Wenger kubwaga manyanga Arsenal

Muktasari:

  • Kocha huyo amekuwa kwenye kikosi hicho tangu mwaka 1996 na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na saba ya Kombe la FA. Ni karibu miaka 22.

LONDON, ENGLAND

HABARI ndiyo hiyo. Arsene Wenger atang’atuka Arsenal mwishoni mwa msimu huu.

Kocha huyo amekuwa kwenye kikosi hicho tangu mwaka 1996 na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na saba ya Kombe la FA. Ni karibu miaka 22.

Wenger (68) anasifika kwakulibadilisha soka la England kwa miongo miwili iliyopita tangu alipotua Arsenal akitokea Japan. Alitua kwenye kikosi hicho kuchukua mikoba ya Bruce Rioch na kuibadili kabisa Arsenal kiuchezaji, ikicheza soka maridadi huko Highbury kabla ya sasa kuhamia Emirates.

Makali yake yalionekana zaidi katika msimu wa 2003/4, ambapo Arsenal ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu England bila ya kupoteza mechi, huku kikosi chake ndicho kilichokuja kuvunja utawala wa Manchester United kuanzia miaka ya tisini hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Upinzani wake dhidi ya Sir Alex Ferguson na Jose Mourinho ulipata umaarufu na kuzifanya mechi za Arsenal na Man United kuwa na mvuto wa kipeke duniani.

Wenger alisema: “Baada ya kufikiria kwa kina na kufuatia majadiliano na klabu, nadhani huu ni wakati mwafaka wa kung’atuka mwishoni mwa msimu huu.

“Nashukuru kwa kupata nafasi kubwa ya kuinoa timu hii kwa miaka mingi. Nimeiongoza klabu kwa kujitoa sana na uhakika mkubwa. Nataka kuwashukuru makocha wengine, wachezaji, wakurugenzi na mashabiki kwa kuifanya klabu hii kuwa spesho kabisa. Nawaomba mashabiki wasimame nyuma ya timu ili tumalize msimu vizuri. Mapenzi yangu na sapoti yangu itakuwa kwenye timu hii milele.”

Kung’atuka kwa Wenger tayari kumezua mjadala ni kocha gani atakayechukua mikoba yake baada ya kuwapo kwa orodha ndefu kuanzia kwa Thomas Tuchel, Joachim Low, Brendan Rodgers, Patrick Vieira, Carlo Ancelotti, Max Allegri, Steve Bould, Luis Enrique, Diego Simeone, Thierry Henry, Mikel Arteta na Antonio Conte.

Wenger ameshindwa kuipa Arsenal taji kubwa la Ulaya tangu alipotua kwenye kikosi hicho na alikaribia mwaka 2006 wakati alipochapwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Barcelona. Lakini, kumbukumbu nzuri juu yake ni pale alipoweza kuihamisha timu hiyo kutoka Highbury hadi Uwanja wa Emirates wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 60,000 wanaoketi.

Lakini tangu alipotua Emirates mambo ndiyo yamekuwa mabaya zaidi na kuibuka kundi linalompinga na kumtaka aachie ngazi mara kadhaa kutokana na kushindwa kuonyesha upinzani anapokabiliana na vigogo wenzake kwenye ligi. Kumbukumbu nyingine nzuri ya Wenger ni ile ya kushindwa kufunga zipu ya koti lake.

Kwa msimu huu, Arsenal ipo kwenye hatari ya kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu msimu ujao kama itashindwa kubeba taji la Europa League, kwa sababu kwenye Ligi Kuu England inashika nafasi ya sita, pointi kibao kuifikia timu ya nafasi ya nne, Tottenham Hotspur.

Mmiliki wa Arsenal, Stan Kroenke alisema: “Hii ni moja ya siku ngumu kabisa kuzikabili katika maisha yote tuliyokuwa hapa. Moja ya sababu iliyotufanya tuwekeza Arsenal ni kwa sababu ya kile Arsene. Kudumu kwake kwa muda mrefu kwenye timu na kudumu kwenye kiwango kikubwa pia kunafanya pengo lake lisizibwe milele. Arsene ni kocha wa daraja la juu sana, ilikuwa vizuri kuwa naye hapa. Kila mtu aliipenda Arsenal.

Mataji matatu ya Ligi Kuu, kucheza msimu mzima bila ya kupoteza na kubeba Kombe la FA mara saba na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka 20 mfululizo hiyo ni rekodi ya kipekee kabisa.

Alibadili pia utamaduni wa klabu na soka la Kingereza kutokana na staili yake ya uchezaji. Kwa sasa akili yetu na mipango yetu ipo kuisaidia timu kumaliza vizuri msimu.”

Kikosi hicho cha Wenger, Arsenal kimetinga nusu fainali ya Europa League, Alhamisi ijayo itakipiga na Atletico Madrid katika michuano hiyo.