STRAIKA WA MWANASPOTI: Kuchaguana kwa kujuana kunaturudisha nyuma

Muktasari:

Viongozi wetu wameweka tumbo zao mbele kwanza hadi kuleta ubinafsi katika vikosi hivyo.

Timu zetu za taifa kwa mara nyingi haswa nchini Kenya zimekuwa hazifanyi vyema katika mashindano ya barani Afrika kisa na maana vikosi vimekuwa vikichaguliwa kulingana na vile watu wanajuana.

Viongozi wetu wameweka tumbo zao mbele kwanza hadi kuleta ubinafsi katika vikosi hivyo.

Katika soka ndugu zanguni wakati wowote ule ukileta urafiki katika kazi basi ni wazi bayana hautafaulu kwa jambo ambalo unaenda kulitenda.

Sikatai kwamba unaweza kuwa na marafiki na ukataka kuwajuim,usha katika kazi zako, lakini cha msingi ni kuwa lazima hao marafiki zako wawe na ufundi wa hali ya juu.

Kwa muda mrefu vikosi vyetu vya timu ya Taifa vimekuwa vikichaguliwa kwa mapendeleo sana.

Nasema hivyo kwa sababu ya uzoefu nilionao katika soka. Mimi siku hizi ni mwandishi na mchanganuzi wa masuala ya soka nchini na kanda hii ya Afrika baada ya kustaafu kucheza soka.

Maisha yangu yote yamekuwa ni ndani ya soka ndugu zanguni.

Nilipata fursa ya kupata mialiko kadhaa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Soka nchini Kenya mara kadha wa kadha.

Katika muda huo wote, kuna mambo mengi nilijifunza na ni mengi niliyaona.

Hapa niotaweka bayana kuwa sio kwamba timu zetu ni mbovu ndio maana hatufanyi vizuri kimataifa, hapana.

Ndugu zanguni shida kubwa ni makocha wetu na viongozi wetu kuwa na ubinafsi katika harakati za kuchagua kikosi cha timu ya Taifa.

Kwa jinsi inavyofanyika, mara nyingi utaona wale wachezaji wanaofaa kusafiri na timu hawasafari na mtu unabaki unajiuliza imekuwaje.

Wale wachezaji ambao wanastahili kuwemo katika kikosi cha timu ya Taifa wengi huachwa kwa sababu makocha wetu na viongozi wetu wao huwa na mapendeleo fulani.

Vikosi vyetu vimejaa ubinafsi na leo hii nitawaambia wazi kuwa hiyo tabia sio eti ilianza juzi. Laa ni tabia ambayo imekuwa tangu jadi.

Nimeona wachezaji wengi sana wakikatwa kutoka kwa kikosi kisa kwa sababu tu kocha ama kiongozi fulani anataka mchezaji fulani ndio asafiri.

Utapata aidha huyo mchezaji ni rafiki yake ama anacheza katika timu yake. Wachezaji wengine wamekuwa wakijipigia debe ili waitwe katika vikosi hivyo.

Utapata kuwa yeye anacheza soka la kulipwa nje ya nchi na ukiangalia kwa undani huyo mchezaji katika klabu yake hachezi.

Sasa ndugu zanguni mchezaji kama huyo unamuita kikosini kufanya nini?

Kuna siku kwa kweli nilikasirishwa sana na kocha fulani ambaye sitamtaja jina hapa lakini mojawapo ya makocha ambao wamekuwa wakiidhalilisha timu ya taifa ya Harambee Stars.

Nilikuwa kambini,mchezaji fulani akaitwa kikosini. Alikuwa na jeraha baya sana, jeraha ambalo wiki yote nzima hakufanya mazoezi na timu ya taifa lakini alikuwa kambini tu.

Cha kushangaza ndugu zanguni alisafiri na kikosi hicho cha timu ya taifa na cha kuudhi zaidi hata kuko timu ilikokwenda hakuchezeshwa.

Ndugu zanguni hebu niambieni swala kama hilo ni la ungwana kweli? Wachezaji waliokuwa fiti kabisa walichujwa, wachezaji ambao wangesaidia timu. Kisa na maana tu ni kwamba alikuwa rafiki wa kocha.

Kinachoudhi zaidi, alikuwa amelipiwa tiketi ya ndege kuja kujiunga na timu ya taifa. Hiyo mechi Kenya ilipoteza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Nigeria.

Hebu angalia hapa, nchi imepoteza hela kulipia mchezaji ambaye tayari ni majeruhi kwa kumlipia tiketi ya kuja nchini na kurejea alikotoka.

Kuongezea, wamempandisha ndege kwenda Nigeria na ni majeruhi. Hakucheza. Mchezaji kama huyo anaisaidiaje taifa. Makocha kama hawa ndugu zanguni ndio wamekuwa wakiingusha nchi yetu kila kukicha.

Kuongezea kwa hayo viongozi wetu wamekuwa pia wana changia saana kwa kudidimia kwa umaarufu wa timu zetu za kitaifa.

Ukiangalia miaka ya huko nyuma, wachezaji ambao walikuwa wanaitwa katika kikosi wote walikuwa wanastahili kuitwa. Walikuwa wanafaa kabisa kutokana na viwango vyao.

Lakini siku hizi wachezaji wanaitwa kikosini kulingana na vile wanajuana na makocha wetu na viongozi wetu. Kila kiongozi ambaye yuko katika ofisi kuu anataka mchezaji wake aitwe.

Na hiyo tabia imesheheni katika vikosi vyetu vyote vya timu zetu za Taifa kuanzia timu zile ndogo hadi timu kubwa. Wale wachezaji ambao wanastahili kuwa katika vikosi hivyo hawapo.

Tunazidi kujaza watoto wa marafiki zetu ndani ya vikosi hivyo kwa sababu zetu za kibinafsi. Mtindo huo ukiwa utazidi kuendelea ndugu zanguni hamna pahali popote tutakapo enda. Mpende msipende.

Kilicho cha muhimu hapa ni viongozi wetu kubadili namna ya kufanya kazi na kuachana na mtindo huo ambao kwa hakika umekuwa ukiturudisha nyuma mno. Kila kiongozi anapaswa kuona aibu kwa hili.