Cannavaro anakabidhi viatu vyake Yanga hapa

UMEKAA unatazama filamu kali ya kimapigano ya Jet Lee iitwayo ‘Tai Chi’. Unamwona yule Jet Lee, ulikuwa hata kwa kuangalia tu kupitia runinga, unamwogopa.

Jet Lee wa sasa hawezi hata kurudisha ngumi kwenye ugomvi. Sio yule tuliyomzoea katika filamu zake tamu zile akiruka angani na kuwadondosha maadui zaidi ya kumi. Umri umemtupa na anaonekana kuchoka sana.

Ndivyo maisha yalivyo. Yanakwenda kasi sana na ukiona tu mambo uliyozoea kufanya yanagoma, jua kabisa ndo basi, wapishe wengine.

Hakuna anayeweza kushindana na kasi hii ya maisha. Unaweza ukapanga kufanya jambo kubwa katika kazi ambayo umeizoea lakini unashindwa kutokana na ukomo wa mawazo yako. Hapo ndipo unagundua haina haja ya kulazimisha, bali kukaa tu pembeni.

Hata kwa upande wa wachezaji, wapo ambao wanakimbizana na maisha na kufanya mambo makubwa lakini wanapofika mwisho, wengine hulazimisha kukaza kuona watafanya jambo kubwa lakini mwishowe wanaishia kuwa vichekesho uwanjani baada ya kusahau jua ni la jioni.

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ nani asiyemjua. Beki kisiki wa Yanga ambaye amedumu na klabu hiyo zaidi ya misimu kumi akiisaidia kubeba mataji kibao.

Bila shaka, msimu huu uliomalizika nahodha huyu wa Yanga amepitia wakati mgumu sana. Amekuwa akisugua sana benchi tofauti na tulivyomzoea, amepata nafasi chache sana za kucheza. Cannavaro ni wa kukalishwa benchi? Hapo ndipo utapogundua kweli maisha yanakimbia si mchezo.

Hapo ndipo unapogundua umri umemtupa mkono na anatakiwa bapishe damu changa itakayoweza kuendana na kasi ya maisha ya sasa. Sina maana kama Cannavaro kafika mwisho, ila ukweli yale makali yake si yale ya miaka mitatu iliyopita.

Sasa jiulize endapo akaamua kutundika daruga, ni nani anaweza kuvaa viatu vyake pale Jangwani?

Mwanaspoti inakuletea wachezaji ambao endapo watapata nafasi ya kucheza katika kikosi hicho cha mabingwa hao wa kihistoria, wanaweza kufanya vizuri na kuisaidia timu.

Juma Kennedy, Singida United

Pamoja na kuwa amecheza msimu uliopita kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara akiwa na Singida United, ameonyesha uwezo wa juu kwa kuwadhibiti washambuliaji wenye uzeofu na ligi hiyo. Urefu, nguvu na akili ni miongoni mwa vitu ambavyo vinaweza kuisaidia Yanga kama itamsajili beki huyo kwa lengo la kuziba nafasi ya Cannnavaro.

Iddy Moby, Mwadui FC

Beki huyu amekuwa na msimu mzuri msimu uliopita. Ameisaidia Mwadui kubaki Ligi Kuu baada ya kujikuta katika hekaheka za kujinasua katika mstari wa kushuka daraja.

Ukiangalia umbo la Moby, utagundua ana kitu cha kupeleka pale Jangwani kuwasaidia. Mwili wake umejengeka kimichezo, kimo cha wastani na nguvu za miguu. Ni miongoni mwa mabeki wasumbufu na ana uwezo wa kupambana na washambuliaji wenye kiu ya kufunga. Ni wazi akikosekana katika kikosi chao huwa ni pengo kwa sababu anamudu zaidi katika safu ya nyuma ya kikosi hicho.

Nudrin Chona, Prison

Beki huyu ana uwezo mkubwa na aliisaidia timu yake kumaliza katika nafasi nzuri msimu uliopita huku ikiwa imeruhusu mabao machache.

Uzoefu wake kwenye Ligi Kuu unamfanya awe mmoja wa mabeki bora na sahihi kwenda kujiunga na Yanga kama atapata nafasi hiyo kuziba pengo la Canavaro.

Agrey Morris, Azam

Itakuaje endapo atasimama pale nyuma pamoja na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wakati Yanga ikipambana kusaka pointi tatu? Lazima wawe chachu ya ushindi kutokana na kombinesheni watakayoiunda kama wafanyavyo katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.

Pale Azam FC ni mchezaji tegemeo katika nafasi ya beki kutokana na umahiri wake. Pamoja na makosa madogo madogo, lakini alikuwa ndiye mhimili mkuu katika safu ya nyuma ya Azam na kuifanya timu yake hiyo kuruhusu idadi ndogo ya mabao msimu uliopita. Akitua pale Yanga atavaa tu viatu vya Cannavaro.

Mohammed Fakhi, Kagera Sugar

Mashabiki wa Simba hawawezi kumsahau beki huyu baada ya kuwatibulia ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2016/17.

Hata hivyo, ni kama machungu yameisha baada ya kutwaa ubingwa huo msimu huu baada ya kuusotea kwa kipindi kirefu, lakini kuhusu zile kadi tatu za njano alizohusishwa nazo Fakhi, sidhani kama watamsahau.

Unaweza kumwita beki wa mechi kubwa kutokana na uwezo wake wa kuzidhibiti timu kubwa. Emmanuel Okwi pamoja na kuwa kinara wa mabao lakini alikuwa akidhibitiwa vizuri tu alipokutana na Fakhi ambaye amekuwa katika ubora. Ni wazi akitua pale Yanga kuvaa viatu vya Cannavaro, vitamfiti sana tu.

Ally Ally, Stand United

Hiki ndio kipaji sasa. Msimu wake wa kwanza tu lakini ameonyesha ukomavu wa hali ya juu katika soka la kiushindani. Ameizoea Ligi Kuu haraka sana na kuwa msaada mkubwa kwa klabu yake.

Msimu uliopita aliweza kuwasumbua washambuliaji nyota na kuwakosesha nafasi za kuonyesha ukongwe wao kila walipokutana na timu yake.

Ni wazi anaweza kuvaa viatu vya Cannavaro pale Yanga kwani ana anaweza kufanya mambo makubwa kutokana na uwezo wake wa kudhibiti washambuliaji.