Banda ana vitu adimu bwana!

Muktasari:

  • Banda alitua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Ijumaa iliyopita na kabla ya kwenda kujiunga na kambi ya Taifa Stars, alikwenda moja kwa moja zilipo ofisi za Mwananchi Communications Ltd, wazalishaji wa gazeti hili la Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen.

UNAPOZUNGUMZA na beki wa Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Abdi Banda kauli yake kubwa anataka ‘kuwasurprise’ Watanzania. Hata hivyo, ‘surprise’ hiyo iko vipi?

Banda alitua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Ijumaa iliyopita na kabla ya kwenda kujiunga na kambi ya Taifa Stars, alikwenda moja kwa moja zilipo ofisi za Mwananchi Communications Ltd, wazalishaji wa gazeti hili la Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen.

Supraizi ya kwanza ni baada ya kufika ofisini hapo, kila aliyemtazama alimwona tofauti na yule aliyekuwa anaichezea Simba msimu uliopita. Waliona amebadilika sana.

Banda wa Baroka ni tofauti, ukimwangalia kimwonekano kuanzia mavazi, kwa sasa ni mzee wa suti na mwenyewe anasema yale mambo ya kuvaa vipensi ama jinsi za kuchanika kwake hayana nafasi.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake tu unabaini kichwani yuko sawa.

Mbali na kubadili mwonekano wa nywele zake kwa kusokota na kupaka rangi ya njano inayoonekana kwa mbali, jamaa anajua kujieleza na kila anachokizungumza kinabeba uzito mkubwa na anajiamini kweli.

ATOA SAPRAIZI

Alipofika tu getini alipokelewa na askari waliokuwepo pale, hapo ndipo alipowashangaza watu alipokuwa akisaini daftari la wageni.

Ilikuwa hivi. Wakati anasaini daftari hilo aliwafanya watu washtuke kidogo. Wengi wamezoea kumwona akitumia mguu wa kushoto wakati akicheza mpira, lakini kumbe hawakujua hata kuandika na kufanya mambo mengine hutumia pia mkono wa kushoto. Hata kusaini daftari hilo alitumia mkono huo.

ANAWAZA KUFIKA MBALI

Hata hivyo, katika maneno yote aliyozungumza kubwa ni namna alivyojipanga kusonga mbele kupitia soka.

Banda, ambaye anaweka wazi yuko chini ya kampuni moja ambayo inamtafutia kila kitu ikiwemo timu na yeye kazi yake ni kucheza tu hivyo, kwa nafasi hiyo amesisitiza siku si nyingi mtamsikia England au Hispania.

“Mpaka sasa zipo timu tofauti zimekuja zikihitaji huduma yangu, lakini binafsi siwezi kufanya uamuzi hadi watu wanaosimamia waseme nini natakiwa kufanya,’’ anasema Banda ambaye anaweka wazi, kampuni hiyo alikuwa nayo kabla ya kwenda kwenye mashindano COSAFA Afrika Kusini.

“Najiamini na ninachokiamini kuna siku nitafanya makubwa na ‘kuwasurprise’ wengi, ndio kwanza nina miaka 22 hivyo, nina muda wa kufanya makubwa zaidi.”

MAISHA YA BAROKA

Banda, ambaye alianza maisha rasmi ya Afrika Kusini alipojiunga na Baroka msimu huu akitokea Simba aliyoichezea kwa misimu mitatu, anasema: “Maisha ya Baroka ni mazuri, ingawa awali si unajua ugeni, nilikuwa muoga kidogo na katika kujifunza kuzoea mazingira, nilijifanya mjinga kwanza ili nione kipi cha kufanya nifanikiwe na kipi naweza kupotea.”

WATANZANIA HAWANA UCHUNGU

Kwa Banda inamuumiza tena inamuumiza kwani tangu alipopata nafasi ya kwenda Afrika Kusini ni mchezaji mmoja tu wa Mbao FC, ambaye hakumtaja jina, ndiye amekuwa akimpigia simu akimsumbua kama anaweza kumtafutia nafasi ya kucheza huko.

