Winga wa Simba anayetesa Azam

ITACHUKUA muda mrefu Simba kushtuka. Unajua kwa nini? Klabu hii imekuwa ikizalisha na kuwaibua nyota wa soka wangali wadogo, lakini imekuwa hainufaiki nao. Simba imekuwa ikitengeneza vijana wengi wenye viwango vikubwa, lakini huwa hawatumiwi vya kutosha na klabu hiyo na kuwafanya watimke katika timu nyingine na kupata mafanikio makubwa wakiwa huko.

Bahati mbaya, mabosi wa klabu hiyo hulazimika kutumia fedha nyingi kuwarejesha tena kikosini vijana waliowaibua baada ya kuona wametamba katika klabu nyingine.

Nyota mwingine aliye zao la Simba ni Idd Kipagwile anayekipiga Azam FC, akiwa kwenye kiwango kikubwa tangu alipokuwa Majimaji kabla hata ya kujiunga na matajiri wa Chamazi.

Mwanaspoti lilifanikiwa kufanya naye mahojiano baada ya kutembelea katika ofisi zake maeneo ya Tabata Relini.

ALELEWA SIMBA, AIBUKIA MAJIMAJI

Winga huyu mwenye spidi ya kufa mtu, alikichezea kikosi cha vijana Simba msimu wa 2014-2015 alipopandishwa timu ya wakubwa, lakini baada ya kukosa nafasi ya kucheza aliomba atimkie Majimaji.

“Msimu huo nilikuja Simba nikiwa kama timu B baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya vijana, nilimkuta Kocha Zdravkov Logarusic, lakini sikupata nafasi. Ila alipokuja Patrick Phiri nilipata nafasi za kucheza ila haikuwa muda mwingi nikaenda zangu Majimaji,” alisema na kuongeza akiwa huko alijitahidi kufanya vizuri kwani lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha anapata nafasi ya kuonekana.

MSIMU HUU JE?

Kipagwile aliyeichezea Azam kwa msimu wake wa kwanza akitokea Majimaji alisema msimu huu umekuwa na changamoto nyingi kwake kutokana na ugeni.

Hata hivyo, cha kufurahisha, alikuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mromania, Aristica Cioaba kabla ya Idd Nassor ‘Cheche’ kuachiwa timu na kuwa chaguo la pili.

“Cheche na Cioaba walifanya kazi pamoja, ila sina tatizo kuanzia benchi, naamini utafika muda naweza nikawa mchezaji wa kikosi cha kwanza, kila kocha huwa na falsafa yake,” anasema.

TOFAUTI YA AZAM

Wakati anaingia Azam nyota tegemeo waliokuwa ndani ya kikosi hicho, John Bocco, Erasto Nyoni, Aishi Manula na Shomari Kapombe walikuwa wakiondoka kikosini.

Wengi waliamini Azam haitofanya vizuri, lakini jambo hilo limekuwa tofauti kwani timu imemaliza nafasi ya pili katika Ligi.

“Mapengo yao hayajaathiri sana na katika hilo ukitaka kuamini, msimu uliopita tulimaliza tukiwa nafasi ya nne na wao walikuwepo, ila msimu huu tumemaliza nafasi ya pili, hii ndio tofauti, japokuwa kullikuwa na majeruhi wengi.”

MZIKI WA KICHUYA

Ni ngumu kuamini, lakini ndivyo ilivyo, winga huyu amejikuta akivutiwa na kiwango cha winga mwenzake, Shiza Kichuya wa Simba.

“Kichuya ni mchezaji mzuri sana ananivutia anapokuwa uwanjani kwani anajituma na ukimwangalia kwa haraka haraka unaweza usijue kabisa anacheza namba ngapi uwanjani,” anasema.

Kipagwile aliongeza, yeye aina ya mchezaji kama Kichuya, kwani anapokuwa uwanjani hupenda kuonekana kila sehemu ili kuhakikisha timu inashinda.

CHAMA LA ZAMANI

Majimaji ni timu aliyoichezea na bahati mbaya msimu huu imeshuka daraja, yeye akiwa ndani ya Azam, winga huyo analizungumziaje?

“ Ni timu yangu ya nyumbani siwezi kuisahau hata kidogo, tatizo mfumo wa uendeshaji, wanatakiwa wabadilike lakini kama hawatobadilika watapanda na kushuka tena na tena, pia lazima viongozi wajenge utamaduni wa kuwalipa wachezaji pesa zao ili waweze kufanya kazi bila kuwa na mawazo mengine.”

Anasema licha ya kuwapo na sababu nyingine za kuzama kwao, lakini kubwa kupungua morali ya wachezaji kiasi wengine kuamua kuingia mitini kuikacha timu hiyo na kuiacha ikizama shimoni.

Anaongeza ipo tofauti kubwa ya Majimaji na Azam, akidai Azam inajiendesha yenyewe huku Majimaji ukiendeshwa na wananchi hivyo kushindwa kuhimili kashkashi za Ligi Kuu Bara.

SIRI YAKE NA SIMBA

Inakumbukwa Kipagwile aliwatungua Simba katika mechi ya makundi ya Kombe la Mapinduzi kiasi cha kubatizwa jina la Mtoto Idd ukirejewa wimbo maarufu wa zamani wa Sir Juma Nature.

Pia ilifichuliwa alikuwa mbioni kurejea nyumbani, Wekundu wa Msimbazi, hata hivyo Kipagwile anafunguka kwa kusema haikuwa kweli kama alikuwa mbioni kurudi.

“Najua kabisa ni rahisi kuingia Simba kama ukiwa umepitia katika falsafa yao ya vijana, nimeliona hilo hata kwa Marcel, lakini kama ikitokea Simba ikataka kunirudisha nitaenda kikubwa ni masilahi, japo kwa sasa akili yangu kumaliza mkataba na klabu yangu.”

HESABU ZA KIBABE

Wachezaji wengi wanapokuwa wakicheza huwa wanafikiria soka la kimataifa ili waenda kucheza soka la kulipwa, kwa upande wake, anasema cha kwanza kwake ni masilahi.

“ Mipango yangu ni kwenda mbele zaidi ya hapa na naamini kabisa nipo sehemu salama, bado sijamaliza ila wachezaji wengi tunapigania masilahi kama nikipata pesa nabaki hapa hapa, wachezaji hutafuta masilahi zaidi, ndio muhimu,” anasema.

AMKUBALI NGOMA

Azam imemsajili Donald Ngoma kutoka Yanga walioachana naye, Kipagwile anazungumziaje ishu ya Mzimbabwe huo?

“Ni mchezaji mzuri anayejua kufunga na miguu yake na hata kichwa, ana vitu vingi sana, kikubwa awe fiti ndio utajua Ngoma ni mchezaji wa aina gani. Huwa namkubali sana huyu jamaa.

Anasema Ngoma ni aina ya wachezaji wapambanaji na anayetaka kufunga muda wote, hivyo kwa upande wake akipata nafasi atakuwa na kazi moja ya kumtengenezea nafasi afunge.