WAKO WAPI MAKOCHA HAWA WALIOPITA SIMBA, YANGA? -4

Muktasari:

  • Majina makubwa ya kigeni ambayo yalizinoa Yanga na Simba na kutimuliwa bila ya kujali wasifu mkubwa ama klabu za maana walizofundisha awali kama Kosta Papi (Yanga) na Patrick Liewig (Simba), sio ishu kabisa.

UKIVURUNDA kwenye klabu za Simba na Yanga hata kama ulikuwa kocha wa zamani wa Manchester United ya England au FC Barcelona ya Hispania, hapa lazima utimuliwe tena mchana kweupee.

Majina makubwa ya kigeni ambayo yalizinoa Yanga na Simba na kutimuliwa bila ya kujali wasifu mkubwa ama klabu za maana walizofundisha awali kama Kosta Papi (Yanga) na Patrick Liewig (Simba), sio ishu kabisa.

Simba na Yanga ambao watakutana, Aprili 29 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, wamefanya mabadiliko ya makocha mara 38 kwenye idadi hiyo, Yanga ni mara 20 huku kwa Simba ikiwa mara 18 toka mwaka 2000.

Tupo kwenye hitimisho ya kukuletea wanachokifanya kwa sasa makocha waliopita kwenye klabu hizo kongwe hapa nchini kwa kipindi chote hicho, wapo wanaoendelea kutesa na wengine ndio wamepotea kabisa. Endelea nayo…

KOSTADIN PAPIC- YANGA

Papic (58) ni mmoja wa makocha wenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika kutokana na kufundisha klabu za mataifa kama Afrika Kusini, Ghana, Nigeria na Tanzania.

Kocha huyo, Mserbia ambaye alijiunga na Yanga kwa kusaini mkataba wa miaka miwili, alijiondoa klabuni hapo mwishoni mwa msimu wa 2011/2012 kutokana na kutofautiana na viongozi wa timu hiyo.

Haikumchukua muda Papic kupata dili lingine mara baada ya kuikacha Yanga, alitua Black Leopards ya Afrika Kusini, aliinoa timu hiyo ya daraja la kwanza kwa msimu mmoja wa 2013-2014.

2014 akajiunga na Chippa United ambayo aliifundisha kwa nusu msimu na kutimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ndani ya mwaka huo huo, alipata kibarua kingine cha kuinoa Polokwane City ambayo ilitaka kumsajili, Elias Maguli.

Papic akiwa na Polokwane alidumu kwa misimu miwili na kutimuliwa msimu uliopita wa 2016-2017. Mwanzoni mwa msimu huu alipata kibarua cha kuinoa, Royal Eagles ya daraja kwanza nchini humo, lakini kutokana na mwenendo mbaya ametimuliwa na nafasi yake kushikwa na Roger Sikhakhane.

MILOVAN CURKOVIC –SIMBA

Kibarua cha Milovan Simba kiliota nyasi Aprili 2008, Mserbia huyo naye ni miongoni mwa makocha waliopita Simba na kukaa kwa kipindi kifupi.

Milovan alijiunga na Simba Novemba 2007, alipotimuliwa alitokomelea kwao, Serbia.

SAM TIMBE- YANGA

Mganda Timbe, ambaye aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-2012 mara baada ya kuchukua mikoba ya Kostadin Papic hakuwa na maisha marefu sana Yanga.

Alipotimuliwa Yanga, Timbe alikwenda Burundi ambako na kwenye aliipa ubingwa, Atraco.

Timbe kwa sasa ni kocha wa Tusker ya Kenya ambayo pia alikuwa akiichezea winga wa Kitanzania, Abdul Hilal ambaye ametimka kwenye timu hiyo kwa mkopo kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga ni miongoni mwa makocha bora wa ukanda huu wa Afrika Mashariki kutokana na mafanikio aliyonayo ya kushinda mataji manne ya kombe la Chalenji.

MOSES BASENA-SIMBA

Majanga ya Phiri, ambaye alitimuliwa kwa kipindi kifupi ndani ya Simba kwenye awamu yake ya tatu, yalimkuta na Basena ambaye aliifundisha Simba kuanzia mwezi Juni hadi Novemba, 2011.

Basena, ambaye mwaka jana alitangazwa na Rais wa Chama cha Soka Uganda, Fufa, Eng. Moses Magogo kuwa kocha wa muda mfupi, kwa sasa hana timu.

Kabla ya kuwa kocha wa muda wa The Cranes aliwahi kuwa msaidizi wa Bobby Williamson ndani ya timu hiyo na baadaye 2013 kutimka kwenye usaidizi.

Lakini, kocha huyo alirejea kwenye nafasi hiyo, 2015 na kuwa chini ya Micho, baada ya Micho kuondoka alipata kibarua hicho cha muda mfupi na kuiongoza Uganda kwenye michezo minne kisha nafasi yake ikachukuliwa na Mfaransa, Sébastien Desabre.

TOM SAINTFIET- YANGA

Kati ya makocha wa kigeni waliozunguka kwenye klabu nyingi zaidi hadi kutua nchini, Tom anaweza kuwa namba moja, jamaa alizinoa timu 13 kabla ya kuingia mkataba na Yanga, 2012 akitoka kuwa Kocha wa timu Taifa ya Ethiopia.

