AMERUDI

Muktasari:

Saida Karoli anasema anarudi kwa sasa na mashabiki wake waliokunwa na kazi zake za nyuma za nyimbo asilia wajiandae kupata burudani.

NI kweli kwa muda mrefu alikuwa kimya kiasi cha mashabiki wake kudhani ameachana na muziki, lakini Diamond Platinumz akaja kumfufua kimtindo kwa kuurejea wimbo wake wa ‘Chambua Kama Karanga’, akiupa jina la ‘Salome’.

Saida Karoli anasema anarudi kwa sasa na mashabiki wake waliokunwa na kazi zake za nyuma za nyimbo asilia wajiandae kupata burudani.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kufanya mahojiano naye na kufunga mambo mengi ikiwamo mipango yake ya kurejea kivingine kwenye ‘gemu’, hebu msikie mwenyewe anachokisema katika mahojiano hayo mafupi:

KATOKA MBALI

Saida anasema muziki ameuanza kitambo na ndio maana inakua vigumu kwake kuachana nao kwa sasa.

“Nimekulia katika mikono ya watu wengi enzi zile kabla ya ajali ya MV Bukoba nilikuwa maarufu kwa kuimba muziki wa asili, kwani nilianza nikiwa na umri wa miaka mitano.”

Saida alianza kusikika akiimba muziki wa Lugha ya Kihaya miaka 15 iliyopita lakini hata alipoboresha muziki wake, ulivuma kimataifa na kufika mbali zaidi.

Mwimbaji huyo anasema anatarajia kuadhimisha miaka hiyo katika muziki Julai Mosi mwaka huu na kuongeza kuwa kama kila kitu kingekuwa kimekaa sawa kwake kwa sasa hakuna mwanamuziki yeyote wa kike nchini angemfikia.

KACHOKA KUPIGWA

Saida anasema kwa kipindi alichoamua kuingia katika muziki kama ajira alijikuta akirudi kwao mikono mitupu, kutokana na kushindwa katika baadhi ya mambo.

Wakati akitambulisha ujio wake rasmi kwa video ya Wimbo wake ‘Orugambo’ alioutambulisha katika futari aliyoiandaa usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita, Saida anasema kutokusimamiwa vizuri kimuziki na kutokujua soko kulimrudisha nyuma kwa vile watu walimtumia kama mrija kumpiga fedha.

Anasema muziki alioufanya kipindi cha nyuma ulimpa umaarufu pasipo fedha, hivyo kujikuta akirudi katika muziki wa awali ambao alianza kuufanya tangu akiwa na umri wa miaka mitano.

“Wazazi wangu waliponituma nije mjini kutafuta, nilikuja, nikafanya muziki, nikajulikana na kuvuma kimataifa, lakini kwa bahati mbaya nilirudi mikono mitupu. Safari hii sitaki nirudi nilikotoka nataka hata nyumbani waone Saida si yule wa mwanzo, nimejifunza kutokana na makosa,” anasema.

KOLABO KAMA KAWA

Saida anasisitiza kwa upande wa wasanii wa muziki kushirikiana naye kwani hahitaji chochote kwa sasa kwani nia yake ni kujijenga kimuziki.

Anasema yupo tayari kufanya kazi na yeyote kwani anahitaji kufanya muziki wa kimataifa ili aweze kukitumia kipaji chake vilivyo kuleta manufaa katika nchi.

“Wasanii mwenzangu naomba niwe muwazi sihitaji pesa yoyote, sihitaji gari la kifahari hata bajaji napanda, naomba tushirikiane ili kuuwezesha muziki wetu uvuke kimataifa malengo yangu sasa yapo mbali sana naomba ushirikiano.”

MEDIA YAMRUDISHA

Saida anasema katika kipindi chote alichokuwa mbali na muziki, aliviona vyombo vya habari kama maadui zake, hakuweza kuvisogelea na hata akipigiwa simu hakuzipokea.

Anasema hata hivyo, kadiri alivyozidi kuisha kimuziki bado vilimtafuta na kumpa thamani aliyostahili, alijiuliza maswali mengi akagundua kwamba bado ana thamani kubwa katika muziki.

“Vyombo vya habari vimenifuata nimejificha kwenye shimo, nimejificha kwenye nyumba na kwingineko vinanifuata maana nilikuwa naona aibu nionekane vipi kwenye jamii,” anasema na kuongeza:

“Kwa mara ya kwanza natafutwa ilivumishwa kwamba nimekufa, vyombo vya habari vilinipigia simu nikiwa Mbeya vijijini napiga ngoma nimechoka, nimeisha napanda Fuso, natembea kwa miguu kwenda sokoni jina lilishakuwa kubwa, lakini kila nikiangalia kila mtu amenitupa, ila vyombo vya habari bado vilinithamini. Kwa hakika navithamini kwa sasa kwani vimenifufua upya.”

HAACHI MUZIKI NG’O

Mkali huyo wa Chambua Kama Karanga anasema hatarajii kuacha muziki kwa siku za karibuni kwani ni kazi ya maisha yake.

Anasema alipokuwa akiimba awali wengi walimshangaa, wengine walimkubali na wapo waliomkataa kwa kusema ‘ mtoto huyu ameharibikiwa’, lakini yeye alisonga mbele.

“Sitarajii kusema kwamba naacha muziki, sitarajii kusema kwamba nastaafu muziki kwani ni maisha yangu, nasisitiza kwamba nimenyanyuka tena kwa mara nyingine naomba mnibebe, nisonge mbele,” anasema Saida.