Kinda aliyeaminiwa na Kocha Guardiola Etihad

Muktasari:

  • Jina lake ni Oleksandr Zinchenko na alizaliwa Desemba 15, 1996 katika mji wa Radomyshl nchini kwao Ukraine. Alianza kucheza soka katika klabu ya Youth Sporitve School Karpatiya iliyopo katika mji wao wa Radomyshl ambayo ilikuwa inafundishwa na kocha,Serhiy Boretskyi.

MANCHESTER, ENGLAND

MANCHESTER City imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England. Katika makinda ambao Pep Guardiola amewatumia msimu huu ni Oleksandr Zinchenko ambaye mashabiki walikuwa wanajiuliza ni wapi alikuwa ametokea mpaka akaaminiwa na Guardiola kucheza katika mechi muhimu za kuelekea kusaka ubingwa. Ni nani huyu kinda?

Mtoto halisi wa Ukraine

Jina lake ni Oleksandr Zinchenko na alizaliwa Desemba 15, 1996 katika mji wa Radomyshl nchini kwao Ukraine. Alianza kucheza soka katika klabu ya Youth Sporitve School Karpatiya iliyopo katika mji wao wa Radomyshl ambayo ilikuwa inafundishwa na kocha,Serhiy Boretskyi.

Akiwa kinda alikuwa akicheza kama winga wa kushoto huku ikijulikana kwamba alikuwa ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani. Baadaye klabu ya FC Monolit Illichivsk ya hapo hapo Ukraine ilikiona kipaji chake na kuamua kumchukua mwaka 2008.

Alicheza msimu mmoja tu na kutamaniwa na moja kati ya klabu kubwa nchini humo, FC Shakhtar Donetsk ambayo ilimchukua mwaka 2009. Alikuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu wa timu ya vijana ya Shakhtar katika msimu wa 2013-14 michuano ya Ligi ya vijana ya UEFA.

Katika michuano hiyo, alifunga bao la kwanza katika ushindi dhidi ya Man United hatua ya 16 bora.

Zinchenko aliichezea Ukraine katika michuano ya Euro ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na ile ya chini ya umri wa miaka 19 ambapo mara zote mbili alikuwepo katika vikosi vya timu bora ya michuano.

Kiwango chake kilizivutia klabu mbalimbali za ndani na nje ya Ukraine ambapo baadaye alikwenda kufanya majaribio na klabu ya Rubin Kazan ya Russia. Hata hivyo, hakufanikiwa kujiunga na timu hiyo na alijikuta akiishia katika mikono ya klabu ya FC Ufa ambayo ilikuwa imepanda Ligi Kuu Russia wakati huo.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Russia Machi 20,2015 akiwa na umri wa miaka 18 tu katika pambano la nyumbani dhidi ya klabu ya Krasnodar ambapo walichapwa mabao 2-0. Msimu huo aliumaliza akicheza mechi saba na kufunga mabao mawili.

Msimu wa 2015-16 ndio ambao ulimtambulisha zaidi na alicheza mechi 24 za kikosi cha kwanza katika Ligi huku mara mbili akicheza katika mechi za kombe la Russia ambapo waliishia kufungwa 2-0 katika pambano la robo fainali na CSKA Moscow ambayo ilikwenda kutinga fainali na kuchukua ubingwa.

Msimu huo alifunga mabao mawili na kupika pasi za mwisho za mabao manne huku akiisadia Ufa isishuke daraja.

Manchester City yamnasa

Julai 2016, Zinchenko alisaini katika klabu ya Manchester City kwa dau ambalo halikutajwa lakini inaaminika kwamba alisaini kwa kiasi cha pauni 1.7 milioni. Uhamisho huo uliwashangaza wengi ingawa skauti mmoja nchini Russia alidai kwamba ‘Zinchenko ni kipaji halisi’. Kabla ya hapo alikuwa akiwindwa vilivyo na Borussia Dortmund ya Ujerumani. Agosti 26, 2016 alitolewa kwa mkopo kwenda PSV Eindhoven kwa msimu wa 2016–17. Alicheza mechi yake ya kwanza Oktoba Mosi akiingia kutokea benchi katika pambano dhidi ya SC Heerenveen ambalo lilimalizika kwa sare ya 1-1.

Alirudi Manchester City katika msimu wa 2017–18 ambapo kocha Pep Guardiola alionekana kuanza kumuamini na kumpanga katika pambano la kwanza jezi ya City mnamo Oktoba 24, 2017 katika kombe la Ligi dhidi ya Wolverhampton Wanderers.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England Desemba 13, 2017 katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Swansea City ambalo walishinda 4-0. Kucheza kwake kulitokana na kuumia kwa walinzi wawili wa pembeni wa timu hiyo.

Kwanza aliumia mlinzi ghali wa upande huo, Benjamin Mendy ambaye alinunuliwa kwa dau la Pauni 37 milioni kutoka Monaco ya Ufaransa katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto. Nafasi yake ilichukuliwa na Fabian Delph ambaye naye aliumia. Bahati ikamwangukia yeye ambaye alikuwa chaguo la nne.

Avunja rekodi ya Shevchenko Ukraine

Zinchenko aliichezea Ukraine mechi ya kwanza katika pambano la kufuzu michuano ya Euro 2016 dhidi ya Hispania mnamo Oktoba 12, 2015. Alifunga bao lake la kwanza mechi za kimataifa dhidi ya Romania katika pambano la kirafiki lililofanyika Turin. Ukraine walishinda 4-3.

Zinchenko alijumuishwa kikosi cha Ukraine kilichoshiriki Euro 2016. Alicheza mechi dhidi ya Ujerumani na Ireland Kaskazini, hata hivyo Ukraine iliaga mapema.