Yanga iliachana naye ndani ya mwaka huo, baada ya kupewa Kombe la Kagame 2012 na unaambiwa Tom hakulaza damu fasta akaibukia dili lingine la kujiunga na timu ya Taifa ya Yemen, ambayo aliifundisha kwa kipindi kifupi na kuwa kocha wa Malawi, 2013.

Mwaka 2014 akajiunga na Free State Stars ya Afrika Kusini nako akatimuliwa Mbelgiji huyo, ambaye alipata dili lingine la kuwa kocha wa Togo ambayo aliingoza na kufuzu kwenye Afcon ya 2017 kule Gabon.

Tom alitimuliwa baada ya kufanya vibaya kwa Togo, lakini alipata dili na kusaini mkataba wa miezi mitatu ya kuinoa, Bangladesh mwezi Juni 2016.

Baada ya miezi mitatu yake kukatika akapata kibarua kingine cha kuifundisha timu ya taifa la Trinidad & Tobago, lakini Oktoba 11 mwaka jana, alipata kibarua kipya alichona nacho mpaka sasa cha kuifundisha timu ya taifa la Malta.

PATRICK LIEWIG- SIMBA

Mfaransa Liewig (68) alipata kibarua cha kuinoa Simba, Disemba 2012 na kufungashiwa virago vyake, Mei 2013 baada ya mambo kwenda kombo akiwa na wababe hao wa Msimbazi.

Stand United ilimshika shati na kocha huyo akakubali kuwanoa kwa muda mfupi kabla ya kutimka na kuelekea Tunisia kwenye klabu ya Grombalia Sport. Mwaka uliofuata alipewa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Ufundi ndani ya klabu huyo.

ERNIE BRANDTS-YANGA

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa la Uholanzi, Brandts naye alitimuliwa Yanga mwaka 2013 baada ya kuwafundisha mabingwa hao watetezi kwa mwaka mmoja na kuwapa mataji yote ya ndani.

Mwaka 2016 alichaguliwa kuwa kocha msaidizi wa Nijmegen Eendracht Combinatie (N.E.C.) ya Ligi Daraja la Kwanza, Uholanzi.

ABDALLAH KIBADENI- SIMBA

Kibadeni ‘King Mputa’ baada ya kutumika sana kwenye soka la Tanzania na kuweka rekodi kwenye uchezaji wake ya kufunga hat trick kwenye mchezo wa watani wa jadi, Julai 19 1977 kwa sasa anaendesha kituo chake cha soka, Kisa.

King Mputa, ambaye aliichezea Simba kwenye kiwango cha juu alitimuliwa kwenye nafasi ya ukocha, Novemba 2013. Kibaden anatajwa kuwa mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa kwenye soka la Tanzania.

Mbali na Simba, pia amepata kuzifundisha timu za Ashanti United, JKT Ruvu, ambazo zote huko alitengeneza vikosi matata na kuibua vipaji vya maana.

HANS VAN PLUIJM- YANGA

Kwa sasa ni Kocha wa Singida United, ambaye ameifanya timu hiyo kuwa ya ushindani licha ya kuwa ngeni Ligi Kuu Bara.

Pluijm kwa sasa anahusishwa kujiunga na Azam, alitimuliwa Yanga kwa awamu ya pili, 2016 akiwa kwenye nafasi ya ukurugenzi wa ufundi baada ya mikoba yake kuchukuliwa na George Lwandamina.

ZDRAVKO LOGARUŠIĆ-SIMBA

Simba ilimtimua, Logaruši mwaka 2014, kocha huyo mara baada ya kutimuliwa alizinoa, AFC Leopards (Kenya), G.D. Interclube (Angola) na Asante Kotoko ya Ghana, Mcroatia huyo kwa sasa anaifundisha timu ya taifa la Sudan.

LWANDAMINA & MAXIMO- YANGA

Mechi ya nani mtani jembe, 2014 ilimuondoa, Mbrazil Marcio Maximo na kurejea kwao Brazil. George Lwandamina, ambaye ameitema Yanga hivi karibuni kutokana na kudai kuchoshwa na baadhi ya mambo. Hata hivyo, Lwandamina ni tofauti na makocha wengine, yeye hajafukuzwa bali amekimbia timu hiyo huku akitoa masharti kadhaa. Pia, ana ofa mezani inamsubiri ya kuinoa Zesco United ya Zambia. Kuondoka kwa Lwandamina ambaye ameiongoza Yanga kwenye mazingira magumu kutokana na kukabiliwa na ukata na majeruhi kwa wachezaji wake muhimu.

KOPUNOVIC, MAYANGA & OMOG – SIMBA

Mserbia Goran Kopunovic ambaye alitimuliwa Simba, 2015 kwa sasa hana timu ila anahusishwa kujiunga na Szeged ya Hungari baadaye mwakani.

Jackson Mayanga, ambaye alitimuliwa Simba Mei 2016 kwa sasa hana timu huku kwa upande wa Joseph Omog, ambaye alichukua mikoba ya Mayanga na kutimuliwa anatarajia kujiunga na AC Leopards ya DR Congo. Omog, ambaye alitumuliwa na nafasi yake kushikwa na Kocha msaidizi, Masudi Djuma anayesaidiana na Mfaransa, Peirre Lechantre kwa sasa.

Kwa pamoja Lechantre na Djuma wanafurahia kikosi cha matata cha Simba, ambacho idadi kubwa ya wachezaji wamesajiliwa chini ya utawala wa Mkameruni hiyo, ambaye pia amepata kuinoa Azam FC.