sababu za Ronaldo kurudi man United

Muktasari:

  • Kwa sasa supastaa huyo wa Kireno anatoa huduma yake huko Santiago Bernabeu, mahali ambako amekuwa akiweka rekodi mpya kila kukicha kutokana na mambo yake ya ndani ya uwanja. Lakini, si unawajua Real Madrid huwa hawacheki cheki na mchezaji wanayemwona kwamba kiwango chake kimeshuka?

MADRID, HISPANIA

BAO lake alilowapiga Juventus limepata sifa kila kona. Mastaa kibao wa soka wamelisifu bao hilo, akiwamo Zinedine Zidane, ambaye alihitimisha kwa kusema Real Madrid ina bahati kwa kuwa na huduma ya staa huyo. Ni Cristiano Ronaldo bana!

Kwa sasa supastaa huyo wa Kireno anatoa huduma yake huko Santiago Bernabeu, mahali ambako amekuwa akiweka rekodi mpya kila kukicha kutokana na mambo yake ya ndani ya uwanja. Lakini, si unawajua Real Madrid huwa hawacheki cheki na mchezaji wanayemwona kwamba kiwango chake kimeshuka?

Jambo hilo ndilo litakalomfanya siku moja Ronaldo aondoke Real Madrid na kurudi Manchester United. Sambamba na hilo, hizi hapa sababu tano zitakazomfanya Ronaldo arudi Man United kumalizia maisha yake ya soka.

5.Kuna mtu anaitwa Asensio

Siku zote watu husema ni kazi ngumu kurithi mikoba ya gwiji ambaye alifanya kila kitu katika kikosi husika ndani ya uwanja. Lakini, mzaliwa huyo wa Palma, Asensio ameshaanza kuonyesha kwamba kuna kitu kikubwa anachoweza kukifanya ndani ya uwanja kutokana na kufanya vizuri mara zote alipohitajika kufanya hivyo.

Kiwango chake kimewafanya mashabiki wa Real Madrid hata kutuma meseji kibao kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakisema “Ronaldo wa kazi gani?”

Asensio ameonyesha ubora wake kwenye mechi hata ya El Clasico na alionyesha kiwango bora kwenye mechi ambazo staa huyo wa Kireno hakuwapo uwanjani.

Kuonyesha kwamba kuna hatima nzuri ya staa huyo, hata kocha Zidane amemsifu kijana huyo akisema anavyoweza kuutumia vizuri mguu wake wa kushoto, ukimwondoa Lionel Messi basi ni yeye Asensio.

4.Ishu ya kodi

Mashabiki wa Ronaldo walikuwa kwenye furaha kubwa baada ya kusikia ripoti kwamba Messi anaweza kufungwa miaka kadhaa jela kutokana na ishu ya kukwepa kulipa kodi. Kwa kipindi hicho hawakuwa wakifahamu kwamba hata mchezaji wao wanayempenda naye atakumbwa na sakata hilo kama lililomkumba Messi. Mara tu, Ronaldo naye akajikuta kwenye shida kama hiyo akidaiwa kukwepa kulipa kodi kiasi cha Euro 14.7 milioni zilizotokana na malipo yake ya haki za taswira zake. Kuweka mambo kuwa mabaya zaidi, hata wakala wake Jorge Mendes naye alijumuishwa kwenye sakata hilo na maofisa wa kodi wa Hispania. Kwa namna mamlaka za kodi zinavyowasumbua wanasoka mahiri huko Hispania na kuwaharibia taswira zao kwenye jamii, Ronaldo itafika wakati ataona ni heri tu kukusanya mabegi yake na kurudi Carrington.

3.Kukinai ushindani na Messi

Kitu kingine kikubwa kilichokuwa kinamfanya Ronaldo kuendelea kuichezea Real Madrid na kufanya kile anachoendelea kukifanya kila siku anapokuwa uwanjani ni ushindani wake na Messi. Ni jambo la kawaida kumsikia Messi anapiga ‘hat-trick’ leo, kesho yake Ronaldo analipa. Kitendo cha kupokezana pia tuzo ya Ballon d’Or katika kipindi cha miaka 10 iliyopita hilo ni jambo lililowafanya wachezaji hao wawili kuwa kwenye upinzani mkali na hilo lilimfanya Ronaldo kufurahia maisha yake ya kwenye soka la Hispania. Lakini, kwa mambo yanavyoonekana kwa sasa Ronaldo na Messi ni kama watu wawili ambao hawana tena upinzani ule wa wakati ule. Hata nafasi zao wanazocheza ndani ya uwanja zimekuwa tofauti kwa kipindi cha karibuni. Ronaldo anacheza zaidi mbele na Messi anaonekana kurudi nyuma zaidi.

2.Hana alichobakiza Real Madrid

Si jambo lenye kificho kwamba Ronaldo ameshinda kila kitu katika maisha yake aliyokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid. Amebeba mataji yote makubwa aliyostahili kubeba akiwa mchezaji wa timu hiyo yenye maskani yake Bernabeu. Kutokana na hilo, utafika wakati akaamua kuachana na maisha ya timu hiyo na kuna dalili zote atakwenda zake Old Trafford.

Man United, Ronaldo hatakuwa mgeni kwani tayari ameshaifungia timu hiyo mabao 118. Kutokana na uwezo wake wa kufunga walau kuanzia mabao 30 na kuendelea, kitu ambacho anaweza kukifanya kwa misimu minne zaidi kutoka sasa, hilo linaweza kuwasukuma Man United kumkaribisha kwenye kikosi chao ili akawasaidie kwenye mikakati yao ya Ligi Kuu England. Lakini, Ronaldo pia atahitaji kurudi Old Trafford ili akaweke rekodi ya kuwa kinara wa mabao wa kihistoria kwenye kikosi hicho baada ya kukamilisha kazi hiyo Real Madrid.

1.Anahitaji kupendwa

Hakuna siri kwamba Man United imekuwa sehemu muhimu sana katika moyo wa supastaa huyo. Hilo linatokana na mashabiki wa timu hiyo ya Old Trafford kuendelea kumpenda Ronaldo licha ya kwamba aliondoka kwenye timu yao akiwa kwenye kiwango bora kabisa.

Man United wanampenda Ronaldo hata kama aliwafunga mara kadhaa alipokutana nao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hawajawahi kuacha kumpenda mwenyewe anaheshimu hilo.