Mourinho: Anavyoukabili ugumu wa kushusha makali ya City

SAWA Manchester United imemaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England, lakini msimu wa 2017/18 ulikuwa mwingine wa ovyo katika maisha yao ndani ya ligi hiyo kwa muongo mmoja uliopita. Kilichotokea ni kwamba yalikuwa maendeleo mazuri tu katika msimamo wa ligi hasa baada ya kumaliza nafasi ya saba, nne, tano na sita kwa misimu minne iliyopita.

Katika ukweli huo huo, Man United hawajawahi hata kuonyesha kuwa na nafasi ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England na mataji mengine mambo ni magumu pia. Wakati Man United ikishindwa kufanya kile kinachoendana na hadhi yao, kwa majirani wanaowaita wapiga kelele, Manchester City mambo ni moto kweli kweli wakibeba mataji tu.

Kwa msimu huu uliomalizika, Man United iliumbuliwa na Man City, wakiachwa nyuma kwa pointi 19. Yani Man United iliyoshika nafasi ya pili imeachwa pointi nyingi na timu namba moja kuliko pointi ilizowaacha Arsenal, waliomaliza nafasi ya sita. Man United imeizidi Arsenal pointi 18, lakini yenyewe imezidiwa pointi 19 na Man City.

Ukweli mwingine ni kuwa Man United wameshuka kwa kasi kubwa tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu. Man City wamekuwa kinyume chake, wanapanda kuliko kawaida, wakizidi kuimarika mwaka hadi mwaka. Kitu ambacho imekifanya msimu huu ni kujaribu kuwazuia tu Man City wasishangilie ubingwa kwenye Manchester derby.

Mambo ni tofauti kabisa na miaka iliyopita, wakati Man United ile ya Sir Alex ilipokuwa ikitoa vipigo tu kwa timu zote duniani.

Msimu ambao kocha huyo raia wa Scotland alipoondoka 2012-13 ndiyo hasa Man United ikaanza kushika kasi katika kuporomoka. David Moyes na Louis van Gaal wakaja kikosini, lakini kwa bahati mbaya Man United haikuwa kiatu cha saizi yao, kilipwaya na hawakuweza kukivaa. Walau kidogo, Van Gaal alikuwa na uzuri wake kuliko Moyes kwa nyakati walizokuwa Old Trafford. Mourinho amefanya vizuri, akishinda ubingwa wa Kombe la Ligi na Europa League mwaka jana na walau kidogo aliwarudisha Man United kwenye makali yao na kurudi Top Two. Lakini, hilo halitoshi. Shabiki wa United hawezi kulikubali hilo kuwa imefikia mafanikio mwaka huu.

Msimu wa 2007-08 na 2008-09, ilishinda ubingwa wa Ligi, wakati huo Man City ikiwa nafasi ya tisa na 10 huko.

Wakati Man United wakianza kushuka kiwango chao kabla ya Ferg hajaachia ngazi, Man City wao taratibu walikuwa bize kupunguza pengo baina dhidi ya mahasimu wao. Man City hii ya sasa haishikiki na ina pesa za kutosha, msimu wa 2009/10 walimaliza ligi wakiwa nafasi ya tano na United wakashika namba mbili. Kumbuka msimu mmoja uliopita kabla ya hapo, Man United walikuwa namba moja na Man City namba 10, lakini hapo City wamepanda hadi namba tano na United wameshuka hadi namba mbili. Msimu uliofuatia, 2010/11 Man City wakapanda hadi nafasi ya tatu, lakini Man United wakabeba ubingwa. Ulipokuja msimu wa 2011-12, Man City wakapindua meza, wakaishusha Man United kileleni na kubeba ubingwa, huku vijana hao wa Old Trafford wakishika nafasi ya pili. 2012/13 Man United wakarudi kileleni na Man City wakawa nafasi ya pili, huo ndiyo uliokuwa msimu wa mwisho wa Ferguson klabuni hapo. Msimu uliofuatia, Man United ikaanguka hadi nafasi ya saba, wakati Man City wao wakibeba ubingwa.

Ikafuatia misimu mitatu mfululizo, Man United iliingia mara moja tu Top Four - ikiwaliza nafasi ya nne kwenye msimu wa 2014/15, nafasi ya tano kwenye msimu uliofuatia na wakashuka zaidi kwenye msimu wa 2016/17 walipomaliza kwenye nafasi ya sita. Kwa upande wa Man City, wao wamekuwa ndani ya Top Four mara zote hizo wakishinda namba mbili, nne, tatu na moja.

Upepo wa mafanikio unaonekana kupinduka tena, Man City wanaonekana kuwa ndiyo wa watalawa na si Man United tena. Amekuja na kujaribu kupambana na hilo, lakini ni kitu kinachonekana wazi kuwa hii ni zamu ya Man City kutesa. Mourinho bado ana kazi nzito kwa sababu mashabiki wa Man United siku zote wanahitaji kuwa juu ya wengine. Kwa sasa anahangaika kutengeneza kikosi cha kushindana na Man City, lakini bado ni vita ngumu kwelikweli kuikabili.