Martial anapoelekea kufuata nyayo za Kevin De Druyne

MANCHESTER,ENGLAND


ANTHONY Martial hana sababu ya kutetemeka kuhusu maisha yake yatakuwaje baada ya kuondoka Manchester United kutokana na Kocha Jose Mourinho kuonekana kutokuwa na mipango naye.

Juventus na Bayern Munich zote zimeonyesha dhamira ya dhati ya kutaka huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa na pengine zinaweza kufanikiwa kumnasa dirisha lijalo la usajili. Kuondokana na presha hiyo, Martial anapaswa kuwatazama wachezaji hawa ambao walibadilisha kabisa maisha yao na kuwa mastaa muhimu katika vikosi vya kwanza huko walikoenda baada ya kuonekana si kitu na Kocha Mourinho.

Leonardo Bonucci

Bonucci hakuwa mchezaji kama alivyo kwa sasa wakati anaibukia kutoka akademia ya Inter Milan, lakini kwa namna alivyo kwa sasa ni jambo linalomfanya kila kocha wa soka kuitamani huduma ya beki huyo wa kati.

Mourinho hakutaka kabisa kumtumia beki huyo. Alikuwa na uwezo, lakini Mourinho hakumpa nafasi. Bonucci alianza kupata nafasi baada ya Inter kuwa chini ya Roberto Mancini mwaka 2006, lakini chini ya Mourinho hakucheza kabisa na kuishia tu kutolewa kwa mkopo, Treviso na baadaye Pisa. Baadye akapelekwa Bari mwaka 2009 kwa kwa umiliki wa pamoja na Genoa, ambapo Diego Milito na Thiago Motta walihusika kwenye dili na kuhamia Inter. Juventus ikaamua kumchukua Bonucci mwaka 2010 na tangu hapo amekuwa beki matata uwanjani akitamba Ulaya nzima na mwaka jana alitua AC Milan.

Romelu Lukaku

Manchester United ya Mourinho ililipa Pauni 75 milioni dirisha la majira ya kiangazi ya mwaka jana kumvuta staa huyo huko Old Trafford.

Lakini, hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Mourinho kufanya kazi na mshambuliaji huyo, ambaye alimpiga bei walipokuwa pamoja huko Chelsea. Wakati anatua Stamford Bridge, Lukaku alikuwa na umri wa miaka 18 na kunaswa kwa Pauni 20 milioni akitokea Anderlecht mwaka 2011, lakini akajikuta akipata ugumu wa kupata nafasi chini ya Mourinho na mwaka 2015 akauzwa kwenda Everton.

Baada ya kufikia Goodison Park, Lukaku alicheza mpira mkubwa sana na kulifanya jina lake kuwa kubwa kiasi cha kumvutia Mourinho kwenda kumsajili tena akachezee Man United na ameshafunga mabao 27 kwa msimu huu.

Mohamed Salah

Ikiwa chini ya Mourinho, Chelsea ililipa FC Basel Pauni 11 milioni Januari 2014 ili kupata huduma ya mchezaji huyo.

Lakini, matokeo yake maisha yalikwenda kuwa magumu Stamford Bridge hakupewa nafasi na ilipofika Februari 2015, akatolewa kwa mkopo kwenye Fiorentina ya Italia na ilipofika mwisho wa msimu akapelekwa tena kwa mkopo AS Roma. Baadaye, AS Roma ikaamua kumchukua jumla staa huyo kabla ya mwaka jana kunaswa na Liverpool kwa Pauni 34 milioni.

Tangu atue Anfield, Salah amekuwa bonge la mchezaji na kuitikisa Ulaya nzima kutokana na kiwango chake ambacho kimeanza kuvifanya vigogo kama Real Madrid, Paris Saint-Germain na Barcelona kukosa usingizi kuifikiria huduma yake.

Kevin De Bruyne

Hakika yalikuwa makosa makubwa sana kwa Mourinho kuwaruhusu Salah na Kevin De Bruyne kuondoka kwenye vikosi vyake.

Wakali wote hao wawili walikuwa chini yake huko Chelsea na kama kungekuwa na uvumilivu au kupewa nafasi ya kucheza, basi mambo yangekuwa tofauti sana. De Bruyne hakuwa akipewa nafasi ya kucheza Stamford Bridge na matokeo yake akapigwa bei kwenda Wolfsburg kwa ada ya Euro 20 milioni mwaka 2014. Baada ya kutua tu kwenye kikosi hicho cha Wolfsburg, De Bruyne aliuwasha moto na kuwa staa mkubwa sana jambo liloloifanya Manchester City kuvutika na kutoa Pauni 55 milioni kuinasa saini yake mwaka 2015.

Huko Man City, De Bruyne amekuwa mtamu zaidi hasa kwa msimu huu akiwa chini ya Pep Guardiola.

Anthony Martial

Staa huyo wa Ufaransa hali yake ya mambo huko Old Trafford haipo vizuri kabisa baada ya Kocha Jose Mourinho ameonekana kumnyima nafasi hasa baada ya usajili wa Alexis Sanchez kwenye kikosi cha Manchester United.

Kwenye dirisha la Januari, Martial alihitaji sana kwenda Arsenal, lakini Mourinho aligoma kulifanya hilo kutokea na hivyo kuamua kumhusisha Henrikh Mkhitaryan kwenye dili la kubadilishana na Sanchez. Mourinho pengine anaogopa kumwachia Martial isije kutokea kile kilichotokea kwa wachezaji hao wengine hasa ukizingatia anafahamu wazi uwezo wa mshambuliaji huyo kuwa ni mkubwa sana.