SIYO ZENGWE: Nadhani Ninje alistahili zaidi timu ya vijana ya klabu

KWA mtu ambaye alishuhudia mechi ya juzi baina ya Timu za Taifa za Tanzania, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, atasema nimeandika safu hii kwa sababu ya matokeo. La hasha!

Nimeongeza tu hii aya ya kwanza ili kuweka bayana kuwa nilichoandika nilikiamini kabla ya matokeo ya juzi Ahamisi katika Uwanja wa  Kenyatta mjini Machakosi.

Kwa takriban siku sita nilikuwa nakiifuatilia timu yangu ya taifa ya kwa upande wa Tanzania Bara, ambayo sasa inashiriki michuano iliyofufuliwa ya Kombe la Chalenji yanayoendelea Kenya.

Hasa nimekuwa na hamu ya kusikiliza falsafa za Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje, kwa kuwa sijamsikia sana katika anga za soka, zaidi ya wakati ule alipoitwa na Mshindo Msola katika timu ya taifa, miaka mingi nyuma.

Nilikuja kushtuka kwamba kumbe ni Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, kazi ambayo alipewa bila kelele za kawaida za kutangazwa rasmi kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Suala hilo ndilo lililonifanya nimfuatilie kwa makini kutaka kumjua zaidi kama ni kocha sahihi wa timu yangu ya Tanzania Bara kulingana na falsafa zake.

Kabla ya kwenda Kenya nilimsikia Ninje akizungumzia maandalizi ya timu yake na kudokezea falsafa yake. Kimsingi nilimsikia akizungumzia masuala ya msingi ambayo kocha yeyote angezungumzia, hasa wa timu ambayo inakua, yaani ya vijana.

Na juzi baada ya mechi na Libya, nilimsikia tena akizungumzia mchezo huo na maandalizi kwa ajili ya mechi inayofuata dhidi ya Zanzibar. Alizungumzia recovery ya timu, yaani muda wa kupumzika ili kurudisha nguvu na jinsi ya kucheza baada ya kupokonywa mpira ili kuurudisha kwenye timu.

Pengine nitakuwa nimeangalia mambo machache sana kuweza kumchambua kocha huyo. Labda ni mzuri, lakini hajui azungumze nini kabla na baada ya mechi au anachokizungumza ndicho anachokifanya.

Kocha wa timu ya taifa ni kama mratibu wa wachezaji tofauti walio tayari kimchezo, yaani wamekamilika, wana utimamu wa mwili na wanaitwa kwa sababu wanaweza kutumika kwa aina fulani ya mchezo anaoutaka kocha, na si wanaohitaji muda ili kukua na kuwa wazuri.

Kwa hiyo, Ninje anaposema kwamba timu ilifanya vizuri katika kiungo, ila bado haikuwa nzuri katika kutafuta mpira baada ya kupokonywa mipira, anamaanisha kuwa atakapocheza mechi ya pili atakuwa na tatizo jingine la kupata mabao ya kufunga na hivyo atahitaji muda wa kulifanyia kazi tatizo hilo.

Hii inamaanisha kuwa, baada ya mechi ya tatu atakuwa na timu iliyokamilika na hivyo mechi zinazofuata atakuwa akishinda tu kwa kuwa ameshafanyia kazi udhaifu wote aliouona katika kikosi chake.

Kwa kuwa kocha wa timu ya taifa ni mratibu tu, kazi yake kubwa ni kuangalia ni wachezaji gani wanafaa kwa aina ya mchezo anaoutaka. Wako timamu?

Maana yake ni kwamba anapochambua mchezo baada ya mechi, anaangalia pia udhaifu wa mfumo aliotumia upo sehemu gani na kama ni mchezaji ndiye aliyesababisha mfumo usifanye vizuri, hana budi kumzungumzia na kueleza dawa ni nini.

Sijamuona wala kumisikia Ninje akizungumzia mchezo wa timu yake kama kocha aliyekusanya wachezaji timilifu anaotaka wacheze aina fulani ya mchezo anaoutaka au watumie mbinu fulani inayofaa kwa mechi fulani.

Kocha anayesema kwamba ameanza kuijenga timu sehemu, mfano kwenye kiungo halafu ahamie sehemu ya ngome ya ulinzi, timu yake isipofanya vizuri ni lazima atarudi kuzungumzia yale masuala yaliyozoeleka kuwa wachezaji bado hawana uzoefu, bado hatujaendelea kisoka na mengine mengi.

Nadhani, Ninje angefaa zaidi kufundisha timu ya vijana ya klabu ambayo atakuwa na muda mwingi wa kufundisha idara tofauti tofauti hadi timu ikamilike na si timu ya taifa ambayo anakuwa na siku tatu hadi tano za maandalizi kabla ya mechi.

Hapo ndipo pangemfaa zaidi kabla ya kupiga hatua na kufundisha timu za madaraja tofauti kisha kupewa timu kubwa na nyingine hadi kufikia hadhi ya kukabidhiwa timu ya taifa.

Kocha wa taifa hawajibiki kujenga timu, bali kukusanya vipaji tofauti kulingana na aina ya mchezo anaoutaka na aina ya mpinzani anayekutana nayo.

Huko tunakokwenda, tutafikia sehemu klabu zitakataa kutoa wachezaji kwa zaidi ya siku tano kwa ajili ya kuipa timu ya taifa muda wa kutosha wa maandalizi kwa kuwa kanuni za Fifa zinawalinda na wana mantiki kwa kuwa wao ndio wanawalea wachezaji, wanawalipa na kuwatibu, hivyo wanayo haki ya kuwakatalia pale wanapoona hakuna haja na kanuni zinawaruhusu.

Katika mazingira hayo, tunahitaji kocha wa timu ya taifa anayeweza kuteua wachezaji kamilifu na kuunganisha vipaji tofauti, si kuwaita kwa ajili ya kuanza kuwafundisha mpira.