwango kizuri kulinganisha na misimu mitatu iliyopita. Cavaliers tangu msimu wa ligi wa kawaida ‘Regular Season’ ilikuwa inachechemea japo walitumia uzoefu wao kushinda hatua ya mtoano ukanda wa Mashariki.

Cavaliers ilifanya kazi kubwa ya kushinda ubingwa wa Kanda ya Mashariki dhidi ya mabingwa wa Kihistoria Boston Celtics waliowatangulia katika mechi za fainali yao iliyoamuliwa na mchezo wa saba ambao Cavaliers waliibuka na ushindi.

Katika mchezo wa mwisho jana alfajiri, Cavaliers wakuwa na mchezo mbovu zaidi ya mechi mitatu ya awali na walionekana kuchoka na kushindwa kuhimili mbele ya

Warriors waliocheza kwenye kiwango bora kuanzia robo ya kwanza hadi ya mwisho na kushinda kwa uwiano mkubwa zaidi 108-85 ambao ni tofauti ya pointi nyingi zaidi kulinganisha na mechi 3 za kwanza.

Nyota LeBron James ndiye aliyeibeba timu hiyo kucheza fainali ya kikapu kutokana uwezo binafsi alionao tofauti na wengine waliopo kwenye timu hiyo pamoja na Kevin Love ambaye anashirikiana naye kuisaidia timu hiyo ambayo tangu kuondoka kwa nyota Kyrie Irving aliyeacha pengo kikosini.

Ubovu wa timu hiyo umewafanya washindwe kupata angalau ushindi katika mechi 4 kama walivyojaribu msimu uliopita waliposhinda mchezo 1 na kulazimisha mechi ya 5, endapo Cavaliers wangepindua matokeo ya 3-0 wangekuwa timu ya kwanza kufanya hivyo kwenye historia ya kikapu nchini humo hakuna timu iliyowahi kufungwa mechi 3 za mwanzo na kupindua matokeo.

LEBRON KUIKACHA CAVALIERS?

Hili ni swali ndilo linaloulizwa na wengi wakitaka kujua uwezekano wa nyota huyo kuikacha timu yake ya Cavaliers kutokana na kumalizika kwa mkataba wake ndani ya timu hiyo na sasa yupo huru kuchagua timu ya kuchezea msimu ujao.

Kuna uwezekano mkubwa zaidi wa LeBron kuachana na timu hiyo haswa kutokana na kubebeshwa zigo zito tofauti na nyota mwenzake anayetajwa kwa ubora kama yeye Stephen Curry ambaye hatumikii mzigo mzito kwenye timu yake ya Golden State Warriors kutokana na uwepo wa nyota wakali Klay Thompson na Kevin Durant.

HAKUNA ZIARA YA WHITE HOUSE

Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa hatotoa mwaliko kwa nyota LeBron James wala Stephen Curry pamoja na timu itakayobeba ubingwa wa msimu huu.

Kauli ya Trump ilikuwa ni kama majibu kwa nyota wa timu hizo LeBron na Curry ambao walishazungumza mapema kwamba hawana mpango wa kutembelea Ikulu hiyo baada ya kumalizika kwa fainali baina yao, hivyo Golden State Warriors haitaenda White House licha ya kubeba taji hilo.