“Watanzania hatuna uchungu wa maisha tunaona bora liende tu tofauti na wenzetu wa mataifa mengine kama Nigeria na kwingine. Niko huko, kwa kipindi chote sijaona wachezaji wakiniuliza umetumia mbinu gani na sisi tutoke au tufanyie mpango wa kucheza huko,” anasema Banda na kufafanua hawamsumbui yeye na hata wengine wa nje kwa sababu wanawasiliana na wenzake na wanasema hivyo.

“Ni mchezaji mmoja tu wa Mbao ndiyo huwa nazungumza naye na ameonyesha nia yake ya kutaka kucheza kule. Ligi ya Afrika Kusini ina madaraja matano na mashindano mengine tofauti, kama hukupata la kwanza, yapo hayo mengine ya chini unaweza ukajaribu maisha, lakini hakuna.”

ULIMWENGU, SAMATTA WALIMTIA ‘KICHAA’

Banda mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya beki ya kushoto, kiungo na beki ya kati anasema, katika safari yake ya maisha ya soka, wachezaji ambao wamempa changamoto ni Thomas Ulimwengu ‘Kumbakumba’ na Mbwana Samatta kutokana na namna wanavyopata heshima kila wanapotua nchini.

“Kucheza nje ya nchi kuna faida nyingi, kwanza ni heshima kwako na Taifa, pia unabadilisha maisha yako kwa jumla kuanzia kipato na mambo mengine kwa sababu, unakutana na watu tofauti katika maisha,” anasema Banda, ambaye alianza safari ya maisha yake ya soka akiwa na African Sports aliyoichezea kwa miezi sita, Coastal Union miaka mitatu na baadaye Simba aliyoichezea kwa misimu mitatu.

“Nilikuwa naona walivyokuwa wanapokewa na wao wenyewe wanavyoishi, nilikuwa natamani na niliweka malengo kuwa lazima nikajaribu huko.”

PESA ANAZOLIPWA NI MARA TANO YA SIMBA

Banda amesema hakufanya makosa na anajisikia furaha baada ya kuamua kwenda kucheza nje kwa sababu hata kipato anachokipata kutokana na kazi yake ni mara tano ya kile alichokuwa analipwa Simba.

“Kusema kweli mambo yangu si mabaya na pesa ninazopata zinaweza kuzidi mara tano ya ile niliyokuwa nalipwa Simba,” anasema Banda.

KUMBE NI BABA WA FAMILIA

Kiraka huyo ambaye kwao wamezaliwa watano na yeye akiwa ni wa pili ni kama baba wa familia, yaani kwa mama na ndugu zake kwa sababu ndiye anayepambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanaishi.

“Kitu kikubwa ni familia yangu, ukiniumiza mimi umeumiza sehemu kubwa ya familia yangu wanaoishi kwa kunitegemea,” anasema Banda ambaye anamtaja Abdul Boznia ndiye aliyechangia kubadili sehemu kubwa ya maisha yake na ni kama mzazi wake tangu anasoma mpaka maisha ya soka.

Amesisitiza katika kumtengenezea maisha mdogo wake Omary Banda anayecheza Azam FC ni kumtafutia timu nje na amepanga msimu ujao ambebe aende naye Afrika Kusini.

MAHUSIANO

Banda amekiri ana uhusiano na mdogo wa Ally Kiba na Abdul Kiba, aitwaye Zabibu Kiba na amepanga kumuoa mwaka huu.

“Kwa takribani miaka mitatu niko na uhusiano na Zabibu na hiyo ni kawaida kwa sababu mimi ni mwanamume na mwishowe natakiwa na familia yangu,” anasema Banda anayeweka wazi sababu ya kuwa pamoja kwa kipindi kirefu ni binti huyo ni masikilizano.